Na Editha William, Bukoba, Kagera
WAKAZI na wageni wanaoingia katika Manispaa ya Bukoba wametakiwa kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa usafi wa mazingira, hususan kwa kusafisha mitaro ili kurahisisha upitishaji wa maji ya mvua na kuzuia mafuriko.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Idara ya Taka Ngumu, Gesi, Usafi na Mazingira katika Manispaa ya Bukoba, Joseph Tambuko, aliyesema kuwa usafi wa mazingira ni jukumu la kila mtu na unapaswa kuzingatiwa katika maeneo ya makazi, biashara na maeneo ya umma.
Tambuko amesema hali ya usafi katika manispaa hiyo kwa sasa ni nzuri, hivyo ni muhimu kwa wananchi kuendelea kushirikiana na mamlaka husika ili kudumisha mafanikio hayo, hasa katika kipindi hiki cha mvua.
Amesisitiza kuwa kusafisha mitaro kabla na wakati wa mvua ni hatua muhimu katika kuhakikisha maji yanapita kwa urahisi na kupunguza uwezekano wa kutuama katika maeneo ya makazi na shughuli za kiuchumi.
Aidha, amewataka wananchi kutoridhika na hali nzuri ya usafi iliyopo, bali waendelee kuzingatia utupaji sahihi wa taka, kutunza mitaro na kuhakikisha mazingira yanayozunguka makazi yao yanakuwa safi wakati wote.
Kwa upande mwingine, Tambuko amewataka wageni wanaoingia katika manispaa hiyo kuzingatia taratibu za usafi na kushirikiana na wakazi katika kutunza mazingira, akieleza kuwa jukumu la kuuweka mji safi halibagui mtu kwa kuzingatia anapotoka.
Ameongeza kuwa kuendeleza siku za usafi na kuzingatia utaratibu wa ukusanyaji taka ni miongoni mwa hatua muhimu za kuhakikisha Manispaa ya Bukoba inaendelea kuwa safi na kupunguza hatari za kiafya zinazoweza kusababishwa na uchafuzi wa mazingira.





No comments:
Post a Comment