HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 04, 2013

MAKOCHA RIADHA WAASWA KUJITOLEA ZAIDI

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Riadhaa Tanzania (RT), Tullo Chambo akimkabidhi cheti mmoja wa washiriki wa kozi ya ukocha ngazi ya kwanza, Mary Christopher, kozi hiyo imeandaliwa na Chama cha riadha Mkoa wa Dar es Salaam (DAAA), kwa ushirikiano na shirikisho hilo, iliyomalizika jijini Dar es Salaam. (Picha na Habari Mseto Blog)
Washiriki wa kozi ya ukocha wa riadha ngazi ya kwanza wakiwa katika picha ya pamoja na wakufunzi wao baada ya kukabidhiwa vyeti vyao na mgeni rasmi, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Tullo Chambo (wa tano kutoka kushoto mstari wa nyuma), aliyemwakilisha Rais wa Shirikisho hilo, Anthony Mtaka. 

Na Elizabeth John

MAKOCHA wa riadha waliohitimu Kozi ya Ukocha Ngazi ya Kwanza  (Level One Coaches Course), jijini Dar es Salaam, wametakiwa kwenda kufanyia kazi kivitendo mafunzo waliyopata huku wakitanguliza kujitolea zaidi badala ya fedha.

Wito huo, ulitolewa lei wakati wa kufunga kozi hiyo kwenye Shule ya Msingi Kibasila jijini Dar es Salaam na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Riadha Tanzania (RT), Tullo Chambo, aliyemwakilisha Rais wa Shirikisho hilo, Anthony Mtaka.

Chambo, aliwataka walimu hao kuhakikisha uelewa na utaalamu waliyoupata, unakuza mchezo huo na hasa shuleni ambako ndiko vipaji viliko ili riadha iweze kupiga hatua zaidi ya sasa.

“Kama mnavyojua hakuna mchezo wowote ambao hauanzii chini na kama tunahitaji kuwapata wanariadha bora, tunatakiwa kuanzia chini viliko vipaji, hasa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari,” alisema Chambo huku akiwataka kuendelea kujitolea zaidi, badala ya kutanguliza fedha zaidi katika kutoa ujuzi wao, jambo ambalo limekuwa likiwafanya baadhi ya wadau kuwakimbia na kuwachukua watu wasio na ujuzi katika matukio mbalimbali ya riadha ili kuepuka gharama.

Akijibu ombi la wakufunzi hao kutumika katika mashindano mbalimbali yakiwamo ya Taifa, Chambo alisema, RT inawaenzi wataalamu wake na itaendelea kuwatumia katika matukio mbalimbali ingawaje si wote kwa pamoja.

Kwa upande wa mkufunzi, Samwel Tupa, ambaye anatambulika na Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF), alisema mbali ya mafunzo ya nadharia na vitendo ambayo walimu hao walifundishwa juu ya mchezo wa riadha, pia wamejifunza falsafa ya michezo.

"Tumewafunza kuwajenga nguvu wanariadha, makuzi na mabadiliko sambamba na utaratibu wa mazoezi," alisema Tupa na kuwataka kwenda kuyafanyia kazi yale yote waliyofundishwa ili kuendeleza mchezo huo hapa nchini, badala ya kwenda kujikweza kwa kupata vyeti hivyo, kitendo alichofananisha sawa na kuweka chemli chini ya uvungu chumbani.

Kozi hiyo ilishirikisha waalimu 23 wa shule za Msingi na Sekondari kutoka mikoa mitatu, Dar es Salaam, Lindi na Shinyanga, ambako mbali na Tupa, wakufunzi wengine walikuwa ni Kapteni mstaafu, Lucas Nkungu na Idd Mhunzi kutoka Chama cha Riadha Mkoa wa Dar es Salaam (DAAA).

Katika hatua nyingine, Rais wa RT, Anthony Mtaka, ameondoka nchini usiku wa kuamkia leo kwenda Moscow nchini Russia, kyshiriki mkutano mkuu wa IAAF, ambao utafanyika sambamba na mashindano ya dunia, ambako Tanzania inawakilishwa wanariadha wawili, Msenduki Mohamed na Faustine Mussa. 

No comments:

Post a Comment

Pages