HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 11, 2012

BENITEZ 'FULL MCHECHETO' KLABU BINGWA YA DUNIA


YOKOHAMA, Japan

"Ni michuano mikubwa yenye ushindani. Sina matatizo makubwa katika suala zima la shinikizo. Nina uzoefu wa kutosha, na ningependa kufurahia kila dakika ya uwapo wangu hapa – kwa kufanya kilicho bora na kujaribu kadri niwezavyo kushinda ubingwa wa michuano hii"

WAKATI mabingwa wa soka barani Ulaya Chelsea Alhamisi hii wakitarajia kujitupa ndani ya dimba la International jijini hapa kuumana na Monterrey katika nusu fainali ya Klabu Bingwa ya Dunia, kocha wa klabu hiyo ya jijini London,  Rafael Benitez amesisitiza kuwa michuano hiyo ni mtihani mzito kwa kikosi chake.

The Blues wako katika michuano hiyo kaka wawakilishi wa bara la Ulaya katika michuano hiyo ya timu saba, zikiwamo sita mabingwa wa mabara tofauti, ambapo Alhamis watashuka dimbani katika nusu fainali ya michuano hiyo dhidi ya klabu hiyo kutoka nchini Mexico.

"Ni michuano mikubwa yenye ushindani," alisema Benitez, ambaye alitwaa ubingwa wa michuano hiyo akiwa na Inter Milan ya Italia mwaka 2010.

"Nadhani kila mmoja hapa katika hii klabu ana wazo sawa na mimi, kushinda ubingwa wa michuano hii kadri tuwezavyo."

Benitez, 52, anahaha kuwatuliza mashabiki wasiomtaka klabuni Stamford Bridge, alikoanza na matokeo ya sare mbili, kichapo kimoja, kisha kushinda mechi mbili – moja ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na ile ya Ligi Kuu, ambapo sasa anageukia Klabu Bingwa ya Dunia kujaribu kurejesha imani kwa mashabiki wanaompinga katika kila mechi.

Ushindi huo wa Benitez wa mabao 6-1 dhidi ya FC Nordsjaelland katika hitimisho la mechi za makundi Ulaya na ule wa mabao 3-1 dhidi ya Sunderland – umeipa nguvu mpya Chelsea – bingwa wa kwanza wa Ulaya kuondoshwa hatua ya makundi, kufanya kweli katika michuano hii ya siku 10 jijini hapa.

Benitez amesema kuwa, licha ya ushindani anaoutarajia katika michuano hii, hajiisi kuwa kwenye presha kubwa katika mashindano, ambayo yanampa yeye nafasi ya kutwaa kombe la kwanza kama kocha wa Chelsea.

"Sina matatizo makubwa katika suala zima la shinikizo," alisema Benitez na kuongea: "Nina uzoefu wa kutosha, na ningependa kufurahia kila dakika ya uwapo wangu hapa – kwa kufanya kilicho bora na kujaribu kadri niwezavyo kushinda ubingwa."

Klabu Bingwa ya Dunia ni michuano ya siku 10 kuanzia Desemba 6 hadi 16, ambayo hushiriki mabingwa wa mabara sita yaliyo chini ya Fifa, pamoja na klabu moja mweji wa michuano hiyo, ambayo bingwa wan chi mwaandaaji uchukua nafasi hiyo.

Katika nusu fainali nyingine ya michuano hii, mabingwa wa Afrika, Al-Ahly ya Misri, wataumana na mabingwa wa Amerika Kusini, Corinthians ya Brazil.

Benitez ana rekodi mchanganyiko katika michuano hii, ambayo awali ilianza kwa kushirikisha timu nane mwaka 2000, kabla ya kuwa kubadilishwa na kubaki timu sita kuanzia mwaka 2005.

Alipoteza pambano la fainali mbele ya Sao Paulo wakati akiiongoza Liverpool mwaka 2005 – ambayo alilazimika kukosa mazishi ya baba yake kuwahi mechi y fainali, kabla ya kutwaa ubingwa akiwa na Inter Milan mwaka 2010.

Chelsea inawania kuwa klabu ya pili ya England kutwaa ubingwa wa michuano hii, baada ya Manchester United kufanikiwa kuutwaa mwaka 2008.

No comments:

Post a Comment

Pages