HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 20, 2013

MCHAKATO TIKETI ZA ELEKTRONIKI WAFIKIA ASILIMIA 80


DAR ES SALAAM, Tanzania

Ujenzi wa vifaa (turnstiles) vitakavyotumika kwa ajili ya tiketi za elektroniki kwenye viwanja saba kati ya nane vitakavyotumia mfumo huo umekamilika kwa asilimia 80.

Viwanja hivyo ni Chamazi (Dar es Salaam), Jamhuri (Morogoro), Kaitaba (Bukoba), Sokoine (Mbeya), Sheikh Kaluta Amri Abeid (Arusha), na Mkwakwani (Tanga).

Wakati Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam tayari una turnstiles, Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza bado haujaruhusu ufungaji wa vifaa ukisubiri idhini kutoka kwa wamiliki wake (CCM Makao Makuu).

Vifaa vitakavyotumika kusoma tiketi za elektroniki katika viwanja hivyo vinatarajiwa kuwa vimefungwa kufikia Februari 20 mwaka huu.

Hakutakuwa na matumizi ya fedha taslimu mara baada ya mradi huo wa tiketi la elektroniki kuanza, kwani tiketi zitakuwa zikinunuliwa kwa kadi maalumu (smart card) katika vituo mbalimbali vitakavyotangazwa baadaye.

Benki ya CRDB ndiyo iliyoingia mkataba na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutengeneza tiketi za elektroniki baada ya kuibuka mshindi kwenye tenda.

WAKENYA KUCHEZESHA MECHI YA AZAM
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limewateua waamuzi kutoka Kenya kuchezesha mechi ya kwanza ya raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho kati ya Azam ya Tanzania na Al Nasir Juba ya Sudan Kusini itakayofanyika jijini Dar es Salaam kati ya Februari 15 na 17 mwaka huu.

Mwamuzi wa kati atakuwa Davies Omweno na atasaidiziwa na mwamuzi msaidizi namba moja Peter Keireini, mwamuzi msaidizi namba mbili Gilbert Cheruiyot wakati mwamuzi wa mezani Anthony Ogwayo.

Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Hassan Mohamed Mohamud kutoka Somalia. Waamuzi wa mechi ya marudiano itakayochezwa jijini Juba watatoka Rwanda wakiongozwa na Gervais Munyanziza.

CAF YATEUA WATANZANIA KUCHEZESHA CAMEROON
Waamuzi wa Tanzania wakiongozwa na Israel Mujuni wameteuliwa kuchezesha pambano la awali la raundi ya kwanza kuwania Kombe la Shirikisho kati ya UFC Haut Nkam ya Cameroon na US Bougouni ya Mali.

Kwa uteuzi huo wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Mujuni na wenzake Ali Kinduli, Samuel Mpenzu na Waziri Sheha watachezesha mechi hiyo itakayofanyika kati ya Februari 15 na 17 mwaka huu.
Pierre Alain Mouguengui kutoka Gabon ndiye atakayekuwa Kamishna wa mechi hiyo. UFC Haut Nkam na US Bougouni zitarudiana wiki mbili baadaye nchini Mali.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment

Pages