Utangulizi
Ndugu
zangu, Watanzania Wenzangu;
Ni furaha na faraja kubwa kuifikia
siku hii adhimu ya kuuaga mwaka wa 2012 na kuukaribisha mwaka 2013. Ni jambo la
bahati ambayo hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujaalia
uzima na kutuwezesha kuumaliza mwaka huu salama. Wapo ndugu, jamaa na marafiki zetu wengi
ambao wangependa kuiona siku hii lakini hawakujaaliwa. Wametangulia mbele ya
haki. Tuendelee kuwaombea kwa Mwenyezi
Mungu awape mapumziko mema. Amin. Nasi tumuombe Mola wetu atujaalie fanaka tele
katika mwaka ujao.
Mapitio
ya Mwaka 2012
Ndugu
wananchi;
Mwaka tunaoumaliza leo ulikuwa wenye mambo
mengi mazuri na mafanikio makubwa, lakini, pia, ulikuwa na changamoto zake. Baadhi
zilikuwa ngumu na zipo zilizokuwa za kusikitisha na kuhuzunisha.
Ajali za barabarani na majini
ziliendelea kupoteza maisha ya watu wengi na kusababisha majeraha na ulemavu
kwa maelfu. Ajali mbaya kuliko zote kutokea,
mwaka huu, ilikuwa ile ya meli ya MV Skagit iliyotokea tarehe 18 Julai, 2012 ambapo
watu 144 walipoteza maisha. Ajali za barabarani zilizosababisha vifo nazo
ziliongezeka kutoka 3,012 mwaka 2011
hadi kufikia 3,144 na kusababisha
vifo vya ndugu zetu 3,714.
Ndugu
Wananchi;
Kufuatia ajali ya MV Skagit ambayo ilitokea miezi 11 baada ya ile ya MV
Spice Islander, Serikali zetu mbili zimekuwa zikishirikiana kwa karibu kuhusu masuala
ya usafiri wa majini kati ya Tanzania Bara na Zanzibar. Kwa ajili hiyo SUMATRA na Zanzibar Maritime
Authority zinafanya kazi kwa karibu zaidi na kanuni za usafirishaji wa abiria
na mizigo na za usajili na ubora wa meli zimewianishwa. Ni matumaini yetu kuwa hatua hizo zitasaidia
kumaliza ajali zinazotokana na makosa ya wanadamu.
Ndugu
Wananchi;
Kwa upande wa ajali za barabarani tuliendelea
na tutaendelea kuwahimiza madereva kuheshimu Sheria za Usalama Barabarani, waepuke
uzembe na hasa ulevi wakati wa kuendesha.
Tutaendelea kuwakumbusha wenye magari kuhakikisha kuwa uzima wa magari
yao unakuwa wa kiwango cha juu. Hali kadhalika,
tumewataka Polisi waongeze ukali na kuwabana ipasavyo madereva na wamiliki wa
magari ili watekeleze wajibu wao na wasipofanya hivyo wawajibishwe
inavyostahili.
Hali
ya Usalama
Ndugu
wananchi;
Tunaumaliza mwaka huu nchi yetu ikiwa shwari,
salama na tulivu. Tuombe Mungu hali hii
iendelee mwaka 2013 na idumu milele. Mipaka
ya nchi yetu ipo salama na uhusiano na majirani na nchi zote duniani ni mzuri. Tunaendelea kutafuta suluhu ya mgogoro wa mpaka
kati ya nchi yetu na Malawi katika Ziwa Nyasa kwa njia ya mazungumzo. Suala
hilo limewasilishwa kwa pamoja na Serikali zote mbili kwa Mheshimiwa Joaquim
Chissano, Mwenyekiti wa Umoja wa Viongozi Wastaafu wa Afrika kwa ajili kuzisaidia
nchi zetu kupata ufumbuzi. Matumaini
yetu ni kuwa viongozi hao watalishughulikia suala hili mapema iwezekanavyo.
Ushirikiano
wa Kanda
Ndugu
Wananchi;
Ushirikiano wetu wa kikanda katika
Jumuiya ya Afrika Mashariki na katika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika
(SADC) unaendelea vizuri. Mwaka huu nchi
yetu imepewa heshima kubwa ya kuwa Mwenyekiti wa Chombo cha SADC
kinachoshughulikia masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama.
Jukumu hilo ni zito na hasa katika kipindi hiki ambapo kuna changamoto
za kisiasa na kiusalama katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,
Madagascar na Zimbabwe. Nchi yetu
inatarajiwa kuongoza juhudi za kupata ufumbuzi wa migogoro hiyo migumu. Ndiyo maana tulifanya Mkutano Maalum wa Wakuu wa Nchi za SADC hapa Dar es
Salaam tarehe 7 na 8 Desemba, 2012. Mwaka
ujao, kwa kushirikiana na wenzetu, tutaendeleza juhudi zetu. Ni matumaini yangu kuwa tukipata ushirikiano
wa viongozi na wananchi wa nchi husika na jumuiya ya kimataifa tutapata ufumbuzi
tunaotaka.
Ndugu
Wananchi;
Kwa upande wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki, tumeendelea kushuhudia Jumuiya hiyo na harakati za utangamano zikizidi
kustawi. Jengo la Makao Makuu ya Jumuiya
limekamilika na kuzinduliwa rasmi tarehe 28 Novemba, 2012. Siku hiyo hiyo kule Athi River, Kenya,
barabara ya kutoka Arusha hadi Athi River ilizinduliwa. Barabara hii ni moja ya miradi kadhaa
inayotekelezwa kwa pamoja na nchi wanachama wa Jumuiya wa Afrika Mashariki.
Mchakato wa utangamano wa kiuchumi wa
Afrika Mashariki unaendelea kwa kasi. Tanzania
ikiwa sehemu kamili ya mchakato huo, lazima tuhakikishe kuwa tunakwenda nao
sambamba. Tusikubali kuachwa nyuma wala
kuwa chanzo cha kuuchelewesha mchakato huo bila ya sababu za msingi. Utangamano una maslahi kwa nchi yetu na
manufaa yake ni makubwa. Kwa mfano,
mauzo yetu katika soka la Afrika Mashariki yameongezeka sana kutoka dola za
Kimarekani milioni 58.6 mwaka 2000 hadi kufikia dola za
Kimarekani milioni 409 mwaka 2011.
Jumuiya imekuwa kichocheo muhimu cha kukuza
uzalishaji, ajira na uchumi hapa nchini.
Kwa ukubwa wa nchi yetu na rasilimali tulizonazo tuna matumaini makubwa
ya kunufaika zaidi siku za usoni. Naweza
kuthubutu hata kusema kuwa Tanzania inaweza kunufaika zaidi kuliko nchi
nyingine wanachama wa Jumuiya hiyo. Kinachotakiwa
ni sisi kujipanga vizuri kwa sera na mipango ili tuzitumie fursa tulizonazo kwa
maslahi ya uchumi na maendeleo ya nchi yetu na watu wake. Tuache woga,
tujiamini.
Matishio
ya Usalama
Ndugu
Wananchi;
Licha ya kumaliza mwaka nchi ikiwa
shwari na yenye amani na utulivu, yalikuwepo matukio yaliyotishia usalama wetu. Bahati mbaya na kwa masikitiko makubwa matukio
hayo yalisababishwa na baadhi ya viongozi wa dini na siasa na wafuasi wao. Kwa kweli kwa mara ya kwanza nchi yetu ilifikishwa
kwenye hatari ya kutokea mgawanyiko mkubwa wa Watanzania au hata mapigano ya
raia kwa misingi ya dini zao. Bahati
nzuri hilo halikutokea na Mungu aliepushe lisitokee kamwe.
Nimeshalisemea jambo hili siku za
nyuma na napenda kurudia tena leo kuwasihi Watanzania wenzangu kupima athari za
kauli zetu na matendo yetu kwa mustakabali wa jamii yetu, nchi yetu na watu
wake. Viongozi wa dini, waumini na
viongozi wa siasa na wafuasi wao wanao wajibu maalum wa kuhakikisha kuwa Watanzania
wanaendelea kuishi kwa upendo, amani na ushirikiano bila kujali tofauti ya dini
zao, makabila yao, rangi zao au maeneo watokako. Hiyo ndiyo sifa ya nchi yetu tunayoijua sote
ambayo ni njema na watu wengi wanataka kuja kujifunza kwetu na wale wenye shida
wanatamani wawe kama sisi. Hii ni tunu
muhimu ya taifa ambayo tusikubali kuipoteza kwa maslahi binafsi ya watu
wachache.
Ndugu
Wananchi;
Wakati wo wote, lazima tutambue
umuhimu wa kuvumiliana na kuheshimiana kwa tofauti zetu za kidini, rangi,
kabila, tutokako na ufuasi wa vyama vya siasa.
Lazima pia tuhakikishe kuwa tunaheshimu
sheria na taratibu zinazotawala mikutano na maandamano. Tukiyazingatia hayo nchi yetu itakuwa haina
tishio lo lote kwa amani na usalama wake.
Yasipozingatiwa tunaiweka nchi yetu hatarini. Sisi katika Serikali tutakuwa hatuna la
kufanya bali kutimiza wajibu wetu wa kulinda usalama wa raia na nchi yetu. Wahusika watachukuliwa hatua na vyombo vya
usalama na kisheria kwa mujibu wa sheria za nchi. Tulifanya hivyo mwaka huu na hatutakuwa na
ajizi kufanya hivyo siku yo yote kama hapana budi.
Uhalifu
Unapungua
Ndugu
Wananchi;
Inatia
moyo kuona kuwa mwaka huu makosa ya jinai yalipungua na kufikia 66,255 yakilinganishwa na makosa 69,678 ya mwaka jana au 94,390 ya mwaka juzi. Hii inathibitisha kuimarika kwa kazi nzuri
inayofanywa na Jeshi la Polisi wakishirikiana na wananchi na vyombo vingine vya
usalama. Pamoja na hayo lazima tuongeze
juhudi za kupambana na uhalifu kwani bado matukio ni mengi mno na upungufu bado
ni mdogo. Tutaendeleza kazi tuifanyayo
sasa ya kuliimarisha Jeshi la Polisi kwa rasilimali watu, zana na vitendea kazi
husika.
Uhalifu
wa Kimtandao
Ndugu
Wananchi;
Tutaongeza nguvu katika kupambana na
uhalifu unaoendeshwa na mitandao ya uhalifu ndani na nje ya nchi. Mitandao hiyo hasa imekuwa inajihusisha na biashara
ya kusafirisha wanadamu, biashara ya dawa za kulevya na biashara ya nyara za
Serikali.
Mapambano dhidi ya uhalifu wa
kimtandao yametuwezesha kukamata wahamiaji haramu 4,765 na tayari 1,611
wamerudishwa kwao. Kwa upande wa dawa za
kulevya watuhumiwa 6,929 walikamatwa
mwaka huu ukilinganisha na 209 mwaka
2011. Kilo 55,285 za dawa za kulevya
zilikamatwa mwaka huu ukilinganisha na kilo 17,752.4 mwaka jana. Kwa
upande wa nyara za Serikali, zilizokamatwa ni 1,416 na kati ya hizo 736 ni meno ya tembo. Watuhumiwa 1,037 walikamatwa na kesi 746
zipo Mahakamani katika hatua mbalimbali.
Ndugu
Wananchi;
Taarifa hizi zinathibitisha kuimarika
kwa jitihada za kupambana na uhalifu wa kimtandao. Tutaimarisha zaidi jitihada zetu mwaka 2013
ili tupate mafanikio zaidi. Tutaviongezea uwezo wa rasilimali watu, zana,
vifaa na fedha za uendeshaji vyombo vyetu vya usalama vinavyoongoza mapambano
haya.
Tutaimarisha na kuendeleza ushirikiano
baina ya nchi yetu na nchi jirani na nyinginezo duniani. Hii itasaidia kutuongezea uwezo wa kupambana
na mitandao ya uhalifu ndani ya nchi, kikanda na kimataifa. Pia tutazipitia upya sheria za kupambana na makosa
haya kwa nia ya kuziboresha.
Ndugu
Wananchi;
Katika mwaka 2013, tutapanua na
kuimarisha huduma ya matibabu kwa watu walioathirika na dawa za kulevya kote
nchini. Tutakamilisha ujenzi wa kituo
cha Dodoma na kujenga kingine kipya Dar es Salaam. Natoa wito kwa wale wote walioathirika au
watu wenye watoto au rafiki au jamaa walioathirika waende hospitali kupatiwa
matibabu kwani matibabu hayo ni bure.
Hali
ya Uchumi
Ndugu
wananchi;
Katika mwaka 2012, tunaoumaliza leo, uchumi wa nchi yetu uliendelea kukua na kuimarika
licha ya kuwepo kwa changamoto za upatikanaji wa umeme, kupanda kwa bei za mafuta
na chakula duniani na uhaba wa mvua katika maeneo mengi nchini uliosababisha kupungua
kwa uzalishaji na kupanda kwa bei za vyakula nchini. Pia, licha ya kuendelea kwa msukosuko wa uchumi
wa dunia na hasa katika Bara la Ulaya ambako ni soko kuu la bidhaa zetu na watalii. Mategemeo yetu ni kuwa, mwaka huu, uchumi
wetu utakua kwa asilimia 6.8 na mwakani (2013) utakua kwa asilimia 7.0 ukilinganisha na asilimia
6.4 mwaka 2011.
Kwa jumla, ukilinganisha na makadirio
ya IMF ya kiwango cha ukuaji wa uchumi wa dunia kuwa asilimia 3.3 mwaka huu, ni dhahiri kuwa uchumi wetu unakua kwa kasi
nzuri na kuifanya Tanzania iendelee kuwa miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake
unakua kwa kasi kubwa.
Hali hii ya uchumi wetu ina maana kubwa
mbili. Kwanza, kwamba uchumi wetu
umejenga uhimilivu dhidi ya misukosuko ya uchumi wa dunia. Na pili, kwamba shughuli za uzalishaji na
huduma zinazidi kukua na mauzo ya bidhaa ndani na nje ya nchi yameongezeka. Kuongezeka kwa mauzo ya nje kumefanya akiba
yetu ya fedha za kigeni kufikia dola za Marekani
bilioni 3.9 mwezi Novemba, 2012 kiasi ambacho kinatuwezesha kuagiza bidhaa
kutoka nje kwa miezi minne.
Ndugu
Wananchi;
Makusanyo ya mapato ya Serikali
yatokanayo na kodi yalifikia shilingi
bilioni 580.3 mwezi Oktoba, 2012 ikilinganishwa na shilingi bilioni 479.3 mwezi Oktoba 2011. Matarajio yetu ni kufanya vizuri zaidi mwaka
2013 kwa mapato yatokanayo na kodi na yale yasiyotokana na kodi ambayo bado ni
chini ya lengo.
Ndugu
Wananchi;
Mfumuko wa bei kuwa juu ni changamoto
ambayo tunaendelea kuikabili ili kuleta utulivu uliokamilifu kwa uchumi wetu na
kuwapunguzia ukali wa maisha wananchi wa Tanzania. Serikali imechukua hatua kadhaa kudhibiti
hali hiyo na mafanikio ya kututia moyo yameanza kuonekana. Kwa mfano, mfumuko wa bei umepungua kutoka asilimia 19.8 mwezi Desemba 2011 hadi asilimia 12.1 mwezi Novemba, 2012. Kiwango hicho bado ni cha juu na
hakikubaliki. Tutaendelea kuchukua hatua
zaidi ili tuweze kufikia lengo letu la mfumuko wa bei kuwa chini ya asilimia 10 ifikapo mwezi Juni, 2013.
Miongoni mwa mambo tuliyopanga kufanya
ili kupunguza mfumuko wa bei ni kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme na
kudhibiti mwenendo wa bei ya mafuta. Kufanya
hivyo kutasaidia kupunguza gharama za uzalishaji na uchukuzi wa bidhaa. Aidha,
tutaendelea kutekeleza mipango na mikakati ya kukuza na kuboresha kilimo nchini
kwa lengo la kujihakikishia usalama wa chakula, kukuza pato la taifa na
kupunguza umaskini hasa miongoni mwa wakulima.
Utekelezaji
wa Miradi ya Maendeleo
Ndugu
wananchi;
Mwaka huu tunaoumaliza leo ulikuwa na
mafanikio ya kutia moyo kwa upande wa utekelezaji wa miradi ya kuendeleza miundombinu
nchini. Tumeshuhudia miradi ya barabara,
madaraja, viwanja vya ndege, reli, bandari, umeme na maji ikikamilika, au
kuanzwa au utekelezaji wake ukiwa unaendelea.
Hakika lengo la kuunganisha mikoa yote ya Tanzania Bara kwa barabara za
lami siyo ndoto tena bali ni jambo la uhakika na litatimia muda si mrefu
ujao.
Ndugu
Wananchi;
Kwa upande wa reli, mwaka huu tumeendelea
kukarabati reli ya kati na kurejesha usafiri wa treni kutoka Dar es Salaam
kwenda Mwanza na Kigoma. Mwaka ujao
(2013) tutaendeleza kazi ya ukarabati wa reli hiyo muhimu na kuzidi kuboresha
huduma. Tumekamilisha ujenzi wa viwanja
vya ndege vya Mpanda na Songwe na tunaendelea kuboresha viwanja vya Tabora,
Kigoma, Bukoba, Mafia, Mwanza na Zanzibar.
Tumeendelea kujenga na kupanua miundombinu ya maji nchini na kuboresha upatikanaji
wa maji salama kwa Watanzania. Kwa mwaka huu usambazaji wa maji salama umefikia asilimia 87 kwa watu wa mijini na asilimia 61.5 vijijini. Tutaendeleza
kazi hiyo mwaka 2013.
Msongamano
wa Magari Dar es Salaam
Ndugu
Wananchi;
Katika Jiji la Dar es Salaam tumeendelea
na tutaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kupunguza msongamano wa magari unaozidi
kuongezeka. Barabara mpya zimejengwa na zinaendelea
kujengwa ndani na kuzunguka Jiji.
Barabara kadhaa zimepanuliwa na nyingine zitaendelea kupanuliwa. Ujenzi wa miundombinu (barabara na vituo) ya
mabasi yaendayo haraka umeanza. Mwaka
2013 ujenzi wa barabara za juu ya nyingine katika makutano ya TAZARA utaanza na
matayarisho ya kufanya hivyo kwa makutano ya Ubungo yatakamilishwa.
Tumetimiza ahadi yetu ya kutumia treni
kusafirisha abiria katika jiji la Dar es Salaam. Usafirishaji umeanza na unaendelea kati ya
Stesheni na Ubungo na kutoka Stesheni ya TAZARA hadi Pugu – Mwakanga. Mwaka ujao tutaendelea kuimarisha usafiri huo
kwa kuongeza treni na idadi ya safari.
Tayari Mshauri Mwelekezi ameshateuliwa kufanya upembuzi yakinifu na
kushauri kuhusu kupanua huduma hiyo mpaka ifike Tegeta, Bunju, Kimara,
Luguruni, Kibaha, Mbagala-Rangi Tatu na Kongowe. Ushauri huo pia utahusu kuwa na huduma bora
ya usafiri wa treni katika Jiji la Dar es Salaam kwa maana ya aina ya njia,
vichwa vya treni na mabehewa. Tuliamua
kuanza na reli na treni iliyopo, lakini nia yetu ni kufanya vile hasa
inavyotakiwa iwe kwa usafiri wa treni mijini.
Umeme
Ndugu
Wananchi;
Mwaka tunaoumaliza leo haukuwa rahisi
kwa upande wa upatikanaji wa umeme.
Mabwawa ya kuzalisha umeme ya Kidatu, Kihansi, Mtera, Pangani na Nyumba
ya Mungu yameendelea kutokuwa na maji ya kutosha kwa sababu ya uhaba wa
mvua. Hivyo basi taifa limelazimika kutegemea
umeme wa kukodi unaozalishwa kwa kutumia mafuta. Umeme huo umekuwa wa gharama kubwa na hivyo
kuwa mzigo mkubwa kwa TANESCO na taifa. Serikali imeendelea kushirikiana na
TANESCO na kuisaidia kubeba mzigo huo. Tutaendelea
kufanya hivyo mwaka ujao na mpaka tutakapofikia hatua ya kutokuwa na ulazima wa
kutumia umeme wa kukodi.
Ndugu
Wananchi;
Mtakumbuka kuwa tulipopata tatizo la
ukame na upungufu wa umeme mwaka 2006/2007, Serikali yetu iliazimia kuongeza uzalishaji
wa umeme kutokana na vyanzo vingine vikiwemo gesi asili, makaa ya mawe, upepo
na jua. Nafurahi kusema kuwa, tangu
wakati ule Serikali imeiwezesha TANESCO kujenga vituo vitatu vinavyozalisha MW 245 kwa kutumia gesi.
Hatukuweza kuongeza zaidi uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi kwa
sababu ya kiasi cha gesi kinacholetwa Dar es Salaam kutoka Songo Songo kuwa
kidogo. Ndiyo maana tukaamua kujenga
bomba jipya kubwa la kusafirisha gesi kutoka Songo Songo hadi Dar es Salaam.
Ndugu
Wananchi;
Kwa nia ya kutaka kuhakikisha kuwa
kutakuwa na gesi ya kutosha kuzalisha umeme mwingi zaidi pale inapohitajika,
ikaamuliwa bomba hilo liendelezwe mpaka visima vya gesi vya Mtwara. Ujenzi wa bomba hilo umeanza mwezi Novemba,
2012 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 18. Gesi itakayopatikana ina uwezo wa kuzalisha MW 3,000 za umeme. Tayari mipango inaendelea
ya kujenga mitambo ya kuzalisha MW 900
pale Kinyerezi ili mara gesi itakapofika umeme uzalishwe. Hatua hiyo itatuwezesha kuung’oa mzizi wa
fitina wa mgao wa umeme na mzigo wa kununua umeme ulio ghali.
Utafutaji
wa Gesi
Ndugu
Wananchi;
Tangu mwaka 2010 gesi nyingi
imegundulika baharini na nchi kavu katika Mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani.
Utafutaji bado unaendelea na tuna matumaini kuwa gesi nyingi zaidi huenda ikagundulika. Hivi sasa Serikali inaandaa sera na sheria
mpya ya gesi ili kuboresha zinazotumika wakati huu. Nia yetu ni kutaka kuhakikisha kuwa
rasilimali hii adhimu inasimamiwa vizuri kwa manufaa ya nchi yetu na watu wake
pamoja na kulinda maslahi ya wawekezaji.
Napenda kutumia nafasi hii
kuwahakikishia ndugu zetu wa kule gesi ilipogunduliwa au popote
itakapogundulika, kuwa watanufaika sawia na katu hawatasahaulika. Rai yao ya kutaka na wao wanufaike inakubalika
na Serikali inajiandaa hivyo. Viongozi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa mfano,
wanajua maelekezo niliyotoa kuhusu kuiandaa miji ya Mtwara na Lindi kupokea
uchumi wa gesi.
Lakini, sharti la kutaka gesi
isisafirishwe kwenda kokote na kwamba kila kitu kifanyike kwao halikubaliki. Rasilimali
inayopatikana po pote katika nchi hii ni mali ya taifa zima na hutumika kwa
manufaa ya taifa. Katu siyo mali ya watu
wa pale ilipogundulika au pale shughuli hizo zinapofanyika. Jumla ya makusanyo ya
mapato yatokayo sehemu zote za nchi yetu na kutokana na vyanzo mbalimbali ndiyo
yanayotumika kuhudumia watu wote po pote walipo.
Ndugu
Wananchi;
Huu ni msingi mzuri, ni sera nzuri na ni jambo
jema la tunu, tulilorithi kwa
waasisi wa Taifa letu, ambalo hatuna budi kulienzi na kulidumisha. Nawasihi wanasiasa wenzangu tusiwaelekeze kwenye
mambo mabaya wananchi tunaodai kuwapenda. Kutafuta umaarufu kwa agenda
zinazopandikiza chuki kwa watu na kuligawa au kulibomoa taifa, ni upungufu
mkubwa wa uongozi na uzalendo. Tuache
siasa za ubarakara na kuwapa watu matumaini yasiyotekelezeka. Nawaomba wananchi msiwasikilize, si watu
wanaowatakia mema na wala hawaitakii mema nchi yetu.
Elimu
Ndugu
wananchi;
Tumeendelea kupata mafanikio katika
utekelezaji wa sera yetu ya kupanua fursa ya elimu kwa Watanzania katika ngazi
zote. Mwaka huu vijana wetu wengi zaidi walijiunga
na elimu ya msingi, sekondari, ufundi na elimu ya juu. Hivi sasa tunaelekeza juhudi zetu zaidi
katika kuongeza ubora wa elimu. Kwa ajili hiyo, tumechukua hatua za makusudi
za kupanua mafunzo na ajira za walimu wa shule za msingi na sekondari. Kwa mfano,
mwaka huu walimu 24,621 wapya
waliajiriwa kati yao 11,379 wa shule
za msingi na 13,242 wa shule za
sekondari. Januari, 2013 tunategemea
kuajiri walimu 28,746 kati yao 14,606 wa shule za msingi na 14,060 watakuwa wa shule za sekondari.
Kwa sababu hiyo, uwiano wa mwalimu kwa
wanafunzi umeendelea kuwa mzuri. Hivi
sasa kwa shule za msingi uwiano umefikia 1:46
ukilinganisha na 1:56 mwaka 2005. Uwiano
unaostahili ni 1:40. Kwa upande wa
sekondari uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi hivi sasa ni 1:29 ukilinganisha na 1:20
unaostahili. Kutokana na upanuzi wa vyuo
vya kufundisha walimu nchini, bila ya shaka baada ya miaka mitatu hivi upungufu
wa walimu wa shule za msingi na sekondari haitakuwa kilio tena.
Ndugu
Wananchi;
Upatikanaji wa vitabu nao unazidi kuwa
bora. Hivi sasa uwiano wa kitabu kwa mwanafunzi
ni 1:3 kwa shule ya msingi na
sekondari 1:3 ukilinganisha na 1:5 kwa shule za msingi na sekondari 1:4 mwaka 2009. Hata hivyo, tutaendelea kuongeza mgao wa
fedha katika bajeti ya elimu ili kuongeza upatikanaji wa vitabu na vifaa
vingine vya kusomea na kufundishia. Tunataka
katika muda mfupi ujao uwiano uwe 1:1.
Kwa upande wa maabara za sayansi, tarehe
4 Novemba, 2012, nilipokuwa kwenye ziara ya Mkoa wa Singida, nilitoa agizo la kutaka
ndani ya miaka miwili, kuanzia mwaka 2013, kila shule ya sekondari ya kata nchini
iwe na majengo ya maabara yaliyokamilika.
Yawe pia yanatumika kwa maana ya vifaa na mahitaji muhimu. Nimewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya
kuhakikisha kuwa agizo hili linatekelezwa kwa ukamilifu. Kuanzia sasa, katika ziara zitakazofanywa Mikoani
na mimi, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu tutapenda kupata taarifa ya maendeleo ya
utekelezaji wake.
Ndugu
Wananchi;
Kwa upande wa ufundishaji imedhihirika
kwamba mkakati maalum unahitajika kuboresha ufundishaji wa masomo ya hisabati,
kiingereza na sayansi katika shule za msingi na sekondari. Matokeo ya mitihani ya darasa la saba na
kidato cha nne kwa miaka mingi sasa yanathibitisha haja hii. Sasa wakati umefika kwa suala hili kulipa
uzito unaostahili. Tutafanya hivyo
kuanzia mwaka 2013.
Afya
Ndugu
Wananchi;
Mwaka 2012 ulikuwa na mafanikio mengi
ya kutia moyo kwa upande wa sekta ya afya nchini pamoja na kuwepo kwa
changamoto mbalimbali. Kazi ya kusogeza huduma ya afya karibu na wanapoishi watu
kwa maana ya kujenga zahanati, vituo vya afya, hospitali mpya na kuimarisha
zilizopo iliendelea kutekelezwa kwa mafanikio kote nchini.
Hali kadhalika, uwezo wetu wa ndani wa
uchunguzi na tiba ya magonjwa makubwa umezidi kuimarika mwaka huu. Upatikanaji
wa dawa, vifaa vya uchunguzi na vifaa tiba umeendelea kuboreshwa. Aidha, mafunzo na ajira za madaktari, wauguzi
na wataalamu wengine wa afya vimeendelea kuongezwa. Kituo cha Tiba ya Maradhi ya Moyo kimekamilika
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na mwaka ujao (2013) shughuli za
upasuaji na nyinginezo husika kutibu maradhi ya moyo zitakuwa zimeboreshwa sana. Upanuzi mkubwa wa Hospitali ya Saratani ya
Ocean Road umekamilika. Kwa ajili hiyo,
huduma zitakuwa bora zaidi na msongamano wa wagonjwa hospitalini hapo utakuwa
umemalizika. Ujenzi wa hospitali kubwa
ya kisasa katika Chuo Kikuu cha Dodoma unaendelea vizuri na inatarajiwa
kukamilika mwaka 2014. Hospitali hiyo
itatumika kufundishia wanafunzi wa udaktari na uuguzi.
Ndugu
Wananchi;
Mwaka huu pia, tumekamilisha matayarisho ya kuanza ujenzi wa hospitali
kubwa na ya kisasa kabisa kule Mlonganzila, Dar es Salaam. Ujenzi utaanza Februari 2013 na kukamilika Februari,
2015. Hospitali hii pia itakuwa ya
kufundishia wakati Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili kitakapohamishia
sehemu kubwa ya shughuli zake huko Mloganzila.
Mchakato wa ujenzi wa Chuo hicho nao unakaribia kuanza. Kuwepo kwa hospitali hizi kutaongeza sana uwezo
wetu wa ndani wa uchunguzi na tiba. Sasa
naweza kuthubutu kusema kuwa safari ya kupunguza wagonjwa tunawaopeleka nje
tumeianza kwa dhati.
Ndugu
Wananchi;
Tumeendelea kupata mafanikio katika mapambano
dhidi ya magonjwa makubwa yanayosababisha vifo vingi kama vile UKIMWI, Kifua Kikuu
na Malaria. Maambukizi na vifo vinazidi
kupungua. Pia vifo vya kina mama na watoto vinaendelea
kupungua.
Kwa mujibu wa taarifa za mwaka huu za
Shirika la Afya Duniani, vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano hapa Tanzania
vimepungua kutoka vifo 81 kwa kila watoto
1000 waliozaliwa hai mwaka 2009 hadi kufika vifo 65.2 mwaka 2011 na vifo vya watoto
wachanga vimepungua kutoka vifo 51 kwa kila watoto 1000 waliozaliwa hai mwaka
2009 na kufikia vifo 45 mwaka 2011.
Mafanikio haya yanaiweka Tanzania katika orodha ya nchi 10 zinazofanya vizuri duniani katika kupunguza vifo vya watoto
wenye umri wa chini ya miaka mitano.
Ndugu
Wananchi;
Hatuna budi kufahamu kuwa haya ni matokeo ya kufanya vizuri kwenye chanjo
kwa watoto ambayo imefikia wastani wa asilimia
90. Pia imechangiwa na mafanikio
yetu katika kupunguza maambukizi ya malaria na UKIMWI kwa watoto. Naamini tutapata mafanikio makubwa zaidi
kuanzia mwaka 2013 tutakapoanza chanjo dhidi ya kichomi (pneumonia) na ugonjwa
wa kuharisha kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano. Aidha, tukiendelea kutekeleza kwa dhati mpango
wa kila mtoto kulala kwenye chandarua kilichotiwa dawa na ule Mpango Kabambe wa
Kuzuia Maambukizi ya Mama Kwenda kwa Mtoto niliouzindua kule Lindi tarehe 1
Desemba, 2012, mambo yatakuwa vizuri zaidi.
Sensa
ya Watu na Makazi
Ndugu
wananchi;
Leo asubuhi kwenye viwanja vya Mnazi
Mmoja nilitangaza matokea ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika mwezi Agosti,
mwaka 2012. Matokeo haya yanaonyesha
kwamba idadi ya watu nchini Tanzania ni milioni
44,929,002 kati yao watu milioni 43,625,434
wanaishi Tanzania Bara na milioni 1,303,568
wanaishi Zanzibar. Ukilinganisha na Sensa
ya mwaka 2002 tulipokuwa na watu milioni 34.4,
hili ni ongezeko la watu milioni 10.5
au wastani wa asilimia 2.6 kwa
mwaka.
Matokeo haya yana maana kubwa kwa
Serikali na kwa kila mmoja wetu. Kwa
kasi hii ya ongezeko la watu ifikapo mwaka 2016 Tanzania itakuwa na watu milioni 51.6. Hii
ni idadi kubwa sana ya watu inayoleta changamoto kwa Serikali na
jamii. Hatuna budi kutambua maana ya
idadi hiyo ya watu na kujipanga vyema kukidhi mahitaji yao na hasa kuhakikisha
kuwa maskini hawaongezeki na huduma zinatosheleza mahitaji na zina ubora wa
juu. Kazi hiyo lazima ianze sasa na
ionekane katika Mipango ya Maendeleo.
Ndugu
Wananchi;
Kwa upande wetu, sisi wananchi,
taarifa hii inamlazimu kila mmoja wetu atambue kuwa kwa kasi hii, siku za usoni
nchi yetu itakuwa na watu wengi, hivyo ushindani kwa rasilimali utakuwa
mkubwa. Watakaofanikiwa wakati huo ni
wale wenye familia ndogo au zile ambazo zimepanga uzazi. Tukipanga uzazi tunajipa nafasi ya kutunza na
kulea vizuri watoto wetu na kuwapatia mahitaji yao muhimu ya maisha.
Ndugu
Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kurudia
kuwashukuru wananchi wenzangu wote kwa ushirikiano wenu uliowezesha zoezi zima
kufanikiwa kiasi hiki. Aidha,
nawashukuru kwa dhati viongozi, watendaji wakuu na maofisa wote waliopanga,
kuratibu, kusimamia na kutekeleza zoezi la kuhesabu watu. Natoa shukrani maalum kwa Kamati ya Kitaifa
ya Sensa, Kamati za Sensa za Mikoa na Wilaya, Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Jamhuri
ya Muungano na Afisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar na makarani wote wa sensa. Penye nia pana njia. Tumeweza kushinda changamoto zote na
kuwapatia Watanzania nyenzo muhimu ya kupanga mipango ya maendeleo yao.
Vitambulisho
vya Taifa
Ndugu
wananchi;
Mwaka huu tumeanza zoezi la kusajili
watu na makazi kwa ajili ya kuandaa kutoa Vitambulisho vya Taifa kuanzia mwaka
2013. Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa
ilifanya zoezi la majaribio katika mkoa wa Dar es Salaam na wilaya ya Kilombero
ambalo lilifanikiwa. Hivi sasa wanaendelea
na zoezi hilo Zanzibar. Maandalizi kwa ajili ya kutekeleza zoezi la kutoa
vitambulisho nchi nzima kuanzia mwaka 2013 yanakwenda vizuri. Napenda kuwasihi wananchi wenzangu wakati
utakapofika kutoa ushirikiano unaostahili kwa maafisa watakaohusika na
kukusanya taarifa na kutoa vitambulisho ili zoezi lifanikiwe ipasavyo. Nawaomba muitumie vizuri fursa hii ya
kujisajili na kupata vitambulisho.
Mchakato
wa Katiba Mpya
Ndugu
wananchi;
Mtakumbuka
kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nililiyoiunda tarehe 1 Mei, 2012 ilianza kazi
yake rasmi tarehe 29 Juni, 2012 na inaendelea vyema. Mpaka sasa Tume imekamilisha hatua ya kwanza
ya kukusanya maoni ya mtu mmoja mmoja katika Mikoa yote nchini. Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru
wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kutoa maoni.
Zoezi linalofuata ni la kukusanya maoni ya makundi maalumu kuanzia mwezi Januari, 2013. Natoa wito kwa makundi hayo nayo kushiriki vizuri
kwenye hatua hii muhimu. Baada ya hatua
hiyo kukamilika, Tume itaandaa Rasimu ya Katiba ambayo wanategemea itakuwa
tayari mwezi Mei, 2013.
Ndugu Wananchi;
Kwa mujibu
wa ratiba ya Tume, rasimu hiyo itawasilishwa kwenye Vikao vya Mabaraza ya
Katiba vitakavyofanyika kati ya mwezi Juni na Agosti, 2013. Tume
itatangaza muundo na namna ya kuwapata Wajumbe wa Mabaraza hayo na utaratibu
utakaotumika wakati wa kujadili na kutoa maoni juu ya Rasimu ya Katiba wakati
huo ukiwadia.
Baada ya kukamilika
kwa Vikao vya Mabaraza ya Katiba, Tume itakamilisha Rasimu ya Katiba ambayo itachapishwa
kwenye Gazeti la Serikali kama yalivyo matakwa ya Sheria. Aidha, itachapishwa katika magazeti ya
kawaida kwa wananchi kusoma. Mwezi
Novemba, 2013 rasimu hiyo itawasilishwa kwenye Bunge Maalum kujadiliwa na
kupitishwa. Baada ya Bunge Maalum kupitisha
Rasimu ya Katiba, Rasimu hiyo itapelekwa kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho
kupitia kura ya maoni.
Ndugu Wananchi;
Matarajio
yetu ni kwamba kama kila kitu kitakwenda kama inavyotarajiwa nchi yetu itakuwa
na Katiba Mpya iliyotokana na maoni na matakwa ya wananchi ifikapo mwaka 2014. Mwaka huo Muungano wetu utakuwa unatimiza
miaka 50 hivyo hiyo itakuwa zawadi ya tunu kubwa. Tukifanikiwa kupata Katiba mpya wakati huo, tutafanya
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa kutumia Katiba hiyo. Inshallah, Mwenyezi Mungu atajaalia baraka
zake, nia yetu njema itatimia. Pamoja na
hayo, natoa wito kwenu wananchi wenzangu kushiriki kwa ukamilifu katika hatua
zote za mchakato ili tuweze kujenga muafaka kuhusu Katiba tunayoitaka.
Marekebisho ya Sheria
Ndugu
Wananchi;
Katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi wa Februari, 2012, nilieleza
kwamba katika mazungumzo baina ya Serikali na
vyama vya siasa na wadau wengine juu ya marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba tulikubaliana tushughulikie marekebisho ya Sheria hiyo hatua kwa
hatua. Tulikubaliana kuanza na mambo
yanayohusu Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni ya Wananchi ili Tume iundwe na
ianze kazi. Baada ya hapo tuangalie
vipengele vinavyohusu Bunge Maalum na Kura ya Maoni.
Tulifanya hivyo kuhusu Tume ya Katiba na sasa tunajiandaa
kuanza mazungumzo kuhusu ngwe iliyobaki yaani, Bunge Maalum na Kura ya Maoni. Kama mazungumzo yatakamilika mapema kunako
Januari, 2013 mapendekezo hayo yatafikishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano
katika kikao cha Februari kwa uamuzi. Vinginevyo itakuwa katika Bunge la Aprili,
2013.
Ndugu
Wananchi;
Kuhusu Kura ya Maoni, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inaelekeza
kuwa Kura ya Maoni itatungiwa Sheria yake maalum. Ni matumaini yangu kuwa matayarisho yake
yataanza mapema iwezekanavyo. Nawasihi
wananchi wenzangu, viongozi wa vyama vya siasa na asasi za kijamii tuwe
watulivu, tuendelee kushirikiana katika mchakato huu wa Katiba mpaka
tulifikishe jahazi ufukweni salama kwa mustakabali mwema wa nchi yetu na watu
wake.
Mfumo
wa Dijitali
Ndugu
wananchi;
Bila ya shaka mtakumbuka taarifa za Wizara
ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na Tume ya Mawasiliano kwamba kuanzia
tarehe 1 Januari, 2013 nchi yetu itahamia katika mfumo wa mawasiliano unaotumia
teknolojia ya dijitali (au kidijiti kwa tafsiri ya BAKITA) badala ya huu wa
sasa wa analojia. Uamuzi huu unakuja kufuatia uamuzi wa kimataifa kwamba nchi
zote duniani ziwe zimeingia kwenye mfumo huu ifikapo mwaka 2015. Pia unazingatia uamuzi wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki kwa nchi zetu kuanza safari hiyo tarehe 1 Januari, 2013.
Hapa nchini zoezi hili litafanyika kwa awamu. Litaanza katika mikoa saba ya Dar es Salaam, Arusha,
Dodoma, Mbeya, Kilimanjaro, Mwanza na Tanga na mingine itafuata kwa mujibu wa
ratiba itakayopangwa.
Ndugu
Wananchi;
Teknolojia ya dijitali katika mfumo wa
mawasiliano hufanya picha za televisheni kuwa nzuri na hazina chenga chenga. Mawasiliano ya simu yatakuwa mazuri
zaidi. Vile vile, itakuwa rahisi kupata
huduma za televisheni kwenye simu za mkononi na huduma ya intaneti kwenye
televisheni.
Ndugu
Wananchi;
Ili kuweza kutumia teknolojia hii, kila
televisheni inatakiwa iwe na kifaa kiitwacho king’amuzi. Vifaa hivi vipo kwa wingi
madukani na wengine tayari wanavyo. Naomba niwatoe hofu kwamba kwa kuingia
katika mfumo huu siyo lazima kununua televisheni mpya. Televisheni yo yote yenye
vitundu vitatu vya rangi za njano, nyeupe na nyekundu itaweza kufanya kazi
kwenye mfumo wa dijitali. Hata wale ambao hawana televisheni za namna hiyo wanaweza
kununua kifaa cha kuunganishia king’amuzi na mambo yakawa mazuri.
Uhusiano
wa Kimataifa
Ndugu
wananchi;
Katika mwaka 2012, uhusiano wetu na
washirika wetu wa maendeleo ulikuwa mzuri na uliendelea kuimarika. Wote wanaridhika na kusifu kazi nzuri
inayofanywa na Serikali yetu na ndiyo maana wanaendelea kushirikiana nasi na kutoa
misaada ya maendeleo. Aidha, wameonesha
nia thabiti ya kuendelea kushirikiana nasi na kutusaidia katika harakati zetu
za kujiletea maendeleo.
Napenda kutumia nafasi hii kwa niaba
yenu nyote kutoa shukrani za dhati kwa washirika wetu wa maendeleo kwa mchango
mkubwa wanaoendelea kutoa kwa maendeleo ya nchi yetu. Nawahakikishia kuwa tunathamini sana
ushirikiano wao na misaada yao na tutafanya kila tuwezalo kudumisha ushirikiano
baina yetu.
Mkutano
wa Smart Parntership
Ndugu
Wananchi;
Mwaka huu nchi yetu ilipata bahati ya
kuwa mwenyeji wa mikutano mikubwa ya kikanda na kimataifa. Mikutano hiyo ni pamoja na Mkutano Mkuu wa
Shirika la Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA), Mkutano wa Mwaka wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB), Mkutano Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Chanjo
(GAVI) na Mkutano wa Wakuu wa Nchi za
SADC.
Bahati nzuri mwaka 2013 Tanzania
itakuwa mwenyeji wa mikutano mingine ukiwemo ule wa Global 2013 Smart Partnership Dialogue utakaofanyika Dar es Salaam
kuanzia tarehe 24 – 28 Mei, 2013. Huu ni
mkutano unaohusisha nchi nyingi duniani na kutoka takriban mabara yote. Mkutano huu hukutanisha na kushirikisha viongozi
wa Serikali wakiwemo Wakuu wa Nchi na Serikali, viongozi wa sekta binafsi wakiwemo
wa makampuni makubwa ya kimataifa, wasomi na wawakilishi wa asasi za kiraia na watu
binafsi.
Kwa kawaida katika mkutano kama huu
huwepo agenda maalum, aghalabu kuhusu masuala ya uchumi, biashara na maendeleo. Mkutano
wa mwaka 2013 utazungumzia “Matumizi ya
Sayansi na Teknolojia kwa Ajili ya Maendeleo ya Afrika” (Leveraging Science
and Technology for Africa’s Development).
Kwa kweli ni kipaumbele muafaka kabisa, ndiyo maana na sisi tumefarijika
kuukaribisha.
Ndugu
Wananchi;
Kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa kama huu
wa watu zaidi ya 500 mashuhuri, ni
heshima kubwa kwa nchi yetu. Ni nafasi nzuri
ya kuitangaza Tanzania na fursa zake za uwekezaji, biashara na utalii. Pia, ni
nafasi nzuri kwa wafanyabiashara wetu kutangaza shughuli zao na fursa za
biashara na uwekezaji wanazotaka kushirikisha wafanyabiashara wa nje. Naomba tuitumie vyema fursa hiyo adimu kwa
manufaa ya taifa na ya waanyabiashara wetu.
Tuwaonyeshe wageni wetu upendo na
ukarimu kama ilivyo sifa yetu Watanzania ili waondoke na kumbukumbu nzuri za
nchi yetu na watamani kurudi tena kutembea au kuwekeza.
Hitimisho
Ndugu
wananchi;
Tunatarajia kuwa mwaka 2013 utakuwa
mwaka wa mafanikio makubwa zaidi katika nyanja zote kuzidi mwaka 2012. Mambo yaliyokwama mwaka 2012 yatakwamuliwa. Ajira zitaongezeka kwa uwekezaji vitega
uchumi kuongezeka na kuwajengea uwezo wajasiriamali wazalendo, ili waweze kujiajiri
wenyewe na kuajiri wengine. Kwa ajili
hiyo, Mifuko ya kusaidia wajasiriamali wadogo, wanawake na vijana itafufuliwa
na kutengewa fedha nyingi katika bajeti ya Serikali.
Mwaka 2013 ni mwaka wa matumaini, hivyo kila
mmoja wetu anatakiwa kujituma na kutimiza wajibu wake. Maisha bora yatakuja kwa kila mmoja wetu kutimiza
wajibu wake ipasavyo. Kama kila mtu atafanya
kazi kwa bidii na maarifa, na, kama kila mmoja wetu atajivunia matokeo ya kazi
yake na siyo uhodari wa maneno yake ya uchambuzi wa hali. Kila mtu achukie uvivu na tabia ya kulalamika
pasipo kufanya kazi.
Ndugu
Wananchi;
Mimi na wenzangu Serikalini
tunawaahidi ushirikiano wa hali ya juu na kwamba tutawatumikia kwa moyo wetu
wote, kwa nguvu zetu zote na kwa maarifa yetu yote. Tunataka kukidhi matarajio na imani ya
wananchi kwa Serikali yao. Tutaendelea kuimarisha utendaji kazi Serikalini na
kuhimiza uwajibikaji katika ngazi zote za uongozi. Tutaendeleza mapambano dhidi
ya rushwa bila ajizi na watumishi wasio waaminifu, wazembe, wabadhirifu wa mali
ya umma watawajibishwa ipasavyo. Wananchi pia wanao wajibu wa kuwa raia wema na
wazalendo wa kweli kwa nchi yao. Kila mmoja wetu ajiulize ataifanyia nini jamii
yake na nchi yake badala ya kuuliza itamfanyia nini.
Ndugu
zangu,Watanzania Wenzangu;
Nawatakieni nyote heri na fanaka tele
katika mwaka mpya wa 2013. Tusherehekee pamoja kwa amani na utulivu.
Mungu
Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment