Na
Elizabeth John
VIJANA wa Kitanzania wameshauriwa
kutobweteka badala yake wajishughulishe na kazi mbalimbali sio kutegemea ajira
za serikalini pekeee.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es
Salaam jana na Mchoraji wa michoro ya Tingatinga, Abbas Mbuka na kwamba yeye anajivunia
kuwa mchoraji wa michoro hiyo kutokana na faida anazozipata.
“Mimi
nawashauri watanzania wenzangu wafanye kazi mbalimbali na sio kukaa tu mitaani
kama wanavyofanya vijana wengi, mimi napata kipato cha kunitosheleza kupitia
kazi hii kinachotakiwa ni ubunifu tu,” alisema.
Alisema kupitia kazi hiyo aliweza
kuhudhulia mkutano wa tano wa kuzungumzia Maendeleo ya nchi za Afrika
ujulikanao kama Tokyo International Conference on African Development (TICAD -
V) mjini Yokohama, Japan ambapo aliweza kuonesha jinsi ya kuchora michoro hiyo
pamoja na kuziuza kwa raia wa huko.
Alisema mkutano huo uliwashirikisha
viongozi wa Afrika akiwemo Rais Jakaya Kikwete, viongozi wa Japan na mashirika
ya maendeleo ya Afrika ikiwamo Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB), Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU) na Shirika la
Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP).
Alisema awali picha za michoro hiyo ya Tingatinga ilianza kuuzwa Fukohama, Goya
ambapo waliuza picha 160, Wosaka waliuza picha zaidi ya 100 na Yokohama waliuza
picha zaidi ya 220.
Alisema lengo la picha hizo kupelekwa
nchini Japan ni kuonyesha vitu mbalimbali vinavyopatikana Afrika kupitia
michoro ya sanaa hiyo ya Tingatinga.
Alisema katika mkutano huo, kila nchi
ilikuwa inaonyesha bidhaa zao, hivyo na wao walipata fulsa ya kuonyesha za
kwao, na kufanikiwa kuuzika zaidi na walivyotarajia.
Mbuka alisema bado nchini humo kuna
watu ambao wanaona wanyama kwenye luninga, hivyo kuona kwao katika michoro
kunawafanya wajifunze mengi zaidi kutoka Afrika.
“Wasanii wa Tingatinga tunaweza kufika
mbali sana, kwani michoro yetu inakubalika kila nchi na hii itawafanya pia watu
waamini kuwa michiro ya Tingatinga imetokea Dar es Salaam Tanzania na si nchi
nyingine kama watu wanavyosema,” alisema Mbuka.
No comments:
Post a Comment