Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MKUU wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuwa mdau muhimu katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha sekta ya elimu wilayani humo.
Mkuu huyo wa Wilaya alitoa pongezi hizo wakati wa hafla ya kupokea msaada wa meza 60 na viti 60 uliotolewa na Benki ya CRDB kwa ajili ya Shule ya Sekondari Kibweheri, iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.
Alisema CRDB imekuwa ikishirikiana na Serikali kwa kutoa misaada na michango mbalimbali inayolenga kuboresha miundombinu ya elimu katika shule za msingi na sekondari.
“Mara kadhaa mmekuwa mkitukimbilia na kutupa misaada na michango mbalimbali kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya sekta ya elimu. Tunawashukuru sana CRDB kwa michango yenu,” alisema.
Aidha, aliipongeza benki hiyo kwa kuendelea kushiriki katika shughuli na mikakati mbalimbali ya Serikali, ikiwemo elimu, mazingira na afya, akisema mchango huo unaongeza nguvu katika utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa jamii.
Alisema Serikali wilayani Ubungo inatambua mchango wa CRDB katika kurejesha sehemu ya faida kwa jamii na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano ili miradi inayotekelezwa na benki hiyo iweze kuleta tija kwa wananchi.
Kwa upande wake, Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Pwani, Muhumuliza Buberwa, alisema benki hiyo kupitia CRDB Bank Foundation ina utaratibu wa kutenga sehemu ya faida inayopatikana kwa mwaka kwa ajili ya shughuli za kurejesha kwa jamii.
Buberwa alisema msaada huo ni sehemu ya jitihada za CRDB katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, hususani katika sekta ya elimu.
“Leo hii ni zamu ya Sekondari ya Kibweheri kupata meza 60 na viti 60. Kabla ya zoezi hili, Shule ya Sekondari Kwembe ilinufaika na msaada wa madawati 40,” alisema.
Aliongeza kuwa CRDB itaendelea kushirikiana na jamii katika maeneo mbalimbali, ikiwemo elimu, afya pamoja na kuwawezesha vijana na wanawake.
“Hatutaishia hapo. Tutaendelea kusaidia kwenye sekta za elimu, afya, vijana, wanawake na sekta nyingine,” alisema.
Buberwa alisema CRDB itaendelea kusikiliza mahitaji ya wateja na jamii na kushirikiana nao katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.














No comments:
Post a Comment