HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 19, 2013

CCM isiwaadhibu Wananchi, ikalia yenyewe!

NAPE
Na Bryceson Mathias

HIVI karibuni Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kutumia Ubabe wa Kiti cha Spika na Uwingi wao bungeni, kiliwaadhibu wananchi kwa kupitisha tozo ya Sh. 1,000/- kwa kila laini ya Simu ya Kiganjani inayotumiwa na wananchi, huku wengi wakiwa ni walalahoi wasio na mlo mmoja.

Aliyetota hajui kutota! Mtu mwenye Maslahi yake binafsi au amenogezwa kitu kidogo, hata useme mpaka ulie utoe damu, hakusikii. Mfano; Wabunge wa Upinzani waliposema, Elimu tangu Darasa la awali hadi Chuo kikuu inaweza kuwa bure, walikejeli, leo wanalinadi hilo hilo!

Kutokana na ukweli, wabunge CCM walikuwa nyuma ya Serikali kufanya uamuzi wa kuweka tozo hiyo, na walipobaini wananchi wanaipinga, Chama hicho kupitia kwa viongozi wapiga vuvuzela si tarumbeta, wameanza kuruka kimanga kuepa hila na Makosa waliyofanya.

Tukumbuke, tozo hiyo ilipitishwa na Bunge katika kikao cha Bajeti hivi karibuni, na pia liliridhia Sheria ya Fedha, Serikali ilipopeleka mapendekezo juu ya tozo hiyo, na ilikuwa Bunge iyakubali au kuyakataa.

Zaidi ya theluthi mbili ya wabunge wa CCM na ukweli ni kweli ndio hao hao waliopitisha Bajeti ya Serikali na mapendekezo yake kuhusu tozo ya laini za simu, kama kawaida ya Kiti cha Spika, wanaosema ndiyo waseme Ndiyoo na wanaosema siyo..Ndiyooo, waliosema Ndiyo…wameshinda!.

Kama wahenga wanavyosema, ‘Mchelea Mwana kulia, hulia yeye’ Hatua ya CCM  kuilaumu Serikali pekee baada ya tozo hiyo kupingwa na wananchi ni kutoitendea haki na ni Unafiki, ila inataka kujinusuru kisiasa, ijifiche na kujikomba nyuma ya wananchi.

Maumivu wanayoyapata watanzania na watakayopata wananchi walalahoi nchini kuhusu tozo ya 1,000/- ya laini za simu na mambo mengine yanayofanana na hayo kama kudorora kwa Elimu nchini, sasa hivi wa kulaumiwa ni CCM na wapiga Vuvuzela badala wake!.

Kama nilivyosema, aliyetota hajui kutota, Ulikuwa ushabiki na hila za kisiasa, sasa wananchi wanaumia wakiwemo Babu zenu wazaa baba na mama, wajomba, mabinamu, Mabibi na shangazi zenu, kila mmoja anapigika; ‘Mchelea Mwana kulia, hulia yeye’.

Hata hii tabia ya kuwapiga watu mabomu ambayo mimi siipendi, hadi kuwaua akina, Daudi Mwangosi, Wanachama wa Chadema, wananchi wasio na hatia, Viongozi wa Dini misikitini na makanisani, na kuwatesa akina Absalomu Kibanda, Dk. Stephen Ulimboka hadi kuwang’oa kucha, ipo siku itakataliwa na wananchi kama laini. ‘Mchelea Mwana kulia, hulia yeye’.

Siku kadhaa nilimshangaa pia Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba, aliposema wizara yake haikubaliani na tozo hiyo. Ilinisikitisha kuona yeye kama Kiongozi wa wizara hiyo anapingana na dhana ya uwajibikaji wao wa pamoja,

Tozo hiyo iliwekwa na Serikali yenyewe, ambapo Makamba ni mmoja wa watendaji wake. Jamani! huo si mwendelezo wa utamaduni wa kuruka kimanga hata kama nao walishiriki katika chombo kilichoamua kuanzisha tozo hiyo inayopingwa na wananchi?.

Hali na usanii huo, ndio uliokifanya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimjie juu Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, kuacha unafiki wa kupinga kodi ya sh 1,000 kwa kila laini ya simu wakati wabunge wake ndiyo walioipitisha! Ndiyooo..ikimaanisha wananchi waumie!.

Hivo hatua anayofanya Nnauye, wananchi wanaona ni Usanii wa kisiasa kwa sababu ni sawa ujiumize halafu ulie mwenyewe. Wengine wanasema hiyo ni mbinu ya CCM ikitaka kujiosha, ili hadi badiliko litakapofanywa! Tayari watakuwa wamewakomba walalahoi fedha ya kutosha.

Tusiume maneno, kama Katibu wa Chadema, Amani Golugwa, alivyosema, kodi hiyo ilipitishwa kwa kishindo na wabunge wa CCM ambao ni wengi, wakati wale wa CHADEMA walipokuwa kwenye maombolezo ya wananchi wanne waliouawa kwa bomu, hivyo haiwezekani leo CCM kuikataa; Mchimba shimo, huingia mwenyewe!

Hapa ndipo watanzania tumtake Nape aache siasa za unafiki; awe mkweli tu, haiwezekani wabunge wa CCM wapitishe kodi inayowaumiza wananchi tena wa kipato cha chini, halafu ajikoshe kwenye vyombo vya habari akiipinga. CCM isingeikubali, kodi hii isingepitishwa bungeni, na hizi ndizo hasara za ndiyooo!

Utamaduni huu wa Undumila kuwili kwa wanasiasa wetu uchwara wa Taifa letu, ndio utakaolimaliza na kuliangamiza, hasa kutokana na baadhi yetu kupenda kuona damu za watu zikimwagiza kwa maslahi yao binafsi, huku wakitumia vitisho na udanganyifu wa hila.

Huko nyuma, ulikuwepo usanii wa Sheria ya Mifuko ya Hifadhi za Jamii ambayo ilipitishwa na Bunge kwa shinikizo la idadi ya wabunge wa CCM, lakini baadaye wakaruka kimanga kwa mbinu za kiitikadi baada ya sheria hiyo kupingwa kila pembe na kona ya nchi.

Ndio maana tunasema katika hili la tozo ya laini za simu, Bunge kupitia Kiti cha Spika linaloacha matusi yatolewe kwenye Taasisi tukufu miongoni mwa Mihimili yenye kuadabika, ndilo libebe lawama, Serikali na Chama Tawala, na si umaskini wa Jamii.

Ni rai yangu kwa Watanzania, katika hili la simu na mengine yanayofanana na hili kama la Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), kuwafanyia Usanii watanzania ili waangamie na Vyakula Feki, Madawa na Vipodozi huku wakijificha kwenye mazoezi feki ya Kamatakamata. Tupige kula ya Siyooooooooo!.

Aidha hata Ndege ana Makinda! Lakini siyo Spika; Sasa sijui kwa kura zetu za Siyooo! Kama Spika Anne Makinda, likirejea Bunge atasema waliosema Siyooooo! Wameshinda.

No comments:

Post a Comment

Pages