Na Bryceson Mathias
Kuanzia Septemba 27, mwaka huu Magazeti ya Mtanzania na Mwananchi yamefungiwa madai yantoa habari za uchochezi dhidi ya Vyombo vya Dola na wananchi .
Gazeti la Mtanzania limefungiwa kwa siku 90, Mwananchi limefungiwa siku 14, huku wadau mbalimbali wakijitokeza kulani na kuipinga adhabu hiyo kwani imetumia sheria Kandamizi ya magazeti ya mwaka 1976 inayolalamikiwa na wadau wa sekta ya habari.
Kimsingi Serikali inatakiwa kujipima upya maana tabia iliyokthiri ya kuyafungia magazeti bila hata kuwa na radha, unaichora vibaya Tanzania mbele ya Wananchi, Jamii ya kiataifa na Kimataifa kwamba haina dhima halisi ya kutaka watu wahabarishwe hata kwenye haki yao.
Mhalifu akilihalifu Taifa tunamuita ni adui wa Taifa, Je sasa wananchi wakiita Serikali ni Mhalifuni wa habari dhidi ya haki wananchi kuhabarishwa watakuwa wamekosea? La hasha kwa sababu wanaona Uhalifu huo kwa macho yao wenyewe bila kuambiwa.
Bado siamini kama Serikali Makini na Sikivu inaweza kuishia kupambana na Magazeti badala ya kupambana na Madawa ya kulevya yanayoitesa Jamii ya Kitanzania na kuathiri kama si kuharibu kabisa nguvu kazi yake ya Vijana.
Kwa nini Serikali isijikite kuhakikisha inawaondoa wahamiaji Haramu wanaopenya kila siku kuingia nchini mwetu kwa njia za panya, badala yake inahangaika na magazeti? Wakulima wanapelekewa Mbolea na Mbegu feki zisizo na virutubisho na kuua mazao yao. Inafanya nini kwenye magazeti?
Zahanati, Vituo vya Afya nchini havina Dawa, Mashine za kupimia maradhi yanayotesa watu wake na wengi kupoteza maisha kwa vifo! Kwa nini inapoteza muda mwingi kuhangaika na magazeti yenye vyombo vya maamuzi?
Yawezekana yuko Mtu mmoja serikalini au kundi la watu; wanatumia nafasi zao kuwafanya Watanzania waichukie Serikali yao kwa binfasi, jambo ambalo kama si uchochezi mkubwa kuliko ule wa Mtanzania na Mwananchi, basi ni Uhaini.
Ni rai yangu Serikali ielewe kuwa, pamoja na kero zingine ambazo zimeendelea kuwatoa machozi watanzania kila siku kuchwapo, sasa inatengeneza bomu lingine ili ichukiwe na walaji wa habari za magazeti na ndugu za wanahabari.
Ukitaka kujua ni wadau wangapi wataichukia Serikali yao! Piga hasabu ya wandishi na wadau wa habari wako wangapi nchini, watoto wao, wajukuu, vilembwe na marafiki wangapi kwa upande wakiume na kike wenye uwezo wa kupiga kura! Halafu pata Jibu.
Si jambo jema kwa Serikali kujidanganya, inaweza kunywa sumu kwa madai itawahi kunywa maziwa kuizima sumu. Hizo ni ndoto za alinacha ambazo Serikali yenye upeo haiwezi kutegemea maziwa. Kama Breki za gari hufeli, Sumu nayo hufeli!.
Kwa muda mrefu masikio na na macho ya watanzania yalizoe kusikia na kuona Ufisadi wa Mabilioni ya fedha kwenye sekta zingine lakini sasa watanzania wanaanza kusikia machungu na kuona Ufisadi wa Habari ambapo naamini wanahabari nao wakifanya maamuzi hali itakuwa siyo nzuri.
Hali itakuwa sio nzuri kwa maana ya kwamba, pengine nao wataamua kugoma kuandika habari za Serikali, au Wamiliki wa Vyombo nao wataungana na Wafanyaka wao, jambo ambalo kimtazamo linaonekana litakuwa baya.
Sioni kama na sisi Tanzania kama tumefikia mahali pa kupelekana ‘The Hague’ kama walivyofanya zetu Kenya kwa Uhalifu wa Mauaji ya Watu. Hivyo kwetu itakuwa aibu kukapelekana kwa kufungia magazeti.
nyeregete@yahoo.co.uk 0715-933308
No comments:
Post a Comment