📍 CCM kupitia mwenyekiti wa mkoa, Yawafariji
Na Mashaka Mhando, Handeni
KILIO, hofu, na sintofahamu vimetanda miongoni mwa wakazi wa Kitongoji cha Kwedifunyela, Wilayani Handeni, kufuatia tukio la kutisha ambapo nyumba sita za familia tofauti ziliteketea kwa moto kwa wakati mmoja, usiku wa manane.
Tukio hilo la aina yake lilitokea Septemba 18, majira ya saa tisa usiku, ambapo moto huo uliozuka kwa kasi uliteketeza kila kitu ndani ya nyumba hizo, huku waathirika wakiambulia kuokoa maisha yao pekee.

Kutokana na mazingira tata ya moto huo kuwaka kwenye nyumba sita zilizo maeneo tofauti lakini kwa wakati mmoja, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa, Rajabu Abdallah, ameiagiza Serikali kufanya uchunguzi wa haraka na wa kina.

"Jambo la kujiuliza ni kwamba nyumba hizi zote zimeungua kwa wakati mmoja. Zingekuwa zimeongozana tusingekuwa na maswali, lakini zipo maeneo tofauti. Nimeielekeza Serikali ufanyike uchunguzi wa kina... wote waliohusika watiwe kwenye mikono ya sheria," aliagiza Abdallah akiwa kwenye mkutano wa hadhara Kijiji cha Mkata Mashariki.
Ili kuwafariji waathirika walioachwa bila makazi wala chakula, Abdallah aliongoza harambee ya papo kwa hapo na kuchangia Shilingi milioni tano.
Michango mingine ilitoka kwa Mbunge wa Handeni Vijijini, Charles Sungura (Shilingi milioni 2.5), Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Tanga, Mwanaisha Ulenge (Shilingi milioni moja), na Mbunge wa Bumbuli, Ramadhani Singano (Shilingi milioni moja), hivyo kufanya jumla ya michango hiyo kufikia Shilingi milioni 9.5.
Akithibitisha kuanza kwa msako huo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi, alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi mkali na linafuatilia kila dokezo ili kubaini ukweli.
"Bado tunaendelea na uchunguzi wa kina. Hadi hivi sasa hakuna mtu yeyote tunayemshikilia, lakini uchunguzi unaendelea na wakati wowote tutafikia mahali pazuri. Endapo itabainika moto huo umesababishwa kwa makusudi, sheria itachukua mkondo wake," alisisitiza Kamanda Mchunguzi.
Akisimulia mkasa huo kwa masikitiko makubwa, Omari Mganga, kaka wa mmoja wa wahanga (Salim Mganga), alisema ilibidi ahatarishe maisha yake kuingia kwenye moto kumwokoa mdogo wake aliyekuwa akijaribu kuokoa mali zake huku nyumba ikiteketea.
"Nilipofika niliambiwa yuko ndani, niliamua kuingia kumuokoa kwa sababu vitu vinaweza kununuliwa lakini maisha hayawezi. Tulikumbwa na cheche za moto usoni, lakini tulifanikiwa kutoka salama huku hatukuokoa kitu chochote," alisema Mganga.
Naye shuhuda wa tukio hilo, Ramadhan Abdallah, alisema taharuki iliongezeka pale walipokuwa wakijaribu kuzima moto mmoja, na ghafla kupokea taarifa kuwa kuna nyumba nyingine inawaka mtaa wa pili ndani ya kata hiyo hiyo, jambo lililowachanganya kutokana na kasi ya moto huo uliochochewa na kuezekwa kwa nyasi.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Salum Nyamwese, ambaye aliupokea msaada huo wa Shilingi milioni 9.5 kwa niaba ya wahanga, aliwashukuru viongozi hao na kuwahakikishia wananchi kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya haitalala hadi chanzo cha tukio hilo kibainike.





No comments:
Post a Comment