MADRID,
Hispania
Nusu fainali ya pili ya Kombe la Mfalme kati ya Barcelona
na Madrid inatarajiwa kupigwa Nou Camp hapo Februari 27, katika mechi
itakayoamua timu ya kutinga fainali baina ya miamba hiyo
MRENO Jose Mourinho bado yu kikaangoni klabuni Santiago
Bernabeu, licha ya kukwepa kichapo na kuambulia sare ya bao 1-1 na FC Barcelona
kwenye dimba la nyumbani katika mechi ya mahasimu ‘El Clasico’ juzi usiku.
Kocha huyo wa Real Madrid alikuwa hatarini kuangukia pua nyumbani
katika nusu fainali hiyo ya kwanza ya Kombe la Mfalme ‘Copa del Rey’ dhidi ya
mahasimu wao na vinara wa La Liga Barca.
Cesc Fabregas (pichani kulia) aliifungia Barca bao lake
dakika tano kabla ya tamati ya kipindi
cha kwanza, kabla ya yoso Raphael Varane, 19, kufunga kwa mara ya kwanza katika
‘El Clasico’ na kuisawazishia Madrid
dakika saba kabla ya filimbi ya mwisho.
Mourinho kocha wa zamani wa Chelsea
na Inter Milan, siku zake zinahesabika klabuni Bernabeu,
akisotea pengo la pointi 15 nyuma ya mahasimu wake hao Barcelona, katika jaribio la kutetea ubingwa
wake wa La Liga.
Tumaini pekee la kuambulia ubingwa msimu huu ni michuano ya
Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambako ataivaa Manchester
United katika mechi mbili za nyumbani na ugenini za hatua ya 16 bora.
Mourinho na kikosi chake watawaalika Man United chini ya Sir
Alex Ferguson hapo Jumatano ya Februari 13, kabla ya kurudiana kwenye nyasi za
Uwanja wa Old Trafford Jumanne ya Machi 5.
Nusu fainali ya pili ya Kombe la Mfalme kati ya Barcelona na Madrid
inatarajiwa kupigwa Nou Camp hapo Februari 27, katika mechi itakayoamua timu ya
kutinga fainali baina ya miamba hiyo.
……BBC/The Sun……
No comments:
Post a Comment