HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 07, 2013

Je; Sitta Aokolewe kwenye Kisima cha Matope? Ndiyoooo!!

Samuel Sitta
John Magufuli
Na Bryceson Mathias

HIVI karibuni, WAZIRI wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mbunge wa Urambo, Samuel Sitta, alimuokoe Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, dhidi ya Makombora ya Tundu Lissu (CHADEMA) asiondolewa Shilingi ya Mshahara wa Waziri huyo bungeni.

Sitta ililazimika kufanya hivyo kutokana na kile kilichodaiwa ni Majibu Goigoi, Mepesi yaliyotafsiriwa ya kuokoteza ya Dk. Nchimbi, hivyo kuibua mvutano mkali wa uelewa baina ya Mbunge wa Singida Mashariki Lisu, na Dk. Nchimbi aliyeelemewa.

Kilichomponza Nchimbi na kumwinua Lissu kilikuwa ni kutoa hoja ya kuondoa shilingi akisema Waziri huyo ametoa maelezo ya mzaha wakati tume aliyoiunda yeye na ile ya Haki za Binadamu iliyoundwa na Rais, kwa nini wameshindwa kuzifanyia kazi?.

Hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge wengi wa upinzani   walioanza kuichangia wakidai Polisi linafanya kazi kwa maelekezo ya wanasiasa, hata kufikia hatua ya kushindwa kuwachukulia hatua vigogo wa CCM kwa amri za wakuu wa Mikoa na wilaya.

Kuokolewa Dk. Nchimbi na Sitta, kunafananishwa na kuokolewa kwa Yeremia kwenye Shimo la Kisima cha Matope, ambapo Ebedmeleki M-Ethiopia, alitumia Matambara na Kamba alivyochukua Chumbani kwa Mfalme akamtupia aweke Kwapani, avutwa na kuokolewa na Kifo, kilichopangwa na adui zake Yeremia (38:10-13).

Bila Kigugumizi Watanzania tunasema, ukweli Sitta aliyeongoza Bunge la 10, alikuwa Spika pekee mwenye Viwango aliyethubutu kutumia Kiti chake Kukemea na Kukataa Rushwa na Ufisadi unaofanywa hata na baadhi ya Wabunge unaowahusisha hata baadhi ya watawala, na Bunge lilikuwa la Heshima.

Ukweli huo, ndio uliopelekea afanyiwe kile kilichodaiwa   kumpindua asiwe Spika wa Bunge la 11, ambalo sasa kila kukicha tunaona Maajabu yakiwemo matusi yasiyotamkika hata na watoto wadogo kiasi cha Bunge kuwa kama limelaaniwa.

Spika, Anne Makinda, akihitimisha kupitishwa kwa Bajeti ya Wizara ya Elimu, Mafunzo na Ufundi Juni 5, mwaka huu alikiri Wabunge wamepungukiwa, maana wanajadili mtu badala Hoja.

Siku chache baada ya Waziri wa Afrika Mashariki Samuel Sitta kumhusisha Dk. John Magufuli (pichani) na kundi la Urais la 2015, Waziri huyo wa Ujenzi, aliibuka na kupinga kauli hiyo, akisisitiza hafikirii kuwania nafasi hiyo.

Waziri Sitta, alinukuliwa na Vyombo vya habari kwamba, Wakati ukifika; Yeye na rafiki zake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Ujenzi, Dk Magufuli na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, watachagua nani awanie urais katika Uchaguzi huo.

Sitta anadaiwa kusema hayo kwenye Kongamano la Mawasiliano katika Nyanja za Digitali la Wanafunzi wa Idara ya Uhusiano na Masoko, Chuo Kikuu cha St. Augustine (SAUT), Mwanza.

Kabla ya hapo alikuwa amewataja rafiki zake hao wakati wa hafla ya kuchangia Kanisa Katoliki, Josephine Bakita, Parokia ya Igoma, Mwanza, katika moja ya Ibada zilizofanyika Jumapili iliyopita.

Alisema, hatagombea tena ubunge 2015, baada ya kuwa katika ulingo wa siasa kwa miaka 35 na badala yake ataangalia namna nyingine ya kuwatumikia wananchi huku akigusia mchakato wa kuwania urais ambao alieleza anamwachia Mungu.

“Kwa ubunge nimekwishawaeleza inatosha, sitagombea tena kwani miaka 35 inatosha. Lakini hatima yangu ni nini siwezi kujua;

Lakini nina afya nzuri na ni mmoja wa wanasiasa wakongwe, wenye afya nzuri, mnaona ninavyopendeza... kwa urais namwachia Mungu tutaona,” alisema Sitta.

Akipinga kuhusishwa na Mchakato huo, Magufuli alisema haelewi msingi wa kauli ya Waziri Sitta, kwani hajui kitu katika mtandao wa urais alioutaja, na kusisitiza hana kundi, hakuwahi kuzungumza wala kuhudhuria vikao vya kundi, na kwamba kundi lake ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mwenyekiti wake ni Jakaya Kikwete.

“Sina kundi. Sijawahi kuwa na kundi na sitarajii kuwa na kundi. Ninachojua kundi langu ni CCM na Kiongozi wake ni Mwenyekiti wake, Rais Kikwete,” alisema Dk. Magufuli akipuuza taarifa kuwa alichangia Harambee hiyo akisema,

“Si kweli, Mwanza sijatoa hata senti na hata siku ilipofanyika hafla hiyo, nilikuwa Dar es Salaam katika mkutano na makandarasi.”

Licha ya kutajwa kuwa miongoni mwa vinara wa urais 2015, Magufuli alieleza kuwa hakuwahi kuzungumza na Sitta suala  linalohusu makundi ya urais 2015.

Baadaye Sitta alikiri kuwa hawakuwahi kuzungumzia suala la kuwania urais isipokuwa ni hisia zinazojengwa na kuwa majina yanatajwa kuwa wanautaka urais.

Hata hivyo siku chache baada ya Magufuli, kumruka kimanaga  Sitta, akisema hahusiki na kundi la mbio za urais 2013, Waziri Mark Mwandosya, naye pia aliruka kiunzi akisema Ikulu bado ina mpangaji.

Wakati Profesa Mwandosya akimsuta hivyo Sitta, Mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja, naye alimshukia Sitta akisema ni msaliti na anayepaswa kufukuzwa kwenye chama.

Mgeja akikurupuka na kufyatua maneno hayo makali! Sijui  kama anafahamu usemi usemeo, Kuvuja kwa Pakacha ni Nafuu ya Mchukuzi!.


Ni rai yangu kwa Sita afahamu haya; Waswahili wanasema, ‘Akumulikaye mchana, Usiku atakuchoma’. Kama anaosema rafiki zake, baadhi yao wamemsaliti na kubakia na wachache ambao hawajasema Neno kwa Ishara ya kukubali, Je walimkusaliti, ana urafiki nao wa kweli?

Nina Neno moja tu na Sitta, aelewe Mungu hutangaza kutoka Mwisho kwenda Mwanzo! Na Mungu aliwaambia wana Israel, Mlivyouzunguka Mlima huu vyatosha; geukeni upande wa kaskazini” (Kumbukumbu la Torati 2:3).


Akanena tena, “Angalieni, nimewawekea nchi mbele yenu, ingieni mkaimiliki nchi Bwana aliyowaapia baba zenu, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kwamba atawapa na uzao wao baada yao”.Kumbukumbu la Torati 1:7-8”  

Baada ya hayo, Nanukuu: “Ndipo mfalme akamwamuru Ebedmeleki, Mkushi, akisema, Chukua pamoja nawe watu thelathini toka hapa, ukamtoe Yeremia shimoni, kabla hajafa.

“Basi Ebedmeleki akawachukua watu hao pamoja naye, akaingia ndani ya nyumba ya mfalme chini ya ghala, akatoa mle nguo zilizotupwa, na vitambaa vikuukuu, akamtelemshia Yeremia shimoni kwa Kamba.

“Naye Ebedmeleki, Mkushi, akamwambia Yeremia, Tia nguo hizi zilizotupwa, na vitambaa hivi vikuukuu, chini ya kamba kwapani. Naye Yeremia akafanya hivyo.  Basi wakamwinua Yeremia kwa kamba hizo, wakamtoa shimoni; naye Yeremia akakaa katika uwanda wa walinzi”.

Sitta; kutenda Kosa si Kosa, ila kurudia Kosa! Je; Sitta Aokolewe kwenye Kisima cha Matope? Ndiyoooo!!

nyeregete@yahoo.co.uk 0715-933308

NB: Picha za Magufuli na Sita zinazotazama.

No comments:

Post a Comment

Pages