Watanzania
wametakiwa kutumia maktaba zilizopo kusoma vitabu na machapisho yaliyopo ili waweze
kujiongezea elimu na ufahamu zaidi wa masuala mbalimbali yahusuyo maisha na
elimu kwa upana wake.
Wito huo umetolewa jana
na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akifungua maktaba ya watoto iliyojengwa
na Serikali ya Korea Kusini kupitia
Taasisi ya Step katika shule ya msingi Mzimuni iliyopo wilaya ya Kinondoni jijinii
Dar es Salaam.
Mama Kikwete ambaye pia
ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema elimu ni
ufunguo wa maisha na kwa njia hiyo Taifa linaweza kupambana na kushinda vita
dhidi ya maadui wakubwa watatu ambao ni ujinga, umaskini na maradhi na matokeo
ya ushindani huo ni kupatikana kwa maendeleo.
“Pamoja na mafunzo
tunayoyapata shuleni, vyuoni na sehemu za kazi bado tunapaswa kuendelea kusoma
zaidi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupambana na adui ujinga, maradhi na
umaskini”, alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti huyo wa Wama
pia aliwataka walimu wa shule hiyo kutunza maktaba hiyo ili iweze kukidhi
malengo ya kuanzishwa kwake kwa kuandaa taratibu bora za kusimamia matumizi na
kuzuia upotevu na uharibifi wa vitabu na vifaa vingine.
Kuhusu suala la
utandawazi Mama Kikwete alisema ni
muhimu jamii ikatunza na kuimarisha utamaduni ili hali wamo katika
utandawazi kwani hivi sasa Dunia imekuwa kama kiganja cha mkono kutokana na kukua
kwa Sayansi ya Teknolojia ila hayo yote yanawezekana ikiwa watasoma zaidi eneo
husika kulingana na mabadiliko yaliyopo.
Mama Kikwete alisema,
“Leo hii tumepata maendeleo kwa ajili ya Sayansi na Teknolojia kwani ukitaka
kujua chochote kinachoendelea Duniani ni rahisi kwa kuwa unaingia katika
mitandao na kuona, hili ni jambo zuri lakini liendane na mila na utamaduni wetu
siyo kila jambo unalichukua, chukua yale mazuri ambayo yatakusaidia na yale
mabaya ambayo hayana maslahi kwa taifa
yaache”.
Kwa upande wake Balozi Young –Shim Dho ambaye ni Mwanzilishi
wa Taasisi ya Step na Balozi wa mradi wa Utalii endelevu kwa ajili ya kuondoa
umaskini wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani alimshukuru Mama
Kikwete kwa kuifungua maktaba hiyo na kuwataka wanafunzi kuitumia kwa kujisomea.
Balozi Young –Shim Dho
alisema miaka michache iliyopita nchi ya Korea Kusini ilikuwa ni moja ya
nchi maskini Duniani lakini kupitia tabia
ya kupenda kusoma vitabu wamefanikiwa kuwa miongoni mwa nchi zilizomo ndani ya
G20 na kuwataka watanzania kutumia vitabu hivyo kusoma.
“Kujengwa kwa maktaba
hii na zingine 23 na kupatikana kwa vitabu pamoja na vifaa vingine vya maktaba
ni jitihada za Mama Kikwete ambaye alizunguka
huku na kule kuomba msaada ambao leo hii umefanikiwa na kuweza kuwasaidia
watanzania wengi”, alisema Balozi Young –Shim Dho.
Ndani ya eneo la shule ya Msingi Mzimuni kuna shule ya Msingi Mikumi
ambapo Mama Kikwete alimuomba balozi Young –Shim Dho kujenga maktaba kama hiyo
kwa ajili ya shule hiyo na Balozi huyo alikubali
na kusema kuwa ifikapo mwakani maktaba hiyo itakuwa imekamilika.
Hii ni maktaba ya 24
kujengwa hapa nchini kwa ajili ya watoto wa shule za msingi moja kati ya hizo
ni maktaba ya watu wazima iliyopo ndani ya Jengo la Makumbusho jijini Dar es
Salaam.
No comments:
Post a Comment