HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 15, 2018

Serikali Yapunguza Udumavu, Vifo vya Watoto Chini ya Miaka Mitano kwa Asilimia 50

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akizungumza wakati alipomwakilisha Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango katika uzinduzi wa machapisho ya uchambuzi wa bajeti katika sekta ya jamii iliyofanyika leo jijini Dodoma.
 
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Serikali imeweza kufanya tahtmini na kubaini kuwa jitihada zilizofanyika zimeweza kupunguza udumavu na vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kwa asilimia 50.

Takwimu hizo zimetolewa leo jijini Dodoma na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alipokuwa akimuwakilisha Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango katika uzinduzi wa machapisho ya uchambuzi wa bajeti katika sekta ya jamii.

Waziri Ummy amesema kuwa katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na upungufu wa viwango vya matatizo ya lishe kwa baadhi ya viashiria ambapo moja ya viashiria vya kupungua kwa matatizo ya lishe ni kushuka kwa tatizo la udumavu, uzito pungufu pamoja na ukondefu wa mwili miongoni mwa watoto.

“Kama tunavyofahamu udumavu huathiri ukuaji wa mtoto kimwili na kiakili na kupunguza uwezo wa kufanya vizuri shuleni pamoja na kupunguza ufanisi wake katika maisha ya utu uzima, hivyo kutokana na juhudi za Serikali na wadau mbalimbali tumeweza kupunguza udumavu kwa kiwango cha asilimia 50 ambapo kwa sasa kuna wastani wa watoto watatu wenye udumavu kati ya watoto 10 walio chini ya umri wa miaka mitano,” alisema Waziri Ummy.

Waziri Ummy ameongeza  kuwa ingawa bado kuna changamoto kubwa miongoni mwa kundi la watoto kwa sababu ya idadi yao kuwa kubwa, kushuka kwa kiwango cha udumavu ni jambo la kujivunia kwani  hali hiyo inaonesha kuwa jitihada za kupambana na tatizo hilo zimezaa matunda.

Akizungumzia kuhusu machapisho hayo, Waziri Ummy amefafanua kuwa  Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na UNICEF walifanya uchambuzi wa bajeti katika sekta mtambuka ya jamii hususan katika Elimu, Afya, Virusi vya Ukimwi, Maji na Usafi wa mazingira na lishe kwa lengo la kuboresha upangaji na utekelezaji wa masuala ya Mama na Mtoto katika mipango na Bajeti.

Akimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa za Michezo, Susan Mlawa amesema kuwa machapisho hayo yanatoa Muhtasari wa Bajeti katika sekta mtambuka ya maendeleo ya jamii kwa kipindi cha kati ya mwaka wa fedha 2013/2014 na 2017/2018.

“Machapisho hayo yameelezea kuhusu kubaini kiasi cha fedha zilizotengwa na kutolewa katika bajeti kwa maeneo muhimu ya sekta ya jamii ambayo ni Elimu, Afya, Virusi vya Ukimwi na Ukimwi, Lishe, Maji na Usafi wa mazingira, kutoa Muhtasari wa Bajeti, kuishauri Serikali katika Sera, Mipango na bajeti yenye kuzingatia kuwapatia watoto makuzi bora na ulinzi kwa Mama na watoto katika jamii pamoja na kutoa elimu kwa wadau mbalimbali,” alisema Susan.

Akiwawakilisha wadau wengine, Mwakilishi kutoka shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto (UNICEF), Maniza Zaman amesema kuwa shirika hilo limekuwa likifuatilia kwa karibu matumizi ya fedha za Umma zinazoelekezwa kwa watoto.

Zaman amefafanua kuwa katika kutekeleza na kuzingatia dira ya Serikali 2025 inayolenga ukuaji wa viwanda na kufikia uchumi wa kati, kumekuwa na hitaji la kuboresha huduma za afya, elimu pamoja na kuondoa changamoto zinazowakabili watoto na vijana nchini ili waweze kuimarisha afya zao pamoja na kuchangia katika maendeleo ya taifa hivyo mapendekezo yaliyotolewa katika machapisho hayo yanalenga kutekeleza lengo hilo.

Machapisho hayo yameandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikisha Wizara za Kisekta; Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Tume ya UKIMWI Tanzania (TACAIDS) na Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC).

No comments:

Post a Comment

Pages