Na Editha William, Bukoba, Kagera
Mganga Mkuu wa Manispaa, Peter Mkenda, amewataka wananchi kuzingatia tahadhari za kiafya na kutoa taarifa mapema wanapobaini dalili zinazoweza kuashiria ugonjwa wa Ebola, ili kuwezesha uchunguzi na hatua za kudhibiti maambukizi kuchukuliwa kwa wakati.
Akizungumza ofisini kwake, Mkenda amesema wananchi wanapaswa kuwa makini na dalili za ugonjwa huo, zikiwemo homa kali, uchovu wa mwili, maumivu ya misuli, maumivu ya kichwa, kutapika na kuharisha.
Amesema kuchelewa kutoa taarifa kwa mamlaka za afya kuhusu dalili zinazotia shaka kunaweza kuchelewesha uchunguzi na juhudi za kudhibiti uwezekano wa kuenea kwa maambukizi.
Aidha, amewataka wananchi kuepuka kugusa mizoga ya wanyama pamoja na damu na majimaji ya mwili wa mtu anayeshukiwa kuwa na Ebola. Ameeleza kuwa mtu mwenye dalili zinazotia shaka anapaswa kupata tathmini ya kitaalamu kupitia wahudumu wa afya.
Katika hatua nyingine, Mkenda amesisitiza umuhimu wa kuzingatia usafi wa mikono kwa kutumia maji tiririka na sabuni, pamoja na kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya.
Amesema kudhibiti magonjwa ya mlipuko kunahitaji ushirikiano wa wananchi, viongozi na wataalamu wa afya, huku akiwataka wananchi kuchukua tahadhari na kutoa taarifa mapema kwa mamlaka husika wanapobaini dalili zinazoweza kuashiria ugonjwa huo.





No comments:
Post a Comment