HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 19, 2012

MORRIS, CANNAVARO WAPELEKWA KAMATI YA NIDHAMU

DAR ES SALAAM, Tanzania

SHIRIKISHO la Sona Tanzania (TFF), limepokea barua ya chama cha mchezo huo cha Zanzibar (ZFA), ikieleza kuwafungia wachezaji kadhaa Wazanzibari wanaochezea klabu mbalimbali za Tanzania Bara na timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars'.

Kwa mujibu wa taarifa Ofisa Habari wa TFF, shirikisho limeamua kulipeleka suala hilo kwa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi kwa hatua zaidi, hivyo kwa sasa Shirikisho litasubiri uamuzi wa kamati hiyo. 

Baadhi ya wachezaji hao ni Aggrey Morris, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Nassoro Masoud Cholo, Mcha Khamis, Seif Abdallah na Selemani Kassim Selembe.

Wachezaji hao wamefungiwa na ZFA baada ya kugoma kurejesha pesa za mgao wa dola 10,000, ambazo Zanzibar Heroes ilitunukiwa baada ya kuibuka washindi wa tatu wa michuano ya Chaalenji nchini Uganda, ambapo nyota wote waligawana pesa hizo, kabla ya wengine kutii agizo la kuwataka warejeshe.

MTIBWA, AZAM ZATINGA NUSU FAINALI KOMBE LA UHAI

Mtibwa Sugar imekata tiketi ya kucheza nusu fainali ya michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha timu za vijana wenye umri chini ya miaka 20 za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom baada ya leo asubuhi kuizamisha African Lyon mabao 3-1.

Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, hadi mapumziko Mtibwa Sugar ilikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa dakika ya 22 na Hillary Kasela. Hassan Kabunda aliisawazishia African Lyon katika dakika ya 53.

Mabao mengine ya washindi yalifungwa na Godfrey Mohamed dakika ya 64 na Juma Lazio akapachika la mwisho dakika ya 87. Kwa ushindi huo, Mtibwa Sugar sasa itacheza mechi ya kwanza ya nusu fainali dhidi ya Azam ambayo nayo leo asubuhi iliilaza JKT Ruvu bao 1-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Chamazi. 

Bao la Azam lilifungwa dakika ya 46 na Mudathiri Yahya.

Mechi hiyo ya kwanza ya nusu fainali itachezwa Ijumaa Desemba 21 saa 8:00 mchana kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam. Nusu fainali ya pili nayo itachezwa kwenye uwanja huo huo kuanzia saa 10 kamili jioni.

Hadi tunakwenda mitamboni, robo fainali ya tatu kati ya Oljoro JKT na Simba, na robo fainali ya nne zinachezwa zilikuwa zikiendelea kupigwa kwenye viwanja vya Karume na Chamazi, Dar es Salaam.

Mechi ya fainali na ile ya kutafuta mshindi wa tatu zitachezwa Jumapili Desemba 23 kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Pages