HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 25, 2015

Simba, Yanga zaibomoa Mbeya City

Nyota wa Mbeya City, Peter Mwalyanzi, akisaini mkataba kujiunga na klabu ya Simba kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, mbele ya Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Collin Frish, jijini Dar es Salaam. (Na Mpiga Picha Wetu)

XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

JAHAZI la timu ya Mbeya City linazidi kutobolewa baada ya klabu kongwe za soka hapa nchini, Simba na Yanga kunyakua wachezaji nyota wa timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2015/16.

Simba na Yanga hivi sasa zimekuwa zikipigana vikumbo kuwania saini za nyota waliong’ara Mbeya City, ambako siku moja tu baada ya mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga kumnasa Deus Kaseke na kuwapiku Simba waliokuwa nao wakimnyatia, Wana Msimbazi hao nao jana wamejibu mapigo kwa kumnyakua kiungo Peter Mwalyanzi.


Habari za kuaminika kutoka ndani ya uongozi wa Simba, zilisema kuwa, klabu hiyo kwa sasa haihitaji kufanya usajili usiokuwa na manufaa kama msimu uliopita, hivyo wamemnasa Mwalyanzi kutokana na kiwango alichokionyesha.

Mtoa habari huyo, alisema nyota huyo tayari amesaini kuichezea Simba kwa mwaka mmoja na tayari atatambulishwa rasmi katika sherehe za Simba Day zinazofanyika Agosti kila mwaka kabla ya Ligi Kuu kuanza.

Alisema nyota huyo alimwaga wino jana mbele ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hanspope pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Collins Frish.

“Simba kwa sasa tunafanya usajili wa nguvu, hatutaki kurudia makosa kama tuliyoyafanya msimu uliomalizika, kwani tulitaka kumsajili na Deus Kaseke, kwa bahati mbaya Yanga wamemnasa tayari,” alisema.

Wakati Simba wao wakijipanga ikiwamo kuwaongezea mkataba wa miaka mitatu mitatu wachezaji wao Hassan Isihaka na Said Ndemla, wenzao Yanga hadi sasa wamewanyakua nyota wawili, Haruna Chanongo aliyekuwa akicheza kwa mkopo Stand United na Kaseke.


Hata hivyo, wakongwe hao bado wanawania pia saini za nyota wawili tena wa Mbeya City, Hassan Mwasapili na John Kabanda. 
CHANZO GAZETI LA TANZANIA DAIMA.

No comments:

Post a Comment

Pages