HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

September 21, 2026

CRDB YAUNGA MKONO BONGO BRAIN BATTLE

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam


BENKI ya CRDB kupitia CRDB Bank Foundation imeeleza kuwa ushiriki wake katika shindano la Bongo Brain Battle unalenga kuwajengea vijana uelewa mpana, hususan katika elimu ya fedha, ujasiriamali na masuala mbalimbali yanayohusu maisha na uchumi.

 

Akizungumza wakati wa msimu wa kwanza wa shindano hilo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Benki ya CRDB, Emmanuel Kiondo, alisema CRDB Bank Foundation imeamua kushiriki katika shindano hilo kutokana na umuhimu wake katika kuwapa vijana jukwaa la kujifunza na kuonyesha uwezo wao.



Alisema CRDB Bank Foundation ina dhamira ya kuwawezesha vijana na wanawake kupitia elimu ya fedha pamoja na ujasiriamali, hivyo Bongo Brain Battle ni moja ya majukwaa yanayoweza kusaidia kufikisha elimu hiyo kwa vijana.


“Tunafurahi kushiriki katika msimu huu wa kwanza na tunaamini huu ni mwanzo. Tutaendelea kushirikiana na Bongo Brain Battle kuhakikisha shindano hili linakuwa moja ya mashindano makubwa nchini, ili kuwapa vijana jukwaa la kujifunza na kuonyesha uwezo wao katika masuala mbalimbali,” alisema Kiondo.


Kiondo alisema kupitia CRDB Bank Foundation, benki hiyo pia imekuwa ikishirikiana na vyuo mbalimbali nchini katika kuwawezesha vijana wenye mawazo ya kibunifu na biashara.



Alitolea mfano ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambapo mwaka huu CRDB ilishiriki katika Imbeju Startup Challenge iliyolenga kuibua vijana wenye mawazo ya biashara na kuwasaidia kuyageuza kuwa biashara zinazoweza kutekelezeka.


Alisema vijana 60 waliofanya vizuri katika hatua hiyo wameingia katika hatua ya kufanyiwa uchambuzi wa mawazo yao ya biashara, kabla ya kupatiwa elimu na baadaye mitaji kwa ajili ya kuanzisha au kukuza biashara zao.


 


Aidha, alisema CRDB Bank Foundation imekuwa ikishirikiana na Chuo Kikuu cha Muhimbili katika kuhamasisha wanafunzi wa masomo ya afya kuwa wabunifu na kuibua mawazo yanayoweza kusaidia kutatua changamoto katika sekta ya afya.


“Tumekuwa tukishirikiana na kuwawezesha vijana wenye mawazo ya ubunifu ili kuyafanya kuwa biashara halisi zitakazoweza kuajiri wenzao na wakati huo huo kutoa mchango katika uchumi wa Tanzania,” alisema.


Kiondo alisema ushiriki wa CRDB katika Bongo Brain Battle ni sehemu ya mwendelezo wa juhudi za benki hiyo katika kuwawezesha vijana, huku shindano hilo likiwakutanisha washiriki kutoka katika makundi mbalimbali ya umri, ingawa vijana ndio wengi.



Kwa upande wake, Mratibu wa Challenge ya Vijana ya Bongo Brain Battle, Dk. Jimmy Minja, alisema shindano hilo linalenga kuwajengea vijana uelewa mpana kuhusu masuala mbalimbali ya dunia.


Alisema miongoni mwa maeneo yanayolengwa ni elimu ya fedha, historia, sayansi na jiografia, hivyo kuwapa vijana nafasi ya kujifunza huku wakishindana na kuonyesha uwezo wao.

 


No comments:

Post a Comment

Pages