Na Mwandishi Wetu
Mtu mmoja amefariki dunia kufuatia mlipuko wa bomu uliotokea katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Parokia mpya ya Olasiti Mkoani Arusha na kusababisha kifo cha mtu mmoja na wengine 60 kujeruhiwa na 42 kati yao wamejeruhiwa vibaya.
Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal amelaani tukio hilo na kusema kuwa Serikali imesikitishwa na tukio hilo na kuvitaka vyombo vya sheria kuhakikisha waliohusika wanakamatwa mara moja.
'Watu hawa wasakwe na kukamatwa mara moja na kufikishwa katika vyombo vya sheria' amesema Makamu wa Rais Dk. Mohamed Gharib Bilal na kuongeza kuwa tukio hilo linaweza kusababisha matakaba na uvunjifu wa amani.
Akizungumza kutoka mjini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi amesema kuwa uchunguzi umeaanza mara moja na watu sita wanashikiliwa na Polisi kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na tukio hilo.
'Tunawashikilia watu sita kwa ajili ya mahijiano kuhusiana na tukio hilo na nimetoa maagizo kwa vikosi vya ulinzi na usalama kuwasaka popote walipo watu waliohusika na tukio hilo'.
Uchunguzi wa tukio hilo umeanza mara moja na katika kuhakikisha waliohusika na tukio hilo wanapatikana mara moja Jeshi la Wanananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kuwasaka na kuwatia mbaroni wahusika wote ambapo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Silima pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi Inspekta Generali wa Polisi (IGP), Said Mwema wapo jijini Arusha.
Mlipuko wa bomu hilo ulitokea majira ya saa 5 leo asubuhi katika uzinduzi wa Parokia mpya ya Olasiti, Jijini Arusha wakati Askofu Mkuu Josephat Louis Lebulu na Balozi wa Baba Mtakatifu nchini, Askofu Mkuu Francisco Montecillo Padilla wakiwa wamejiandaa kuanza maadhimisho ya misa ya kutabaruku kanisa hilo kwa kuwabariki waumini hao tayari kwa ibada.
Akiahirisha Ibada hiyo Vicar General wa Jimbo Katoliki la Arusha Padre Simon Tengesi aliwataka wakristo wote kuondoka eneo hilo na uzinduzi huo umeahirishwa hadi pale itakapotangazwa tena, na watu wameondoka eneo hilo ili kuruhusu vyomvyo vya ulinzi na usalama viweze kuanza uchunguzi.
Chanzo chetu cha habari kinasema eneo lilipolipuka bomu kuna damu nyingi na watu wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas amewataka wananchi kutoa ushirikiano kuweza kuwabaini waliorusha na/au kutega bomu kwenye eneo hilo la Ibada.
No comments:
Post a Comment