Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Wamiliki wa Mabasi
Tanzania (TABOA), kinatarajia kukutana na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam
pamoja na Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), leo ili kujadili
tatizo la wapiga debe katika Kituo kikuu cha Mabasi cha ubungo.
Akizungumza na waandishi wa
habari mwishoni mwa waiki jijini Dar es Salaam, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya
Taboa Rajab Kassim, alisema tatizo la wapigadebe kituoni hapo ni asilimia
themanini, bado kuna haja ya kukutana na wadau hao ili kulitafutia ufumbuzi wa
kudumu si wazima moto.
Alisema wanatarajia
majadiliano hayo yatasaidia kuleta suluhu katika kampeni za kuwaondoa wapi gadebe
kituoni hapo, kufuatia operesheni ya kwanza iliyofanywa na askari wa ulinzi
shirikishi wa chama hicho kwa wakishirikiana na askari wa Jiji, kuleta mafanikio hayo.
“Operesheni hiyo ya wiki
mbili hadi sasa, kwa kiasi kikubwa imefanikiwa kuwaondoa wapigadebe hao ambao
kwa kipindi kirefu walikuwa kero kwa abiria, mkutano wetu wa leo na Mkurugenzi
pamoja na Sumatra utatusaidia kufikia malengo tulioyakusudia” alisisitiza
Kassim.
Alisema kutokana na kero ya
wapigadebe hao iliyokuwa kama ‘mwiba mchungu’ kwa uongozi wa Jiji la Dar es
salaam, Taboa iliamua kuweka mkakati maalumu ulioshirikisha Polisi, Halmashauri
ya Jiji na askari wa ulinzi shirikishi waliopo chini ya Chama hicho.
“Tumeliona jambo hili ndiyo
jukumu letu kubwa katika mipango yetu ya kuboresha huduma za usafiri, ikumbukwe
ni kipindi kirefu kimepita tangua tatizo la wapigadebe hawa lianze
kulalamikiwa, mikakati ni kuwaondoa kabisa wapigadebe hao katika eneo la kituo”
alisema Kassim.
Aidha Kassim alisema
kuondolewa kwa wapigadebe hao kwa kiasi kikubwa kumeondoa adha kwa abiria
waliokuwa wakifika hapo kwa ajili ya kupatiwa huduma ya tiketi ambao mara
nyingi walijikutwa wakiibiwa mali zao kutokana na kuvutwavutwa pasipo na ridhaa
yao.
“Tunawashauri wamiliki wa
mabasi kuachana na wapigadebe hawa na kujiandaa na utaratibu mpya wa ukataji wa
tiketi kwa njia ya mtandao maarufu kama ‘E-Bus Ticketing’ unaotarajiwa kuanza
hivi karibuni mara baada ya marekebisho katika mtandao yatakapokuwa
yamekamilika” aliongeza Kassim.
No comments:
Post a Comment