Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Ummy Mwalimu akizungumza wakati alipomwakilisha Waziri wa Fedha na Mipango,
Dkt. Philip Mpango katika uzinduzi wa machapisho ya uchambuzi wa bajeti katika
sekta ya jamii iliyofanyika leo jijini Dodoma.
Na
Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Serikali
imeweza kufanya tahtmini na kubaini kuwa jitihada zilizofanyika zimeweza
kupunguza udumavu na vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kwa
asilimia 50.
Takwimu hizo zimetolewa leo jijini Dodoma na
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
alipokuwa akimuwakilisha Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango katika
uzinduzi wa machapisho ya uchambuzi wa bajeti katika sekta ya jamii.
Waziri Ummy amesema kuwa katika miaka ya hivi
karibuni, kumekuwa na upungufu wa viwango vya matatizo ya lishe kwa baadhi ya
viashiria ambapo moja ya viashiria vya kupungua kwa matatizo ya lishe ni
kushuka kwa tatizo la udumavu, uzito pungufu pamoja na ukondefu wa mwili
miongoni mwa watoto.
“Kama
tunavyofahamu udumavu huathiri ukuaji wa mtoto kimwili na kiakili na kupunguza
uwezo wa kufanya vizuri shuleni pamoja na kupunguza ufanisi wake katika maisha
ya utu uzima, hivyo kutokana na juhudi za Serikali na wadau mbalimbali tumeweza
kupunguza udumavu kwa kiwango cha asilimia 50 ambapo kwa sasa kuna wastani wa
watoto watatu wenye udumavu kati ya watoto 10 walio chini ya umri wa miaka mitano,”
alisema Waziri Ummy.
Waziri Ummy ameongeza kuwa ingawa bado kuna changamoto kubwa
miongoni mwa kundi la watoto kwa sababu ya idadi yao kuwa kubwa, kushuka kwa
kiwango cha udumavu ni jambo la kujivunia kwani hali hiyo inaonesha kuwa jitihada za kupambana
na tatizo hilo zimezaa matunda.
Akizungumzia kuhusu machapisho hayo, Waziri Ummy
amefafanua kuwa Wizara ya Fedha na
Mipango kwa kushirikiana na UNICEF walifanya uchambuzi wa bajeti katika sekta
mtambuka ya jamii hususan katika Elimu, Afya, Virusi vya Ukimwi, Maji na Usafi wa mazingira na lishe kwa lengo la kuboresha upangaji na
utekelezaji wa masuala ya Mama na Mtoto katika mipango na Bajeti.
Akimuwakilisha
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James, Katibu Mkuu wa Wizara
ya Habari, Utamaduni, Sanaa za Michezo, Susan Mlawa amesema kuwa machapisho
hayo yanatoa Muhtasari wa
Bajeti katika sekta mtambuka ya maendeleo ya jamii kwa kipindi cha kati ya mwaka wa fedha 2013/2014 na 2017/2018.
“Machapisho hayo yameelezea kuhusu kubaini kiasi cha fedha zilizotengwa
na kutolewa katika bajeti kwa maeneo muhimu
ya sekta ya jamii ambayo ni
Elimu, Afya, Virusi vya Ukimwi na Ukimwi, Lishe, Maji
na Usafi wa mazingira, kutoa Muhtasari
wa Bajeti, kuishauri Serikali katika Sera, Mipango na bajeti yenye kuzingatia kuwapatia
watoto makuzi bora na ulinzi kwa Mama na watoto katika jamii pamoja na kutoa elimu kwa wadau mbalimbali,” alisema Susan.
Akiwawakilisha wadau wengine, Mwakilishi kutoka
shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto (UNICEF), Maniza Zaman amesema
kuwa shirika hilo limekuwa likifuatilia kwa karibu matumizi ya fedha za Umma
zinazoelekezwa kwa watoto.
Zaman amefafanua kuwa katika
kutekeleza na kuzingatia dira ya Serikali 2025 inayolenga ukuaji wa viwanda na
kufikia uchumi wa kati, kumekuwa na hitaji la kuboresha huduma za afya, elimu
pamoja na kuondoa changamoto zinazowakabili watoto na vijana nchini ili waweze
kuimarisha afya zao pamoja na kuchangia katika maendeleo ya taifa hivyo
mapendekezo yaliyotolewa katika machapisho hayo yanalenga kutekeleza lengo
hilo.
Machapisho hayo yameandaliwa na Wizara ya Fedha na
Mipango kwa kushirikisha Wizara za Kisekta; Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI), Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Tume ya UKIMWI Tanzania (TACAIDS) na Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC).
No comments:
Post a Comment