HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 08, 2013

Wasomi wanaposema CCM IJiandae kuondoka kwa aibu! Kulikoni?

Na Bryceson Mathias

‘Uzuri wa Mkakasi, Ndani Kipande cha Mti!’

NIMEPATA mshitiko kuona Wasomi nchini, sasa wameamua kuwatetea wananchi waziwazi, na huu ndio wajibu wao, ambapo wanapaza Sauti kusema Chama cha Mapinduzi (CCM) Kijiandae kuondoka madarakani kwa aibu hata kama kikiiba kura.
Kauli hiyo iliyotolewa mbele ya Mwakilishi wa Serikali Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Steven Wasira, inaakisi kuwa waliowasomesha wasomi hawa (Walipa Kodi), sasa wana ufahamu wa kutosha kuwa;

Wakati wa Chaguzi za Mafiga Matatu ya Uongozi nchini, kura huwa zinaibiwa, huku Serikali ya CCM ikinyamaza, ingawa inaona na kufahamu wazi hayo yanafanyika lakini inayanyamazia, kama ilivyo Rushwa, Ufisadi na Dhuluma! Hivyo imefikia pa kuyamwaga hadharani! Yamezwe.

Kama Kauli hiyo imetolewa na Msomi Mzito anayesifika na kufahamika kwa Utashi wa maadili mema asiye na Mawaa, Makamu Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Augustine (SAUT) cha mkoani Mwanza, Dk. Charles Kitima, na kushangiliwa sana na walalahoi! Tujiulize.

Wasira na Dk. Kitima walikuwa kwenye mjadala wa Dira ya Maendeleo ya Serikali, uliofanyika mbele ya wanafunzi wa Chuo cha SAUT Nyegezi Mwanza, ambapo mambo yalivyo sivyo ndivyo serikalini na CCM, yalipaziwa sauti mbele ya Vizazi vinavyolia.

Dk. Kitima alisema, Licha ya Wasira kutokuwa Fisadi na Mwanafunzi mzuri wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wenzake ndani ya Serikali na CCM si waadilifu, hivyo alimtaka awaambie wajiandae kuondoka kwa aibu, wasipobadilika.
Lingine lililopaziwa sauti kwa mwakilishi wa Serikali huyo, ni kwamba CCM imeonyesha Udhaifu mkubwa katika kusimamia baadhi ya mambo, hivyo wajiandae kuondoka kwa aibu.

Sauti ya Dk. Kitima ambaye kimsingi analea watoto walio wengi wa Walalahoi wanaoonja Maisha Magumu SAUT, kunaonesha Wananchi wamechoshwa na Ubabaishaji unaofanywa na baadhi ya Viongozi wa CCM na Serikali, unaosababisha waichukie Serikali yao.

Viongozi wachache wanajaribu kufunika Kombe mwanaharamu apite kwa kutoa Lugha za udanganyifu, lakini ukweli unabaki palepale na kibaya zaidi, usanii wa kubadili ukweli kuwa uongo, unawaelevusha wananchi na kufikia kuichoka Serikali yao.

Nanukuu moja ya msisitizo wa Dk. Kitima kwa Serikali na CCM,  “Mfano mzuri, Singapore wao walianza kusimamia utalii, Serikali yetu ilikosea sana kutokutekeleza mambo ya uzalishaji. Msipotekeleza hili, CCM mtaondoka madarakani.

“Ulaji mkubwa wa fedha umeingilia sekta ya elimu, hamtekelezi kwa vitendo sera na dira za taifa. Nasema msipobadilika serikali ya CCM itaondoka na hata mkiiba kura, lazima mtaondoka tu, tunawaandalia wapinzani,” alisema Dk. Kitima kisha ukumbi mzima ukamshangilia kwa nguvu.

Dk. Kitima ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alisema Rais Jakaya Kikwete anao mawaziri watatu tu ambao wana mlengo chanya wa kuikomboa nchi.

Alibainisha kuwa kitendo cha serikali kuruhusu wawekezaji kuingia nchini na kudharau wazawa na mali zao, hilo litakigharimu na kuiangusha CCM.

Naungana na Dk. Kitima kwa sababu Mawazo  yake ni mazito na ya kweli, kwa sababu kwa uchunguzi wa wawekezaji wa namna hiyo waliomo nchini, wanaongozwa na Vigogo wa nchi hii waliojificha nyuma ya mgongo wao hasa viwanda vya sukari na vingine.

Pia Kitima alienda mbali akibainisha kuwa, kwa sasa vikao vya Bunge, hoja za msingi zinapingwa huku mtoa hoja akizomewa, lakini mambo ya kipuuzi ndiyo yanayoshabikiwa na wabunge wengi na Kiti, Jambo linalowaamsha Wananchi na kutunzwa kumbukumbu mioyoni.

Ingawa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Steven Masatu Wasira, ameliwashukia watumishi wote wanaojihusisha na ubadhirifu wa mali za nchi na kusema lazima watu hao wahenyeshwe kwa kuchukuliwa hatua bila kuonewa aibu, bado naona kauli yake ni ya kisiasa zaidi.

Mtalaam mmoja wa Tabia za Ndege alisema, Kauli za kisiasa kimsingi zinafanana na Uongo wa Jogoo kwa Tetea. Alidai; Jogoo anapomzunguka Tetea na kuinamisha  Bawa lake kulia au kushoto husema, “Nitakununulia Gauni kuzunguka huku na Mpaka Chini’.

Alisema, Nia yake kubwa huwa ni kufanikisha mambo yake ya kibinafsi lakini si kweli kuwa huwa anataka kuwasaidia Tetea Mahitaji yao.

Ukifuatilia hadi hadi leo, Jogoo hajawahi kutimiza isipokuwa kila kukicha huipaka rangi. Leoa anatumia Udini, Kesho Ukabila, Mtongoo, Mabomu na Maji ya kuwasha na Rasimu ya Katiba.

Wasira ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi, alianza kwa kusema: “Mimi nachukizwa sana na wanaoiba mali za nchi. Sipendi wizi na siwezi kuiba wala simung’unyi maneno kusema hili.”

Alisema wapo baadhi ya watumishi wanapoingia kwenye ajira kazi yao ni kuanza kuiba badala ya kujenga taifa, jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo ya nchi, na kwamba fedha za EPA zilizorudishwa na wezi na zimetumika kuinua kilimo. Mbona watu hao hawajachukuliwa hatua?

Aliongeza kuwa, Kupungua kwa uadilifu hapa nchini ni tatizo kubwa, na linaweza kuleta mgogoro mkubwa na kudidimiza zaidi uchumi wa nchi, hivyo lazima kila Mtanzania awe muumini mzuri wa uzalendo.

“Rasilimali zote za nchi lazima zitumike kuwanufaisha Watanzania wote. Na bila hivyo hakuna nchi"

“Kupungua kwa uzalendo na uadilifu ni tatizo kubwa sana kwa nchi. Lazima tuenzi amani na upendo...ukishindwa kulinda na kuiheshimu Tanzania wakati na wewe ni Mtanzania hufai,” alisema Wasira.

Alidai rasilimali zote yakiwemo madini, maziwa, utalii na nyinginezo nyingi ni vema zikageuzwa kuwa mali zinazonufaisha na kuleta maendeleo kwa wananchi na kwamba dira ya maendeleo ya taifa ni kuboresha fursa nyingi za kiuchumi.

Alimalizia ili kufikia malengo halisi, mpango wa serikali uliopo sasa ni kuboresha huduma za viwanda, reli, viwanja vya ndege, kilimo bora, bandari, maliasili, miundombinu na nishati.

Ieleweke kwamba, ndiyo maana tunasema, ‘Uzuri wa mkakasi, ndani kipande cha Mti!’! Ni aibu kama tukisema tuna miundo mbinu mizuri ya Rami nchi nzima na yote aliyosema Wasira ni kweli, lakini kama wananchi wanaishi maisha Magumu, Dhuluma na kutukanwa na wawekezaji nchini mwao, niseme ni aibu na ni utumwa.

Aidha sasa tunataka! Anachosema Wasira, Serikali yake na CCM, Vikifanye kwa matendo. Mwizi aitwe mwizi, Fisadi aitwe Fisadi, Jambazi aitwe Jambazi, na hatua zichukuliwe dhidi yao badala ya kuwaita mwizi hakuiba kasogeza, Fisadi Mwekezaji, na mambo kama hayo!


No comments:

Post a Comment

Pages