Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
Philipo Mulugo akizindua tovuti ya www.shuledirect.co.tz
itakayosaidia kuboresha utoaji wa huduma za elimu hapa nchini. Uzinduzi huo
ulifanyika jijini Dar es Salaam. (Picha na Habari Mseto Blog)
DAR ES SALAAM, Tanzania
NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo,
amerudisha adhabu ya viboko kwa wanafunzi wa shule zote ili kurudisha nidhamu
iliyotoweka kwa wanafunzi.
Mbali na adhabu hiyo kurejea Mulugo pia amewataka walimu
kuwanyang’anya simu wanafunzi watakaokutwa nazo kwani zinachangia kumomonyoa
kiwango cha elimu kwa utumiaji wa facebook.
Akizungumza jijini Dar es salaam wakati wa utambulisho wa mfumo
wa www.shuledirect.co.tz utakaosaidia kuboresha utoaji
wa huduma za elimu nchini, Mulugo alisema kuwa ni jukumu la kila mwanajamii
kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu
nchini.
Mulugo alisema kuwa japo karne hii ni sayansi, teknolojia na
utandawazi ni vyema kuwahimiza wanafunzi kutumia mitandao katika kutafuta
maarifa na kusoma tafiti mbalimbali kwa kuzingatia mila na desturi.
Pia alisema kuwa mfumo huo utasaidia wanafunzi, walimu na jamii
nzima katika kuongeza ufahamu wenye tija katika kuchochoea maendeleo yataaluma.
Naye Mwanzilishi wa program hiyo, Faraja Nyalandu, alisema kuwa
mpango huo ili malengo ya elimu bora yafikiwe ni muhimu kila mtu atimize wajibu
wake.
Nyalandu alisema kuwa Mpango huo ni mfumo wa kuweza kujisomea
katika mtandao kwaajili ya wanafunzi wa sekondari.
Alisema kuwa malengo ya mfumo huo ni kumuwezesha mwanafunzi
kujisomea, kufanya mazoezi, kufahamu mtiririko wa anachopaswa kujifunza kupitia
mtaala wa kuweza kushiriki katika majadiliano ya kiakademia.
No comments:
Post a Comment