Na Mwandishi Wetu
WASANII mbalimbali watakaoshiriki katika Tamasha la Wazi la Filamu Tanzania, maarufu kama ‘Grand Malt Tanzania Open Film Festival’ ambalo litafanyika jijini Mwanza kuanzia Juni 30, wanatarajia kutoa misaada mbalimbali kwa jamii.
Wasanii hao ambao wamewasili Mwanza leo wanatarajiwa kutembelea hospitali ya mkoa ya Sekou Toure, ambapo pia watatoa msaada wa vyandarua.
Mratibu wa tamasha hilo, Musa Kissoky, alisema wasanii hao watatoa msaada huo wa vyandarua, ikiwa ni mchango wao kwa jamii katika kupambana na malaria.
“Tayari wasanii karibu wote wameshawasili Mwanza, hivyo kesho (leo), wanatarajiwa kutembelea hospitali ya Sekou Toure na kutoa msaada wa vyandarua,” alisema.
Kuhusu maandalizi, Kissoky alisema, kwa sasa yamekamilika kwa asilimia 90, hivyo wakazi wa Mwanza wasubiri kuona vitu tofauti katika tamasha hilo.
Naye Meneja wa kinywaji cha Grand Malt walio wadhamini wakuu wa tamasha hilo, Consolata Adam, alisema wameamua kufanya kweli zaidi kwani wanataka kuona Watanzania wanapata kitu chenye uhakika.
“Tumejipanga katika hili na wala hatutanii kwani tunataka kuwawezesha wakazi wa Mwanza na maeneo ya jirani kuhudhuria tamasha hili kwa wingi.
“Tunawakaribisha watu wote wenye mapenzi na filamu zetu za Tanzania kufika na kushuhudia tamasha hili ambalo mwaka huu limeboreshwa zaidi,” alisema Consolata.
Tamasha hilo linatarajiwa kuanza Jumatatu ijayo, ambapo kutakuwa na maonyesho mbalimbali ya filamu pamoja na burudani za muziki kutoka bendi ya Extra Bongo, pamoja na ngoma za asili.
Tamasha hilo la filamu limedhaminiwa na kinywaji cha Grand Malt kisicho na kilevi ambacho kinazalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
No comments:
Post a Comment