Na Bryceson Mathias
WAKATI wanasiasa wengi bila kujali itikadi za vyama vyao na Dini, wamepinga Vikali Sheria iliyopitishwa kwa nguvu ya Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kipindi cha Bunge la Bajeti na kutaka utekelezaji wake uanze Julai 30. Watu wa Kada mbalimbali wanalia.
Sababu ya watu hao kulia wanahoji bila kumung’unya maneno iwapo ni kweli kwa sheria hiyo waliyoipitisha huku fika ikionekana inawakandamiza watanzania walalahoi, Wabunge wa CCM wana Huruma na Watanzania?
Kamati ya Bunge ya Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), ndiyo iliyotaka kuwapo kwa kodi hiyo kwa madai ya kodi hiyo kusaidia shughuli za bajeti ya serikali kuu.
Mbali ya malalamiko ya wanasiasa hao wakiwemo na CCM, walimsuta Chenge aliyelazimisha kuwapo kwa kodi hiyo, huku akishindwa kujua kuwa kuna watanzania wanaokosa hata kula mulo mmoja siku! Je watakuwa na uwezo wa sh 1,000 kila mwezi kwa ajili ya laini ya simu?.
Si rahisi kwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Waziri wa Fedha, William Mgimwa, na familia za wakashindwa kulipia kodi hiyo ya simu ya Sh.1,000/-, maana wana ahueni ya Maisha, hivyo hawaaweza kusema iondolewa, inawaumiza!
Wanaoweza kuthubutu kutamka hayo ni walalahoi wanaosikia maumivu, ambao hata wakipaza sauti zao kusema, agharabu zinaweza zisisikike popote kutokana na mgandamizo uleule uliotumika kuipitisha sheria hiyo kwa nguvu bila kujali maslahi ya waliowengi.
Ijapokuwa kodi hiyo inawabebesha wananchi Mzigo, wako watu wakiwemo baadhi ya wabunge, hawana utu! Wamefikia mahali pa kusema bora mzigo ufike hata kama Punda atakufa. Utakuwa na Mzigo nyumbani lakini gharama ya kumpata punda mwingine ni kubwa.
Kama wabunge hawatakaa, wakaweka Bongo na akili zao pamoja, na kuweka mbali itikadi zao watafute namna gani wajaze pengo la sh bilioni 178/- zinazohitajika kusaidia shughuli za bajeti ya serikali kuu. Bunge na Serikali vitakuwa vinawatwisha watu mzigo wasiuoweza.
Watanzania kukandamizwa na Kodi hii ya simu kunatarsirika na watu mbalimbali kwamba, huenda Waziri wa Fedha Msigwa, amezidiwa nguvu na kiti cha spika kinachounga mkono hoja ya Chenge bila kujali kilio na maumivu ya walalahoi walio wengi ambao hata chai hawanywi.
Mimi najiuliza kwa nini wabunge wa CCM watake kumchinja Ng’ombe wa Maskini aliyekonda, badala ya Tajiri aliyenona? Serikali imenona lakini wanananchi walalahoi wamekonda na maisha Magumu yaliyotufikisha hapa! Wabunge waelewe Ng’ombe hanenepi siku ya Mnada!
Ni rai yangu viongozi wa Siasa na Serikali wafahamu kwamba, Ng’ombe hakamuliwi maziwa bila kulishwa atatoa Damu! Mizigo ambayo watanzania wanabebeshwa kwa sasa kiasi cha kuwafanya washindwe hata kupumua, ndiyo pia inayosababisha kushuka kwa elimu.
Mfugaji mmoja wa Jamii fulani alipewa nafasi atoe salamu za rambirambi kwa wafiwa kwenye Msiba akasema, Marehemu ‘imependesa sana! Imependesa haikupendesa? Watu kimya! Kilio kikaongezeka!
Wakati watanzania wana Changamoto za Njaa, Maisha Magumu na Misiba mbalimbali, Serikali na Wabunge wasiwe kama Mtu anayeamua kupeleka Kadi ya Mwaliko wa Mchango wa Harusi kwenye Msiba, si aibu tu! Ila inasikitisha.
Mgimwa na Chenga, kwa Kodi ya Laini za Simu, ni kama wamewapelekea Watanzania Mwaliko wa Mchango wa Harusi kwenye Msiba, hawajali kilio na huzuni ya waombolezaji.
nyeregete@yahoo.co.uk 0715933308


No comments:
Post a Comment