Baba mzazi wa
aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Regia Mtema, Estaratus Mtemanyenza akitoa shukrani wakati wa kumbukumbu ya
kuadhimisha mwaka mmoja tangu kifo cha mbunge huyo, iliyofanyika jijini Dar es
Salaam juzi. Kulia ni Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Angella Kairuki. (Picha na Habari Mseto Blog)
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika (Kulia), akiwa katika hafla ya kumbukumbu ya mwaka mmoja wa kifo cha Regia Mtema.
Katibu wa Kamati ya Maandalizi na Msemaji wa Regia Foundation, Olivia Sanare akizungumza wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Regia Mtema.
DAR ES SALAAM, Tanzania
ALIYEKUWA Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Regia Mtema, ametimiza mwaka mmoja tangu kufariki kwake, ambapo Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, alihudhuria maadhimisho hayo na kusema demokrasia ya kweli haigaiwi katika sahani ya dhahabu, bali
kwa kuipigania.
Makamba alienda mbali zaidi na kuongeza kuwa, wanaopaswa kupigania haki hiyo ni vijana ambao wanayo nafasi kubwa katika safari ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwaka
2015.
Makamba alitoa
kauli hiyo jana usiku katika hafla ya kumbukumbu ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu
kifo cha Regia, aliyefariki kwa ajali ya gari Januari 14, mwaka jana - hafla iliyofanyiola katika
Hoteli ya Peacock jijini Dar es Salaam.
Akitoa mada
iliyohusu vijana na namna anavyomfahamu Regia, Makamba alisema kama vijana watatumika vizuri katika demokrasia, watakuwa
chachu ya maendeleo na kwamba ujana peke yake si sifa ya kuwa kiongozi.
Makamba ambaye ni
Mbunge wa Bumbuli (CCM), alisema lazima uchaguzi wa mwaka 2015 uamuliwe na
vijana kama alivyokuwa na uthubutu wa kufanya
mambo makubwa Regia.
Naibu waziri huyo
aliwataka vijana kutafakari ni kwa nini walijiandikisha kwa wingi bila ya kwenda
kupiga kura katika chaguzi mbili za 2005 na 2010 na kwamba uchaguzi ujao ni lazima wabadilike na kufanya uamuzi mgumu.
Alitoa mfano
kwamba, mwaka 2015, watajiandikisha vijana wapya
milioni 5 na kutimiza zaidi ya waliojiandikisha milioni 25, uchaguzi
utakuwa umetendewa haki na vijana.
Hata hivyo
alisema ili kusukuma gurudumu la maendeleo si lazima vijana wakagombea uongozi
katika siasa tu bali hata katika sekta
na shughuli zingine.
“Sikugombea nafasi ya uongozi katika nchi hii
kwa sababu ya kutaka ukubwa, bali nilifanya hivyo ili vijana
waige kutoka kwangu na kama sasa wengine
walivyoiga kwa Regia,” alisema Makamba
Akizungumzia
alivyomfahamu Regia, Makamba alisema alimfahamu siku chache kabla ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010,
katika midahalo iliyokuwa ikirushwa na televisheni nchini.
“Nikiwa naangalia
mdahalo wabunge waliokwenda kugombea majimboni, nilimwona Zitto, Halima na dada
mwingine ambaye sikumfahamu akiwa nao, naye akizungumza namna anavyokwenda
jimboni huku akitoa maelezo mazuri,” alisema Makamba
Makamba alisema
baadae alifahamiana zaidi kwa kuonana na kushirikiana naye katika mambo
mbalimbali bungeni ambapo alikiri Regia alikuwa ni mtu mwenye uwezo na upeo mkubwa wa
mambo.
No comments:
Post a Comment