Ras Inno Nganyagwa akionesha tuzo ya Kili Music.
Ras Inno akifanya vitu vyake jukwaani katika moja ya matamasha yake.
Na Francis
Dande
HATIMAYE bendi ya nguli wa muziki wa reggae nchini,
Ras Inno Nganyagwa imekamilika na anatarajia kuizindua rasmi mwezi ujao jijini
Dar es Salaam.
Ras Inno ambaye ni mshindi wa tuzo nne za
mwanamuziki bora wa reggae Tanzania, amesema bendi yake hiyo ina wanamuziki 11
na itazinduliwa katika hafla maalumu katika ukumbi utakaotangazwa hapo baadaye.
Amasema nia ya kuanzisha bendi hiyo ni kuwa na
ufanisi bora zaidi wa kufanya kazi zake za muziki, kwani bendi ya kudumu na
wanamuziki wa kudumu hujenga ‘patern’ ambayo ni sawa na wachezaji waliozoeana
uwanjani.
“Hiyo hulinda ladha ya nyimbo husika kutobadilika
kila show, pia uhakika wa kufanya kazi njema nje ya nchi. Lakini pia kuwa na
bendi huhakikisha upatikanaji wa tija ya kudumu, tofauti na ukiwa ‘solo’ tu bila
jina la bendi kazi huja kwa misimu kutokana na mazoea ya hapa kwetu Bongo,”
amesema.
Amesema bandi hiyo ni mojawapo ya miradi iliyo chini
ya usimamizi wa taasisi yake mahsusi ya kuupromoti muziki wa reggae, kwa
ushirikiano na wadau wengine miongoni wa mitindo mingine kwa kuzingatia weledi.
“Taasisi inaitwa Reggae Production House ambayo
itahakikisha uzalishwaji wa vipaji vipya vya vijana wanaotaka kuingia kwenye
reggae, kwa kufuata njia sahihi itakayowajenga kuwa wanamuziki bora wa reggae
nchini watakaoweza kufanya kazi kimataifa.
“Dhima nzima ni kuufufua muziki wa reggae hapa
nchini si kwa kuwa umekufa, la hasha, ila kuna mazingira yanayoufanya muziki
huu uonekane kama haupo, lakini mahitaji yapo na mashabiki wana hamu kubwa nao.”
Aidha ameongeza kusema kwamba, ukimya wake wa muda
mrefu una sababu kadhaa zikiwemo za kibinafsi kimaisha, lakini muda aliokuwa
nje ya ulingo, ameyasoma vyema mazingira yanayoukabili mtindo wa reggae hivyo
naamini ana dozi ya kuutibu.
“Ninayodhamiria kuyafanya kupitia taasisi yangu na vitengo
vyake ikiwemo bendi, havijapata kuonekana kabla kwenye tasnia ya reggae hapa
nchini. Hivyo basi naamini mwanzo huu wa mapinduzi, utaungwa mkono na wadau wote
wenye mapenzi mema.”
No comments:
Post a Comment