Mkuu wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za
Kulevya, Godfrey
Nzowa akionesha Cocaine zilizokuwa
zimefichwa katika mkanda wa suruali aliyokuwa amevaa raia wa Colombia, Andres
Filipe Ballesteros Uribe (28), mara baada ya kukamatwa kwenye Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. (Picha na Francis
Dande)
Hati ya kusafiria ya mtuhumiwa huyo yenye namba AP816263 iliyotolewa Julai 3,2014
nchini Columbia.
Suruali ya mtuhumiwa huyo ikiwa imezungushiwa Cocaine.
Baadhi ya dawa alizokuwa amemeza mtuhumiwa huyo.
DAR ES SALAAM, Tanzania
KIKOSI cha Kuzuia na Kupambana
na Dawa za Kulevya nchini kinamshikilia Andres Filipe Ballesteros Uribe (28)
raia wa Colombia kwa tuhuma za kuingiza dawa hizo nchini kinyume cha sheria.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo, Mkuu wa Kikosi hicho, Kamanda Godfrey Nzowa
alisema mtuhumiwa huyo aliingia nchini saa nane usiku kwa ndege ya shirika la
Ethiopian akitokea Adisi Ababa.
Alisema mtuhumiwa huyo
alikutwa na Cocaine iliyofungwa kwenye pakiti sita tofauti na kuiweka sehemu za
siri, kiunoni kama mkanda na nyingine tumboni.
Kamanda Nzowa alisema
mtuhumiwa huyo mwenye pasi ya kusafiria namba AP816263 iliyotolewa Julai 3,2014
nchini Columbia, alitoka Columbia kupitia Adis Ababa kuja Tanzania huku
akibainisha kwamba hiyo ni njia mpya ya usafirishaji wa dawa hizo haramu.
“Hawa jamaa wanajaribu kubuni
mbinu mpya kama huyu kijana alikuwa amefunga unga wa cocaine kama zilivyokuwa
zikifungwa pipi na akazimeza… mpaka sasa ameshatoa pipi 13 kwa njia ya haja
kubwa na anaendelea kutoa.
“…Sio rahisi kujua idadi ya
mzigo aliokuwa nao mpaka atakapomaliza kuzitoa zote za tumboni ndiyo tunaweza
kusema uzito wa dawa hizo na thamani yake,” alisema kamanda Nzowa.
Alisisitiza kwamba taarifa
sasa wanazopeana kwenye mtandao wao unawezesha kukamatwa kwa watuhumiwa huku
akibainisha kuwa lengo ni kudhibiti usafirishaji kwa njia yoyote.
Kamanda Nzowa alisema
mafanikio yanaonekana kwa vile kuanzia Juni 24 mwaka huu hadi Agosti 10 hakuna
mtu aliyekamatwa akiingiza huku akibainisha kwamba umadhubuti wa mtandao wao
umefanikisha hilo.
“Asiyeamini kwamba
tumefanikiwa atujaribu aone… naamini tunakokwenda dawa za kulevya hasa cocaine
na heroine zitakuwa hazipiti wala kuingia Tanzania,” alisema na kuongeza kwamba
wanadhibiti pia ulimaji wa bangi.
Kwa mujibu wa kamanda huyo lengo
la mtandao wao ni kudhibiti sio kukamata wala kuteketeza.
No comments:
Post a Comment