‘Siku ya Kufa Nyani Miti yote huteleza’
Na Bryceson Mathias
KILA siku najiuliza Swali, hivi Daudi Mwangosi Mungu amuweke Pema Peponi, angekuwa Mdogo wake na Waziri wa Mambo ya Ndani Dk. Emmanuel Nchimbi,angetaka RPC Iringa Michael Kamuhanda awepo kazini?
Kama wanafunzi watatu, Atu Geofrey, Fidelisi Michael na Barnabas Venanti, waliokufa wakisikitikia Matokeo ya Mabovu ya Mtihani wa Kidato cha Nne 2012, wangekuwa watoto wa Viongozi wa Juu wa Chama Tawala, Wangesema Waziri wa Elimu Dk. Shukuru Kawambwa na Timu yake waendelee Kuula?
Iwapo vifo vya Wachungaji, Mapadri, Ma-Shekhe na Wananchi wanaouawa Kinyama, wakiwapo watu wanakufa mikononi mwa Polisi, ni Ndugu zao na Wabunge akiwemo Spika Anne Makinda, Naibu wake Job Ndugai, Wenyeviti na Wabunge, Waziri Dk.Nchimbi na IGP Said Mwema, wangebaki ofisini mwao?
Ni kweli waswahili walisema, Fumbo Mfumbie Mjinga lakini Mwerevu ataling’amua.ni ukweli usiopingika kama ingekuwa hivyo, ingekuwa patashika Nguo kuchanika, zaidi ya Jeuri aliyofanyiwa Jeryy Muro, Godbless Lema na wapenda Haki wengine nilioacha kuwataja kwa sababu ya Nafasi.
Laiti Wahanga hao wangekuwa Ndugu zao, Wabunge wasingepitisha Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani mpaka Dk.Nchimbi, IGP Mwema naRPC Kamuhanda wamejiuzulu kwa Vifo vya watanzania wasio na hatia wanaofia mikononi mwa Polisi.
Nataka tuambizane kweli bila kutafuna maneno, Hata Mbuyu ulianza kama Mchicha, hivyo Kawambwa angekuwa ameegama kwenye Mchicha, akatangaza Matokeo ya Mtihani yeye, badala ya Joyce Ndalichako, na akatangaza kurekebisha matokeo hayo! Kama hajaegema kwenye Mbuyu, tungemsahau.
Nikifika hapo ndipo ninaposema, tunaishi kwenye nchi ambayo baadhi ya watetezi wa watu wanaumwa, Kisiasa, Kiuchumi, Kiutamaduni na kutokujua Haki zao, na kama wanajua, basi wamegandamizwa na Jiwe la Wayahudi lililomgandamiza Yesu, ingawa yeye alilisukuma akatoka, sisi tumefeli.
Katika hilo ninaunga Mkono ni kweli Taifa linaumwa. Linaumwa Rushwa isiyosemekana, Ufisadi wa kutisha, Elimu ya Danganya toto, na Udini uliopandikizwa kwa makusudi ili watanzania wabaki wakihangaika na Maafa, wao wabebe Rasilimali na kufiche Uswizi!!
Je Kero, Adha na Masahibu hayo,hazitoshi tuseme yatosha? Kwa nini tusiwe Yoel 2:25, Turudishiwe hiyo miaka iliyoliwa na Nzige, na Parare, na Madumadu, na Tunutu, Jeshi letu kubwa lililotumwa kati yetu.mwalimu Nyerere akiwa Kipenzi cha Uhai wa watanzania kuliko hawa wanotuua ovyo?
Dk. Nchimbi, mwema, Kamuhanda, Mwigulu Nchemba, Wabunge, Mawaziri,na Ma-Rais wote Tanzania na Z’bar, Viongozi wa Dini zote na Wanaharakati. Msiba ni mzuri ukiwa kwa Jirani,hapo utasemaNgoja nile nitakwenda, Ngoja Nioge, Nipige Mswaki. Lakini Msiba ukiwa kwko!
Ndiyo maana, Watu huwa hawatani Nywele, Hawaogi, Hawalali Kitandani, Hawapigi Mswaki, Hawafui Nguo, Hawavai Viatu, mtu anaweza kwenda Choo asikumbuke kuvaa viatu;kwa sababu Msiba uko kwake. Hivyo ni Sala yangu wabunge Mbadilike,ile sasa nitawauliza; wanaosemaNdiyo waseme Ndiyo.
Na bungeni mnakosemasasa nitawahoji, wanaosema siyo waseme Siyo! Huo mchezo mnaotudanganya huyo mwanzilishi wa Kauli hiyo, hakufanya kama mnavyofanya Utani. Yeye Mungu alisema, Siyo ya Mungu iwe Siyo,na Ndiyo ya Mungu iwe Ndiyo ya Kweli.
Bungeni Mnasema Siyo! Kumbe Hela mmeweka ziko Uswizi,Watoto wenu wanasoma Ulaya, matokeo mnabadili ili wenu waje, wawatawale wetu, Hapana. Tungeni Sheria wasome na watibiwe humuhumu, ili wote tufe kwa kukosa madawa. Kama hamuwezi, basi tendeni Hakikwa wote na si kwa wachache. Ninyi tuu; Hapana.
nyeregete@yahoo.co.uk 0715933308
No comments:
Post a Comment