Na Mwandishi Wetu
Mwanamitindo wa kimataifa wa Tanzania, Flaviana Matata leo atashiriki katika misa maalum ya kuwakumbuka watanzania waliopoteza maisha katika ajali ya MV Bukoba mwaka 1996.
Misa hiyo itafanyika kwenye eneo la makabuli ya kumbukumbu ya MV Bukoba ambapo Flaviana alipoteza mama yake mzazi na kaka yake katika ajali hiyo.
Mwaka jana, mwanamitindo huyu kupitia shirika lake la Flaviana Matata Foundation alitoa msaada wa maboya yaani vyombo vya kuokoa maisha majini (life vests) 500 kwa mawakala wa meli ya serikali yaani Marine Services Ltd ikiwa ni nja moja ya kujaribu kusaidia usalama majini.
Mkurugenzi wa kampuni ya Compass Communications, Maria Sarungi alisema kuwa mbali ya kushiriki katika misa hiyo, pia mwana mitindo huyo atafanya mazungumzo na wadau mbali mbali jinsi ya kuendeleza juhudi za kuimarisha usalama majini.
Flaviana alisema kuwa juhudi zake kubwa kwa hivi sasa ni kuhakikisha kuwa ajali za vyombo vya kwenye maji zinaepukika na ndiyo maana anapigana huku na kule katika sakata hilo.
Alisema kuwa lengo lake kubwa ni kuona vyombo vya kuokolea katika kila meli vinapatikana na hasa kwa kutafuta misaada kwa wadau mbali mbali.
“Suala la usalama majini bado haujatiliwa mkazo vya kutosha na jamii pamoja na serikali” alieleza mwanamitindo huyu. “Muda umefika kwa wahusika wote kushirikiana kwa pamoja kuzungumzia na kukabiliana na changamoto hii” alisema Matata.
No comments:
Post a Comment