HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

August 20, 2026

SPIKA ZUNGU AKUTANA NA BALOZI WA SERBIA, WAZUNGUMZIA KUIMARISHA USHIRIKIANO

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu (Mb), amefanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Serbia nchini Tanzania, Mhe. Jovica Topalović, jijini Dodoma, ambapo viongozi hao wamejadili hatua za kuendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano wa muda mrefu na wa kirafiki kati ya Tanzania na Serbia.


Katika mazungumzo hayo, Mhe. Spika na Mhe. Balozi wameeleza dhamira ya nchi hizo mbili ya kuupa msukumo mpya ushirikiano uliopo, hususan kupitia diplomasia ya kibunge, ikiwemo kuimarisha mahusiano kati ya Mabunge ya Tanzania na Serbia, kubadilishana uzoefu na maarifa.



Katika mazungumzo hayo, Mhe. Spika alimpongeza Mhe. Balozi pamoja na Serikali ya Serbia kwa uamuzi wa kufungua Ubalozi katika Jiji la Dodoma. Pia, alipongeza nia ya Serikali ya Serbia ya kujenga jengo la Ubalozi katika Mji wa Serikali Mtumba. Kwa upande wake, Mhe. Balozi aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuipatia Serbia kiwanja kizuri katika Mji wa Serikali na kueleza kuwa maandalizi ya kuanza ujenzi wa jengo la Ubalozi yanaendelea.


Aidha, viongozi hao wamejadili fursa za kupanua ushirikiano katika maeneo yenye maslahi kwa pande zote mbili, ikiwemo elimu, biashara, utalii na michezo.


Tanzania na Serbia zimeendelea kudumisha uhusiano wa kirafiki uliojengwa katika historia ya pamoja, kuheshimiana na ushirikiano wa kimataifa, huku pande zote mbili zikionesha dhamira ya kuufanya uhusiano huo uwe na manufaa zaidi kwa wananchi wa mataifa hayo.



No comments:

Post a Comment

Pages