DAR ES SALAAM, Tanzania.
UMOJA
wa Wamiliki wa Mabasi Tanzania(TABOA) umeahidi ‘kuwachongea’ baadhi ya wamiliki
wa mabasi katika Ofisi za Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA),
kwa kukaidi taratibu za uendeshaji wa mabasi yao.
Aidha
umesikitishwa na ajali za mabasi zilizotokea juzi huku uliomba Jeshi la Polisi
kikosi cha Usalama Barabarani kuchunguza kwa makini juu ya tukio hilo kisha
kuwachukulia hatua za kisheria waliosababisha ajali hiyo.
Akizungumza
na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam leo, Katibu Mkuu wa Taboa, Enea
Mrutu, amesema kuwa pamoja na Serikali kuonyesha nia ya kuondoa matatizo yaliyopo
katika sekta ya usafiri, wapo baadhi ya wamiliki wenye nia ya kuhujumu mikakati
iliyopo.
Aliongeza kuwa wapo baadhi ya wamiliki wa mabasi wamekuwa wakienda kinyume na
utaratibu huo kwa matakwa yao binafsi jambo alilosema kuwa linakiuka maagizo
yaliyowekwa.
“Tunaishukuru
Serikali kwa kuwa sasa ipo karibu na sisi katika hatua mbalimbali, ushirikiano
huu umeonyesha wazi kuwa mbeleni utakuja kuzaa matunda ambayo dalili zake hivi
sasa tumeziona isipokuwa wapo baadhi ya wenzetu wanakwenda kinyume na yale
tunayokubaliana” alisema Mrutu.
Mrutu
alisema pamoja na mikakati mizuri iliyofanywa na Serikali kwa kuweka
utaratibu wa ratiba za mabasi, baadhi ya wamiliki wakekuwa wakiendesha
safari kwa utaratibu wao na hivyo kuleta hofu ya kutokea kwa ajali alizodai
kuwa nyingi zinasababishwa na uzembe pamoja na kutofuata ratiba.
“Juzi
tulikuwa na kikao na Kamati ya Bunge, moja ya mambo tuliyokubaliana ni kufuata
ushauri tunaokubalaiana na Serikali, huu ndio ushirikiano ambao kama kweli tuna
nia ya kuendeleza sekta ya usafiri nchini, hatuna budi kuufuata” alisema Mrutu.
Mrutu
alisema kutokana na uwepo wenzao wanaokwenda kinyume na makubaliano hayo,
wameamua kuunda kamati itakayokuwa ikifanya kazi katika njia kuu tano za mabasi
kutokea Dar es salaam, kwa lengo la kuwafuatilia wale wanaokwenda kinyume na
utaratibu huo na ili baadae wakafikishe matatizo yao Sumatra pamoja na Polisi
makao makuu ya Usalama barabarani.
Alizitaja
njia nne zitakazofuatiliwa na kamati hiyo ya watu watano kuwa ni pamoja
barabara ya Dar es salaam kwenda Arusha, Dar es salaam kwenda Mwanza, Dar es
salaam kwenda Mbeya, pamoja na Dar es salaam kwenda Mikoa ya Kusini.
Akizungumzia tukio la ajali iliyotokea juzi na
kupoteza maisha ya watu saba, Mrutu alisema kinachoonekana ni kuwa ajali hiyo
ilisababishwa na uzembe wa madereva, hivyo ni vyema jeshi la Polisi likafanya
uchunguzi wake wa kina na kuwachukulia hatua kali wahusika.
No comments:
Post a Comment