Waziri wa Madini Angellah Kairuki (kulia) akizungumza wakati
makabidhiano ya mashine ya kusaidia kupumua kwa Watoto njiti
ilivyotolewa na taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation kwa hospitali ya
rufaa ya mkoa wa Dodoma ili kusaidia kupunguza vifo vya Watoto Njiti.
Wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation Rosalynn Mworia,
Mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Mollel, Doris Mollel (katikati).
Afisa Muuguzi Msaidizi kutoka Kitengo cha kuhudumia Watoto Njiti
Constancia Mankupe akielezea kwa vitendo namna mashine ya kusaidia
kupumua kwa Watoto njiti inavyofanya kazi, mashine hii ni mojawapo kati
ya vifaa tiba vyenye thamani Sh 25 m vilivyotolewa na taasisi ya Vodacom
Tanzania Foundation vilivyokabidhiwa kwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa
Dodoma ili kusaidia kupunguza vifo vya Watoto Njiti. Kulia kwake ni
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayesimamia Sera, Bunge, Kazi,
Ajira, Vijana na walemavu Anthony Mavunde na Mkurugenzi wa Taasisi ya
Doris Mollel, Doris Mollel. Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation Rosalynn Mworia, akikabidhi mashine ya kusaidia kupumua kwa Watoto njiti kwa Waziri wa Madini Angellah Kairuki (wa pili kulia) na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayesimamia Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na walemavu Anthony Mavunde (kulia) katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma ili kusaidia kupunguza vifo vya Watoto Njiti. Wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Mollel, Bi Doris Mollel.
NA MWANDISHI WETU
KATIKA
kuunga mkono lengo la Serikali la kupunguza vifo vya uzazi na watoto njiti,
Taasisi za Vodacom Tanzania Foundation kwa kushirikiana na Doris Mollel
Foundation, imetoa mchango wenye thamani ya Sh. Milioni 25 kwa Hospitali ya
Rufaa ya Dodoma, ili kulinda maisha ya watoto njiti.
Lengo
la mchango huo ni kupunguza uwiano wa vifo vya uzazi hadi kufikia watoto
292 kati ya watoto 100,000 kwa vizazi hai, kutoka watoto 556 kati ya 100,000.
Hafla
ya kukabidhi kiasi hicho ilishuhudiwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Waziri wa Madini, Angellah Kairuki na Antony
Mavunde, ambaye ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira,
Vijana na Walemavu.
Msaada
huo, unajumuisha vifaa mbalimbali muhimu vya kuhudumia wazazi, pamoja na kuokoa
maisha kama vile vifaa vya oksijeni (Oxygen concentrator) ambavyo vitasaidia
watoto njiti kupumua na vitanda vitatu vya watoto, ambao pia utawasilishwa
katika Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu, Kigoma.
Akizungumza
wakati wa zoezi hilo, Mkurugenzi wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano
wa Vodacom, Rosalynn Mworia, alisema Vodacom imeazimia kupunguza idadi ya
vifo vinavyotokea wakati wa kujifungua pamoja na vifo vya watoto wachanga.
“Vodacom
Foundation inaunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha utoaji wa huduma za
afya. Tunatarajia kwamba mchango wetu utaenda mbali katika safari nzima ya
kuokoa maisha mengi zaidi ya wanawake na watoto,” alisema Mworia.
Kwa
upande wake, Waziri Ummy alisema kuwa, msaada huo umekuja wakati muafaka ambapo
Serikali imeanza kampeni ya kupunguza idadi ya vifo vya akina mama, wakati wa
kujifungua na watoto wachanga hapa nchini.
“Tunapenda
kuwashukuru Vodacom Foundation na Doris Mollel Foundation katika kusaidia nchi
kukabiliana na changamoto hizi. Vifaa hivi ni nafasi muhimu katika kukabiliana
na matatizo ambayo watoto njiti hukutana nayo hasa katika wiki nne za kwanza za
maisha yao,” alisema.
"Ninawasihi
wafanyakazi wa afya katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kutumia kwa usahihi
vifaa hivi. Msiruhusu mashine zikusanye vumbi, mashine hizi ziko hapa kwa ajili
ya kuokoa maisha ya watoto wetu," alisisitiza.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, alisema kupambana na vifo vya
watoto wachanga nchini Tanzania ni suala mtambuka, maana ni wajibu wa kila
mmoja kwa nafasi yake na kwa pamoja.
"Mchango
huu ni ishara kubwa ya ushirikiano kwa kampeni inayoendelea, Jiongeze -
Tuwavushe Salama na inalingana na kiapo nilichochukua, pamoja na wakuu wengine
wa mikoa, ambapo tuliahidi kufanya kazi ya kupunguza vifo vya uzazi na watoto
wachanga nchini Tanzania," alisema.
No comments:
Post a Comment