HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 05, 2013

MBIO ZA TABORA MARATHON 2013 ZAZINDULIWA RASMI

 Mshauri wa Ufundi wa Tabora Marathon, Tullo Chambo (kushoto), akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika uzinduzi wa mbio hizo zinazotarajia kufanyika Juni 22 mjini Tabora. Mkutano huo ulifanyika kwenye Ukumbi wa Yami Yami Garden Restaurant (zamani City Garden) katikati ya jiji.
 Mshauri wa Ufundi wa Tabora Marathon, Tullo Chambo (kushoto), akisisitiza jambo wakati akizungumzia maboresho ya zawadi kwa washindi wa Tabora Marathon 2013. Kulia ni Mratibu wa mbio hizo Ramadhani Makula.
 Mratibu wa Tabora Marathon, Ramadhani Makula (kulia), akizungumza na wanahabari (hawako pichani) katika mkutano huo wa uzinduzi uliofanyika Yami Yami Garden Restaurant jijini Dar es Salaam leo mchana.
Mshauri wa Ufundi Tullo Chambo (kushoto), akionesha kwa wanahabari (hawako pichani), zawadi ya mshindi wa kwanza km 21 kwa wanawake. Kulia ni Mratibu Ramadhani Makula akionesha moja ya medali za dhahabu zitakazotolewa kwa washindi wa mbio hizo.

DAR ES SALAAM, Tanzania

“Licha ya aina ya mbio kuwa kama mwaka jana (km 21, km 16 na km 5), maboresho yetu yako katika zawadi, ambapo washindi wa kwanza hadi wa tatu wataibuka sio tu na fedha taslimu kama mwaka jana, bali pia watapata vikombe na medali za Dhahabu, Fedha na Shaba”

KAMATI ya Mashindano ya Riadha ya Tabora Marathon, imezindua rasmi mbio hizo huku ikitangaza maboresho zaidi, ikiwamo fedha taslimu na zawadi ya vikombe na medali kwa washindi wa kwanza hadi wa tatu wa mashindano hayo ya kila mwaka.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mshauri wa Ufundi wa Tabora Marathon, Tullo Chambo, alisema licha ya maboresho, mbio za mwaka huu zitakuwa kama za mwaka jana, ambazo ni km 21 wanaume, km 16 wanawake na km 5 kwa watu wazima.

“Licha ya aina ya mbio kuwa kama mwaka jana, maboresho yetu yako katika zawadi, ambapo washindi wa kwanza hadi wa tatu wataibuka sio tu na fedha taslimu kama mwaka jana, bali pia watapata vikombe na medali za Dhahabu, Fedha na Shaba,” alisema Chambo.

Aliongeza kuwa, kwa kutambua historia ya mkoa wa Tabora katika Riadha, Kamati yake imeona umuhimu wa kuitumia fursa hiyo kuwekeza mchango wao katika mchezo huo, ili kuwanufaisha wakazi wa mkoa huo, lakini pia taifa kupata wanariadha watakaoliletea sifa.

Aidha, Mratibu wa Mashindano hayo, Ramadhani Makula, aliwashukuru wadau muhimu kwa kusaidia harakati za kuifikisha Kamati yake ilipo kimichezo, huku akiwataja baadhi yao kuwa ni Mkurugenzi wa NGS CO. Ltd ya Simiyu Njalu Silanga, Mmiliki wa Mtandao wa Kijamii wa Habari Mseto Blog, Francis Dande na Emmanuel Mwakasaka wa Tabora mjini

Wengine waliotajwa kutoa mchango uliotukuka kwa Kamati ya Tabora Marathon ni pamoja na Hamisi Kigwangala (Mbunge wa Nzega), Sarah Ramadhani wa Dar es Salaam, mwanariadha Banuelia Brighton na Taasisi ya Filbert Bayi Foundation.

Makula akazitaka taasisi, kampuni na wadau mbalimbali wenye nia ya dhati ya kuleta maendeleo ya michezo hasa riadha kujitokeza kudhamini Tabora Marathon, ili kuibua na kuindeleza vipaji vya mchezo huo, kwa mkoa ambao ulisifika kutoa wanariadha mahiri.

No comments:

Post a Comment

Pages