Nyota wa Mbeya City, Peter Mwalyanzi, akisaini mkataba
kujiunga na klabu ya Simba kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara,
mbele ya Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Collin Frish, jijini Dar es Salaam. (Na Mpiga Picha Wetu)
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
JAHAZI la timu ya Mbeya City
linazidi kutobolewa baada ya klabu kongwe za soka hapa nchini, Simba na Yanga
kunyakua wachezaji nyota wa timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu
Tanzania Bara 2015/16.
Simba na Yanga hivi sasa
zimekuwa zikipigana vikumbo kuwania saini za nyota waliong’ara Mbeya City, ambako
siku moja tu baada ya mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga kumnasa Deus Kaseke
na kuwapiku Simba waliokuwa nao wakimnyatia, Wana Msimbazi hao nao jana
wamejibu mapigo kwa kumnyakua kiungo Peter Mwalyanzi.
Habari za kuaminika kutoka
ndani ya uongozi wa Simba, zilisema kuwa, klabu
hiyo kwa sasa haihitaji kufanya usajili usiokuwa na manufaa kama msimu uliopita,
hivyo wamemnasa Mwalyanzi kutokana na kiwango alichokionyesha.
Mtoa habari huyo, alisema
nyota huyo tayari amesaini kuichezea Simba kwa mwaka mmoja na tayari
atatambulishwa rasmi katika sherehe za Simba Day zinazofanyika Agosti kila
mwaka kabla ya Ligi Kuu kuanza.
Alisema nyota huyo alimwaga
wino jana mbele ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hanspope pamoja na
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Collins Frish.
“Simba kwa sasa tunafanya
usajili wa nguvu, hatutaki kurudia makosa kama tuliyoyafanya msimu
uliomalizika, kwani tulitaka kumsajili na Deus Kaseke, kwa bahati mbaya Yanga
wamemnasa tayari,” alisema.
Wakati Simba wao wakijipanga
ikiwamo kuwaongezea mkataba wa miaka mitatu mitatu wachezaji wao Hassan Isihaka
na Said Ndemla, wenzao Yanga hadi sasa wamewanyakua nyota wawili, Haruna
Chanongo aliyekuwa akicheza kwa mkopo Stand United na Kaseke.
Hata hivyo, wakongwe hao bado
wanawania pia saini za nyota wawili tena wa Mbeya City, Hassan Mwasapili na
John Kabanda.
CHANZO GAZETI LA TANZANIA DAIMA.
No comments:
Post a Comment