HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 24, 2013

MAJERUHI LIONEL MESSI AITWA KIKOSINI ARGENTINA

BUENOS AIRES, Argentina 

Vyombo vya habari nchini hapa vimehoji uhalali wa maamuzi hayo ya kocha Alejandro Sabella kumuita kikosini, yaliyotafsiriwa kama kuhatarisha usalama wa nyota huyo katika mfululizo wa michuano hiyo na ile inayoihusisha klabu yake

LICHA ya kuumia mguu wake wa kushoto wakati wa mechi ya Spanish Super Cup dhidi ya Atletico Madrid na kutarajia kukaa nje ya kikosi chake cha FC Barcelona, mshambuliaji Lionel Messi ametajwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Argentina.

Messi ambaye klabu yake imethibitisha kuwa atakosa mechi ya La Liga wikiendi hii dhidi ya Malaga, ameingizwa katika kikosi cha taifa na kocha Alejandro Sabella kwa ajili ya mechi ijayo kuwania kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Paraguay hapo Septemba 10.

Vyombo vya habari nchini hapa vimehoji uhalali wa maamuzi hayo ya kocha kumuita kikosini, yaliyotafsiriwa kama kuhatarisha usalama wa nyota huyo katika mfululizo wa michuano hiyo na ile inayoihusisha klabu yake.

Jina lake limechomoza miongoni mwa majina 18 tu ya kikosi hicho, akiwa pamoja na wakali kama winga wa Real Madrid, Angel Di Maria na mshambuliaji wa Manchester City, Sergio Aguero.

Kikosi cha Argentina kimetangazwa bila nyota wakali na tegemeo, wakiwamo Javier Mascherano, Gonzalo Higuain, Ezequiel Garay na Federico Fernandez ambao wote wanatumikia adhabu za kufungiwa, pamoja na majeruhi Fernando Gago.

Argentina ‘The Albiceleste’ kwa sasa wanakalia kilele cha msimamo wa Kanda ya CONMEBOL, ikiwa imepoteza mechi moja kati ya 13 ilizocheza, ingawa imeambulia sare tatu katika mechi zake tatu za karibuni.

Mechi yao ya mwisho kushuka dimbani ilikuwa ya ushindi wa mabao 2-1 katika mtanange wa kirafiki dhidi ya Italia iliyopigwa Agosti 14, shukrani kwa mabao ya Ever Banega na Higuain.

Kikosi kamili cha Argentina kwa ajili ya mechi hiyo kinajumuisha makipa: Sergio Romero (Monaco) na Mariano Andujar (Catania).

Mabeki ni: Pablo Zabaleta (Manchester City), Hugo Campagnaro (Inter), Fabricio Coloccini (Newcastle), Marcos Rojo (Sporting Lisbon), Jose Basanta (Monterrey), Cristian Ansaldi (Zenit).

Viungo ni: Ever Banega (Valencia), Lucas Biglia (Lazio), Augusto Fernandez (Celta Vigo), Ángel Di Maria (Real Madrid), Ricardo Alvarez (Inter), wakati washambuliaji ni: Lionel Messi (Barcelona), Sergio Aguero (Manchester City), Ezequiel Lavezzi (PSG), Rodrigo Palacio (Inter) na Erik Lamela (Roma).

Goal.com

No comments:

Post a Comment

Pages