DAR ES SALAAM, Tanzania
BAADA ya sintofahamu ya muda
mrefu iliyokuwa imewakumba wapenzi na mashabiki wa mabingwa wa soka Tanzania,
Simba, juu ya nyota wao wa kimataifa, Mganda Emmanuel Okwi, hatimaye imebainika
amepigwa bei katika klabu ya Etolile du Sahel ya Tunisia.
Okwi ameuzwa dola 300,000 za
Marekani kwa klabu hiyo, ambako dili hilo lilikamilika leo mchana huko
Tunisia, ambako alikwenda kwa majaribio ya kujiunga na klabu hiyo kongwe nchini
humo.
Hivi karibuni, viongozi wa
Simba walikaririwa kwa nyakati tofauti wakidai kwamba, Okwi ameshindwa kuungana
na wenzake kutokana na kwenda nchini Tunisia kwa majaribio katika klabu ya
Esperance, kabla ya baadaye kugeuka na kudai kuwa yupo Etoile du Sahel.
Okwi, amekuwa na historia ya
kuumiza vichwa vya viongozi na mashabiki wa Simba mara kwa mara, kutokana na
kushindwa kujiunga kwa wakati na timu hiyo kila alipokwenda kwao kwa mapumziko.
Hivi karibuni, Okwi
alishindwa kuungana na kikosi cha Simba kilichopo nchini Oman kwa kambi
maalumu, huku viongozi wakitangaza kumtema rasmi kwenye ziara hiyo na
kumuadhibu kutokana na kuchelewa kwake.
Hivyo kwa habari hizo, ni
wazi sasa Simba imemaliza biashara na mshambuliaji huyo mahiri.
Viongozi wa juu wa Simba
walipotafutwa kwa simu jana kuzungumzia hilo, Mwenyekiti Ismail Aden Rage simu
yake haikuwa hewani, huku Makamu wake Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na Katibu Evodius
Mtawala zilikuwa zikiita bila kupokelewa.
Katika hatua nyingine, Simba ambayko
imepiga kambi Muscat, Oman, leo inashuka kwenye Uwanja wa Qaboos Sports
Complex, kukwaana na timu ya taifa ya huko iliyoshiriki michuano ya Olimpiki.
Mbali na mchezo huo, Simba
inatarajiwa kucheza mechi nyingine za kirafiki na timu za Fanja FC na timu ya
jeshi kabla ya kurejea nchini Januari 23.
No comments:
Post a Comment