Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal (katikati) akiwa na baadhi ya Viongozi wenzake kutoka nchi za Maziwa Makuu, wakati walipokuwa katika Mkutano wa Viongozi wa Nchi za Maziwa Makuu, alipoiwakilisha Tanzania katika majadiliano ya mkutano huo uliofanyika Jijini Nairobi, nchini Kenya jana Julai 31, 2013. Picha na OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiongozana na mkewe Mama Asha Bilal, (wa pili kulia) Balozi wa Tanzania Nchini Kenya, Dk. Batrida Burian, na viongozi wengine wakati alipowasili Jijini Nairobi juzi Julai 30, 2013 kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano wa Viongozi Wakuu wa Nchi za Maziwa Makuu, uliofanyika Jiji humo jana Julai, 31, 2013. Makamu anaondoka leo Jijini Nairobi kurejea nchini baada ya kumalizika kwa majadiliano hayo.
NAIROBI, Kenya
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib Bilal ameiwakilisha Tanzania katika mkutano wa Wakuu wa nchi za Maziwa Makuu uliofanyika jijini Nairobi Kenya, jana Jumatano ya tarehe 31, 2013.
Mkutano huu ulihudhuriwa na Mwenyeji wa Mkutano huo, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, Mwenyekiti wa nchi za Maziwa Makuu na Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, Katibu Mtendaji wa Kamisheni yas Nchi za Maziwa Makuu Prof.Ntumba Luaba, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika, wawakilishi wan chi za DRC, Zambia, Afrika Kusini, Rwanda na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa.
Mkutano huo umepokea taarifa kutoka kwa Mawaziri wa Ulinzi kutoka katika nchi za Maziwa Makuu ambayo imepokelewa na kisha kujadiliwa. Pia ripoti kutoka kwa Kamati ya Kimataifa inayoshughulikia suala la Mazungumzo kati ya Serikali ya Kongo (DRC) na wapiganaji wa kikundi cha M23 kinachojihusisha na upingaji wa serikali ya DRC kikifanya machafuko katika Mashariki mwa Kongo (DRC) imepokelewa kujadiliwa na kisha kupitishwa mapendekezo ambayo nchi washiriki zimeyasaini.
Wakati wa uzinduzi wa mkutano huo, nchi washirika walisisitiza kutaka kuona amani inapatikana katika nchi za Maziwa Makuu na hasa DRC, Afrika ya Kati na Sudan. Wawakilishi hao walielezea kusikitika kwao kutokana na machafuko ya amani katika nchi hizo na wakawataka viongozi mbalimbali wanaotajwa kuhusika na machafuko haya kutambua kuwa athari inayotokana na machafuko haya ni kubwa na inaathiri wananchi wengi.
Viongozi hao walisema, nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu zinahitaji utulivu na kwamba mgogoro wa uvunjaji amani katika Kongo DRC unaotokana na kuwepo kwa kikundi cha M23, lazima upewe tiba ya kudumu ili eneo hilo libakie tulivu na watu wake waweze kupata fursa ya utulivu utakjaowasaidia kushiriki katika kazi zao za kila siku.
Akifunga mkutano huo kwa niaba ya Mwenyekiti Yoweri Museveni, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alisema ni wakati sasa nchi za Maziwa Makuu kutambua na kuazimia kwa kauli moja kuwa amani inahitajika katika nchi zote za ukanda huu. Akifafanua zaidi Mheshimiwa Rais Kenyatta alisema wananchi wa ukanda huu wanataka ajira na sio mapigano.
“Hata vijana wanaotumika katika mapigano, tukumbuke kuwa baada ya mapigano watakachohitaji ni ajira. Akina mama na watoto wanataka kuona maisha yao yanaboreshwa na sio vionginevyo. Kwa namna nilivyoona tukishiriki katika mkutano huu ni dhaihiri tumeonesha nia ya dhati ya kuhakikisha maeneo yetu yanakuwa na amani. Tudumishe nia hii nzuri,” alisema Rais Kenyatta.
Makamu wa Rais na msafara wake wanarejea nyumbani leo Alhamisi Agosti Mosi, 2013 tayari kuendelea na majukumu mengine ya kitaifa.
Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais
Nairobi, Kenya
Agosti 01, 2013
No comments:
Post a Comment