Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa wito kwa wawekezaji wa kimataifa na taasisi za fedha za maendeleo kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo nchini, ikisisitiza kuwa juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi lazima ziendane na mabadiliko ya kiuchumi na uboreshaji wa maisha ya wananchi.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, baada ya Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Jukwaa la Kimataifa la Fedha za Mabadiliko ya Tabianchi (Private Climate Finance Community), uliofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York, Marekani ikiwa ni sehemu ya Mikutano ya Athari za Maendeleo Endelevu 2026 (SDIM26) inayoendeshwa na Baraza la Uchumi la Dunia (WEF).
.jpg)
Mhe. Munde alisema kuwa Tanzania imejipanga kikamilifu kugeuza changamoto za kimazingira kuwa fursa za kiuchumi kupitia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
“Tanzania inaamini kuwa ufadhili wa kulinda sayari yetu na ufadhili wa maendeleo lazima viende sambamba, kwa nchi zinazoendelea, hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi lazima zisaidie utengenezaji wa nafasi za kazi, usalama wa nishati na chakula, miundombinu vumilivu, pamoja na ukuaji wa viwanda,” alisema Mhe. Munde.
Mhe. Munde alisema katika kuelekea lengo la kuwa na uchumi wa kipato cha juu cha kati ifikapo mwaka 2050, Sekta Binafsi inatarajiwa kuwa injini kuu ya mabadiliko hayo kwa kuchangia takriban asilimia 70 ya uwekezaji wote unaohitajika, huku sekta ya umma ikiendelea kuweka mazingira wezeshi, sera thabiti na miundombinu muhimu kwa maendeleo.
Alisema Tanzania inakaribisha jumuiya ya kimataifa, taasisi za bima, benki na mashirika ya maendeleo kushiriki katika kufanikisha Dira hiyo ili
kujenga uchumi wa thamani ya dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050, pamoja na kuinua ustawi wa wananchi kwa kufikisha wastani wa kipato cha mwananchi hadi takribani dola 7,000 kwa mwaka.
‘‘Dhamira hii imepokelewa vyema na washirika wa maendeleo tuliokutana nao,
hoja muhimu iliyojitokeza ni namna ambavyo sekta binafsi imehusishwa katika maandalizi na utekelezaji wa miradi itakayotupeleka kwenye uchumi tunaoulenga ambapo tuliwaeleza namna Serikali inavyoendelea kuandaa utaratibu wa kuwashirikisha wadau wa sekta binafsi ili wawe sehemu muhimu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,’’ alifafanua Mhe. Munde.
Alisema kuwa Tanzania inaimarisha uratibu wa fedha za tabianchi na kutengeneza mazingira wezeshi kwa wawekezaji kupitia uoanishaji wa uwekezaji wa umma, ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), na matumizi ya rasilimali za umma kupunguza vihatarishi vya uwekezaji.
‘‘Tanzania ina maeneo makuu ya uwekezaji endelevu na wa kimkakati yanayojumuisha nishati mbadala kama umeme wa upepo, jua na maji, kilimo hifadhi kinachohimili mabadiliko ya hali ya hewa, ujenzi wa miundombinu vumilivu ya usafirishaji na maji, maendeleo ya miji endelevu yenye mipango miji ya kisasa na usafiri wa kijani pamoja na miradi ya hifadhi ya mazingira inayolinda mifumo ya ikolojia huku ikitengeneza mapato,’’ alisema Mhe, Munde.
Aidha Mhe Munde alitoa rai kwa Benki za Maendeleo za Kimataifa na Taasisi za Fedha za Maendeleo kutoa usaidizi wa mapema katika maandalizi ya miradi, upatikanaji wa ruzuku, na fedha za muda mrefu kwa sarafu ya ndani ili kupunguza athari za mabadiliko ya fedha za kigeni.
Msisitizo mkubwa uliotolewa ni kwamba mipango yote inayohusu mazingira na mabadiliko ya tabianchi ni muhimu kushirikisha wadau wote na iwe na uratibu mzuri ili kuepuka taasisi mbalimbali kuandaa mipango mingi inayolenga jambo lilelile, kwani hali hiyo husababisha kurudia kazi na kupunguza ufanisi wa utekelezaji.
Mhe. Munde alisisitiza wawekezaji na wadau wa maendeleo kujihusisha mapema na taasisi za ndani ili kushirikiana katika kuwekeza kwenye miradi inatoa ajira za staha na kuacha thamani endelevu nchini.




No comments:
Post a Comment