HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 31, 2017

TATIZO LA MAJI NCHINI KUWA HISTORIA-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya ilitengewa sh. bilioni 2.72 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji.

Amesema mkakati huo unatekelezwa kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo, wananchi katika maeneo yote nchini watapata huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana (Jumapili, Julai 30, 2017) alipozungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa Halmashauri za Rungwe na Busokelo katika mikutano ya hadhara aliyoifanya Kandete na Tandale katika wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya.

Alisema mkoa wa Mbeya umetengewa sh. bilioni 10.383  kwa ajili ya utekelezaji miradi mbalimbali ya maji, ambapo kati yake sh. bilioni 2.72 zinatarajiwa kutumika katika utekelezaji wa miradi ya maji kwenye wilaya ya Rungwe.

Waziri Mkuu alitaja mradi mwingine unaotekelezwa wilayani Rungwe ni pamoja na mradi wa maji wa Masoko wenye thamani ya sh. bilioni 5.3, utakaohudumia jumla ya vijiji 15. “Mradi huu ni miongoni mwa miradi inayojengwa chini ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa fedha za ndani.” 

Alisema mradi huo utakapokamilika utawanufaisha wananchi wapatao 19,624 katika vijiji vya Bulongwe, Ngaseke, Igembe, Ntandabala, Lupando, Bujesi, Lufumbi, Nsyasa, Ikama, Itagata, Busisya, Mbaka, Isabula, Lwifa na Nsanga. 

Pia Waziri Mkuu alisema wananchi lazima wazingatie sheria ya Mazingira inayozuia kufanya shughuli za kibinadamu pamoja na kujenga kwenye maeneo yote ya vyanzo vya maji ndani ya mita 60 ili kuliepusha Taifa kugeuka jangwa.

Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu aliwaagiza watendaji kuwachukua hatua watu wote watakaokutwa wakiendesha shughuli mbalimbali kama za kilimo, ujenzi wa makazi na uchungaji wa mifugo ndani ya vyanzo vya maji kwa kuwa zinasababisha ukame.

“Hatuwezi kuruhusu Taifa likaangamia kwa ajili ya watu wachache wanaoharibu mazingira kwa kuendesha shughuli za kibinadamu ndani ya vyanzo vya maji. Ni marufuku kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka katika vyanzo vya maji, atakayekutwa atachukuliwa hatua za kisheria.”

Awali Mbunge wa Jimbo la Busokelo Mheshimiwa Fredy Mwakibete na mbunge wa Rungwe Mheshimiwa Saul Amon walimueleza Waziri Mkuu kwamba upatikanaji wa huduma ya maji na salama ni miongoni mwa changamoto zinazoyakabili majimbo yao.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, JULAI 31, 2017

No comments:

Post a Comment

Pages