SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT), jana limemtambulisha Mkufunzi
wa kujitolea kutoka nchini Japan, Ayane Sato.
Mkufunzi huyo, amekuja nchini kupitia ushirikiano uliopo
baina ya Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo la Kimataifa (JICA),
na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Akizungumza na Waandishi wa habari Uwanja wa Taifa jijini Dar
es Salaam jana, Katibu Msaidizi wa RT, Ombeni Zavala, alisema Kocha huyo akiwa
hapa nchini atajikita zaidi katika mbio fupi, za kati, miruko na mitupo.
Zavala, alisema Sato akiwa hapa nchini atafundiosha klabu mbalimbali,
shule na kuwaongezea ujuzi wa makocha wa hapa nchini.
“Tunawashukuru sana wenzetu wa Japan, kwa kweli wameonyesha
nia ya kuhakikisha tunafanya vizuri na kupata ushiriki mkubwa na wa kimafanikio
katika mashindano mbalimbali ya kimataifa hususan Olimpiki ya Tokyo 2020,”
alisema Zavala.
Kwa upande wake, Ayane alisema amefurahi kukutana na
Watanzania ambao ni wakarimu na kwamba anaamini atafundisha vizuri.
Alisema yeye ni mtaalamu wa mbio fupi, za kati, miruko na
mitupo na kwamba atajitahidi kufanya vizuri kuelekea Olimpiki Tokyo 2020.
Alisema kwa kushirikiana na makocha waliopo, atahakikisha
hamwachi nyuma mwanariadha yeyote ambaye atakuwepo kwenye program yake.
Mkufunzi huyo ambaye alikuwa Mruka kwa Upondo ‘Pole Vault’,
atakuwepo nchini kwa miaka miwili na ataanza rasmi program zake Novemba 27
mwaka huu mara baada ya kumalizika kwa Mashindano ya Wanawake ‘Ladies First’
yatakayofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Novemba 24 na 25.
No comments:
Post a Comment