HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 31, 2013

WANACHAMA WAMNG'ANG'ANIA RAGE KUNG'OKA SIMBA
Wanachama wa Simba, wakizungumza kwenye ukumbi wa Idara ya Habari, Maelezo, Dar es Salaam., kupinga hatua ya Shirikisho la Soka Nchini TFF, kuridhia Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Aden Rage kuiendelea na uongozi. Meza kuu, kutoka kushoto ni Husein Mwaikambo kutoka Iringa, Albino Lwilla na Chuma Selemani maarufu wa jina la Hindu. (Picha na Francis Dande)

Na Mwandishi Wetu

KAMATI ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imezidi kushushiwa lawama na wanachama wa Simba kwa walichokiitwa ‘kumkumbatia’ Mwenyekiti wao, Ismail Aden Rage, na kwamba kwa sasa mchakato wa kujiorodhesha ili kupata akidi inayoruhusu mkutano wa kumng’oa unaendelea vizuri.

Kamati hiyo, ilimpa rungu Aden Rage kwa kumtambua kama Mwenyekiti halali wa Simba, baada ya kukutana kujadili barua ya bosi huyo aliyoituma kwa Kamati ya Utendaji ya TFF kuomba ipitie upya agizo la kumtaka aitishe mkutano mkuu wa dharura ndani ya siku 14 wenye ajjenda moja, ambayo aliigomea.

Baada ya Rage kugomea, Kamati ya Utendaji ya TFF ilikabidhi sakata hilo kwa Kamati ya Sheria, ambayo hata hivyo haikuja na karipio, adhabu wala utatuzi wa suala hilo licha ya ukiukwaji mkubwa wa katiba ya klabu hiyo uliofanywa na Mwenyekiti huyo ikiwamo kupuuza agizo halali la TFF.

Wakizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, baadhi ya wanachama wa matawi ya mkoa wa Dar es Salaam na wawakilishi kutoka matawi ya mikoani, walisema hawakubaliani kwa namna yoyote na uamuzi wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF.

Albino Lwila, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Tawi la Simba la New Mapambano la Temeke Dar, aliyaita maamuzi ya Kamati ya Sheria kuwa ni batili, huku akiishangaa kumtaka Rage ajaze nafasi ya Makamu wake Geofrey Nyange ‘Kaburu’ licha ya kutambua kwamba alishaenda kinyume juu ya nafasi hiyo.

“Kwa nini ukiukwaji wa katiba unaofanywa na Rage uko wazi na hakuna hatua dhidi yake zaidi ya kumkumbatia tu? Alipaswa kujaza nafasi ya Kaburu katika kipindi cha siku 90 kama katiba inavyotaka, leo ni siku ya 270 hajajaza, bado TFF inataka kumbeba kwa kumuamuru aijaze?’” alihoji Lwila.

Aliongeza kuwa, wao kama Simba wameumizwa na maamuzi hayo na kwamba hasira zao wanazimalizia katika kujiorodhesha kusaka idadi ya wajumbe 500 inayowaruhusu kuitisha mkutano wa dharura, ili kumuwajibisha Rage kwa kumng’oa madarakani na kuhitimisha zama zake klabuni hapo.

“Kwa sasa tumefikia wanachama 270 na naamini tutafikia 500 haraka ili kukata mzizi wa fitina. TFF inapaswa kutenda haki katika kusimamia soka la Tanzania na kutokumbatia wasiginaji katiba waliopo madarakani kwa maslahi binafsi kama Rage,” alisisisitiza Lwila huku akiungwa mkono na wenzake.

Msemaji mwingine katika mkutano huo alikuwa ni Hussein Mwaikambo, aliyejitambulisha kuwa ni Msemaji wa Simba tawi la Iringa Mjini, ambaye kwa upande wake alilitaka TFF kuona aibu kumlinda kwa gharama kubwa mtoto (Rage) aliyepinga agizo halali la baba yake (TFF) la kuitisha mkutano wa dharura.
“Tumeamua kufuata sheria, tutamwandikia barua Rage kumsisitiza ajiuzulu kwa hiari na nakala yake tutaipeleka TFF, asipotekeleza matakwa yetu, basi tutajikusanya kupanga uamuzi wa mwisho na kisha kuutoa,” alisema Mwaikambo huku akikana madai kuwa wanatumiwa na mtu kumpinga Rage.

Mwanachama mwingine, Ras Simba, alisema, yeye binafsi anashangazwa na vigezo vilivyotumiwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, akisema yeye ana imani na maamuzi ya Kamati ya Utendaji kwa kumsimamisha Rage, kwani walitumia ibara ya 12 (1) ya klabu yao inayozungumzia uvunjaji mkubwa wa katiba, kanuni, maagizo na maamuzi ya Simba.

Simba alibainisha kuwa,uvunjaji huo  unaweza kusababisha kusimamishwa kwa uanachama wa Simba kwa kipindi kisichozidi miaka miwili, kutokana na maamuzi ya Mkutano Mkuu, huku akisema sehemu ya pili ya inasema, kwa tukio la dharura kamati ya utendaji inaweza kutoa adhabu ya muda ya aina hiyo, katika hali hiyo, kusimamishwa kutadumu mpaka mkutano Mkuu unaofuata.
“Kutokana na ibara hiyo, Kamati ya Utendaji Simba ilikuwa sahihi kumsimamisha Rage huku wakisubiri zamu ya wanachama katika Mkutano Mkuu. Ila Kamati ya Sheria ya TFF, imekosea kwani Rage amekiuka katiba, alafu inamtaka aitishe Mkutano wa uchaguzi kwa misingi ipi akiwa amepoteza imani kwa wanachama?”alihoji Simba.

Wanachama wengine walioongea katika mkutano huo walikuwa ni Ali Mkumba, Chuma Suleiman ‘Bi Hindu’ na Ramadhani Mgeni ‘Macho,’ ambao kila mmoja alikiri kuchoshwa na sakata la Rage kupewa jeuri na TFF licha ya maovu yanayohusu ukiukwaji wa katiba ya Simba unaofanywa na Mwenyekiti huyo.

No comments:

Post a Comment

Pages