HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 11, 2012

EVRA: FERGIE ATATUTIMUA SOTE TUKIKOSA TENA UBINGWA


Beki wa Manchester United, Mfaransa Patrice Evra akiwajibika dimbani katika moja ya mechi za timu yake

MANCHESTER, England

“Nadhani Ferguson atamfukuza kima mmoja miongoni mwetu kama tutafanya jambo hilo tena. Hapana, niko ‘serious’ atatutimua. Litakuwa pigo kuu na aibu kwa mashabiki, wachezaji, kwa kila mtu hapa Old Trafford. Mimi nakumbuka kilichotokea mwaka jana. Tulikuwa vinara kwa tofauti ya point nane na, mwishoni, tukapoteza ubingwa wa ligi”

BEKI wa kimataifa wa Ufaransa na klabu ya Manchester United, Patrice Evra amesisitiza kwamba kocha mkuu wa Mashetani hao Wekundu wa Old Trafford, Sir Alex Ferguson anaweza kumfukuza kila mchezaji wa klabu hiyo, iwapo itashuka katika kilele cha uongozi wa Ligi Kuu.

Man United ina kumbukumbu mbya ya kufuta pengo la point inane ililokuwa nalo kileleni, kabla ya kujikuta ikipoteza nafasi ya kutwaa ubingwa kwa tofauti ya mabao, dhidi ya waliotwaa ubingwa huo majirani na mahasimu wao wakuu Manchester City.

Kauli ya Evra ilitokana na swali aliloulizwa kuwa anahisi United inaweza kurejea anguko la msimu uliopita, ambapo alijibu: “Nadhani Ferguson atamfukuza kima mmoja miongoni mwetu kama tutafanya jambo hilo tena. Hapana, niko ‘serious’ atatutimua.

“Litakuwa pigo kuu na aibu ya kila mmoja, kwa mashabiki, wachezaji, kwa kila mtu hapa Old Trafford. Mimi nakumbuka kilichotokea mwaka jana. Tulikuwa vinara kwa tofauti ya point inane na, mwishoni, tukapoteza ubingwa wa ligi.”

Man United ilipanua wigo wake wa pointi kileleni mwa msimamo na kufikia sita, baada ya kuwachapa watetezi hao kwenye Uwanja wa Etihad Jumapili, kwa mabao 3-2.

Lakini Evra, 31, anasema kwamba matokeo hayo kwao yatakuwa na maana kubwa kama watafanikiwa kushinda mechi moja baada ya nyingine, wakianza na mtanange wao wa Jumamosi dhidi ya ‘Paka Weusi’ Sunderland.

Evra akaongeza: “Uongozi wa pointi sita kileleni... ligi bado haijaisha kabisa, kuna safari ndefu kuelekea mwishoni mwa msimu. Lakini kusema kweli nina uhakika tuko tayari kwa mpambano dhidi ya Sunderland.”

Ushindi wa Man United Etihad dhidi ya Man City, ulihitimisha rasmi mbio za mabingwa hao kucheza mechi 37 nyumbani bila kufungwa, iliyoanzia msimu uliopita, lakini pia ikihitimisha ubabe wao katika msimu huu wa Ligi Kuu – ambako ilikuwa haijawahi kufungwa nyumbani wala ugenini.

Evra anaamini kwamba ushindi huo umewaongezea faida kubwa kikosini kisaikolojia na kuwapa nguvu yam bio za ubingwa msimu huu; “Ilikuwa ni jambo muhimu kuishinda Man City na kuwawashia indiketa. Kisaikolojia, ilikuwa muhimu mno.”

No comments:

Post a Comment

Pages