HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 27, 2013

MIZENGO PINDA NA KISA CHA MTU ALIYEKATAA USHAURI MWEMA WA HASIMU WAKE

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda

v     Ni jinsi alivyokataa hoja ya Freeman Mbowe akidhani angeupa sifa Upinzani
v     Alisahau falsafa ya: Ukikutana na Simba usimkimbie, mtazame usoni tu hatokufanya lolote!

Na Bryceson Mathias

Kabla sijaanza mjadal huu, niulize swali hili; Kama mfumo wa vyama vingi uliridhiwa, kwa nini sasa vyama vya upinzani vinapigwa vita na kutafutiwa mbinu ya kuviua kwa hila?

Ni vyema kujua ukiamua kuoa, ufahamu lazima utakuwa na watoto wanaotaka kula, kuvaa na mahala pa kulala, kusoma na mahitaji mengine ya msingi.

Familia moja katika kijiji fulani, ilimpoteza ndugu yao wa kutegemewa baada ya kuliwa na Simba, kutokana na kupuuza ushauri wa hasimu wake aliyemshauri asiende aendako maana kuna simba mkali. Akaenda tu, na hatimaye akararuliwa na Simba akafa!

Wahenga walisema, ‘Ukisafiri mtoto mwachie mchawi’, atamlea, atakutunzia, na atamlisha chakula kizuri, na mahala pa kulala ili kuhakikisha anakuwa salama kiafya kwa hofu kwamba, akiugua akafa! Atatuhumia amemroga.

Katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maji iliyowasilishwa na Waziri wake Prof. Jumanne Maghembe hivi karibuni, mbali ya wabunge kuikwamisha, Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati wa kipindi cha maswali na majibu ya papo kwa hapo, hakukubali ushauri wa Freeman Mbowe aliyetaka hoja hiyo iondolewe ili ikafanyiwe marekebisho.

Kama ilivyo ada viongozi wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujibu hoja kwa kuangalia imeletwa na mbunge wa upande gani, Pinda alikiri kuwa wabunge wengi wameonesha kutoridhishwa na bajeti hiyo, lakini si busara kuiondoa na kusema tatizo uhaba wa fedha.

Licha ya Pinda kukataa hoja ya Mbowe kwa kudhani angeipa sifa kambi ya upinzani, mwongozo wa Mwigulu Nchemba uliokuwa na mwelekeo sawa na muuliza swali, ulikubaliwa na Spika, hivyo kuamua kuahirisha hoja hiyo.

Jambo hilo limenikumbusha, mtu aliyeliwa na Simba kwa kupuuza ushauri wa hasimu (adui) wake, akiamini kuwa hawezi kumshauri mema na kama atafuata ushauri wake ‘atampa kusema’.

Kama Pinda aliona ama kusikia wabunge wengi wanaonesha kutoridhishwa na bajeti hiyo, uamuzi huo ulikuwa ufikiwe mapema kwa Waziri Mkuu kukubali ushauri wa Mbowe wakati akijibu swali lake Bungeni, aliyetaka hoja hiyo iondolewe ili ikafanyiwe marekebisho, jambo ambalo lingeokoa muda na gharama.

Yesu katika Yohana 10 mstari wa 37 hadi 38 alisema: “Kama sizitendi kazi za Baba yangu, msiniamini, lakini nikizitenda, ijapokuwa hamniamini mimi, ziaminini zile kazi mpate kujua na kufahamu ya kuwa Baba yu ndani yangu, nami ni ndani ya Baba. Wakatafuta tena kumkamata, lakini akatoka mikononi mwao.”

Hivyo tabia ya serikali na chama tawala kupuuza ushauri wa wabunge wa upinzani, siafikiani nayo kabisa, maana ni uzembe. Ipo siku adui anaweza kuingia mpakani, wakaelezea jambo lolote la hatari kwa Taifa, mfano; kuna mtu anaweka sumu kwenye maji kama baadhi ya wawekezaji wanavyopiga sumu mazao ya watu tunapuuza, watu watakwisha.

Ni ni ukweli usiopingika kuwa, upinzani pia wamo wabunge waliopevuka kihoja na kielimu zaidi kuliko wale wa chama tawala, kwa nini tusiwakubali kwa kizuri wanachoshauri?

Mtalaam mmoja wa wanyama alisema hivi; Ukikutana na Simba usigeuke ukaanza kumkimbia, bali mtazame jkwa kumkazia usoni ataona aibu na hatokufanya chochote! Badala yake ataondoka na kukuacha bila kukufanya chochote.

Lakini ukimpa kisogo, unamruhusu ujuzi wake wa porini wa kupata wanyama kwa kutumia makucha ili apata kitoleweo na kuonesha umahiri wake wa kuwasaka na kuwanasa wanyama mwituni.

Rai yangu kwa serikali na CCM; Ijue wananchi wanatambua kuwa kuwepo kwa vyama vya upinzani nchini, ndiko ambako kumesaidia maisha yao yasiwe magumu zaidi ya mahali yalipo.

Ukifanya mahojiano na Watanzania kadhaa, wanakiri wazi kwamba kama vyama vya upinzani visingekuwepo, maisha ya Mtanzania yangekuwa duni na hali ya chini mno, kifupi hali ingekuwa mbaya, hivyo ni vigumu kuwasukuma kuamini kuwa wapinzani hawana mchango katika kuboresha maisha yao!

Maswali, maoni ama ushauri kwa mwandishi
Barua pepe: nyeregete@yahoo.co.uk
Simu: 0715933308

No comments:

Post a Comment

Pages