HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 15, 2018

Vodacom Foundation yapiga tafu Hospitali ya Rufaa Dodoma

Waziri wa Madini Angellah Kairuki (kulia) akizungumza wakati makabidhiano ya mashine ya kusaidia kupumua kwa Watoto njiti ilivyotolewa na taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation kwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma ili kusaidia kupunguza vifo vya Watoto Njiti. Wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation Rosalynn Mworia, Mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Mollel, Doris Mollel (katikati). 
Afisa Muuguzi Msaidizi kutoka Kitengo cha kuhudumia Watoto Njiti Constancia Mankupe akielezea kwa vitendo namna mashine ya kusaidia kupumua kwa Watoto njiti inavyofanya kazi, mashine hii ni mojawapo kati ya vifaa tiba vyenye thamani Sh 25 m vilivyotolewa na taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation vilivyokabidhiwa kwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma ili kusaidia kupunguza vifo vya Watoto Njiti. Kulia kwake ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayesimamia Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na walemavu Anthony Mavunde na Mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Mollel, Doris Mollel. 
Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation Rosalynn Mworia, akikabidhi mashine ya kusaidia kupumua kwa Watoto njiti kwa Waziri wa Madini Angellah Kairuki (wa pili kulia) na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayesimamia Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na walemavu Anthony Mavunde (kulia) katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma ili kusaidia kupunguza vifo vya Watoto Njiti. Wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Mollel, Bi Doris Mollel.  

 NA MWANDISHI WETU


KATIKA kuunga mkono lengo la Serikali la kupunguza vifo vya uzazi na watoto njiti, Taasisi za Vodacom Tanzania Foundation kwa kushirikiana na Doris Mollel Foundation, imetoa mchango wenye thamani ya Sh. Milioni 25 kwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, ili kulinda maisha ya watoto njiti.

Lengo la mchango huo ni  kupunguza uwiano wa vifo vya uzazi hadi kufikia watoto 292 kati ya watoto 100,000 kwa vizazi hai, kutoka watoto 556 kati ya 100,000.

Hafla ya kukabidhi kiasi hicho ilishuhudiwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Waziri wa Madini, Angellah Kairuki na Antony Mavunde, ambaye ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu.

Msaada huo, unajumuisha vifaa mbalimbali muhimu vya kuhudumia wazazi, pamoja na kuokoa maisha kama vile vifaa vya oksijeni (Oxygen concentrator) ambavyo vitasaidia watoto njiti kupumua na vitanda vitatu vya watoto, ambao pia utawasilishwa katika Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu, Kigoma.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkurugenzi wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom, Rosalynn Mworia, alisema Vodacom imeazimia kupunguza idadi ya vifo vinavyotokea wakati wa kujifungua pamoja na vifo vya watoto wachanga.

“Vodacom Foundation inaunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha utoaji wa huduma za afya. Tunatarajia kwamba mchango wetu utaenda mbali katika safari nzima ya kuokoa maisha mengi zaidi ya wanawake na watoto,” alisema Mworia.

Kwa upande wake, Waziri Ummy alisema kuwa, msaada huo umekuja wakati muafaka ambapo Serikali imeanza kampeni ya kupunguza idadi ya vifo vya akina mama, wakati wa kujifungua na watoto wachanga hapa nchini. 

“Tunapenda kuwashukuru Vodacom Foundation na Doris Mollel Foundation katika kusaidia nchi kukabiliana na changamoto hizi. Vifaa hivi ni nafasi muhimu katika kukabiliana na matatizo ambayo watoto njiti hukutana nayo hasa katika wiki nne za kwanza za maisha yao,” alisema.

"Ninawasihi wafanyakazi wa afya katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kutumia kwa usahihi vifaa hivi. Msiruhusu mashine zikusanye vumbi, mashine hizi ziko hapa kwa ajili ya kuokoa maisha ya watoto wetu," alisisitiza.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, alisema kupambana na vifo vya watoto wachanga nchini Tanzania ni suala mtambuka, maana ni wajibu wa kila mmoja kwa nafasi yake na kwa pamoja.

"Mchango huu ni ishara kubwa ya ushirikiano kwa kampeni inayoendelea, Jiongeze - Tuwavushe Salama na inalingana na kiapo nilichochukua, pamoja na wakuu wengine wa mikoa, ambapo tuliahidi kufanya kazi ya kupunguza vifo vya uzazi na watoto wachanga nchini Tanzania," alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages