.Watakiwa kumfariji Rais Kikwete kwa medali
.Rais RT aipiga kombora Wizara ya Michezo
Wawakilishi wa wachezaji wa
timu za Tanzania wanaokwenda katika kambi ya mazoezi nje ya nchi kwa ajili ya
kujiandaa na michezo ya Jumuiya ya Madola, Samson Ramadhan (kushoto), na Neema
Mnaisyula (kulia), wakipokea kwa pamoja bendera ya taifa kutoka kwa Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe (wa tatu kushoto),
wakati wa kuaga timu zinazokwenda kuweka kambi nje ya nchi kwa ajili ya
maandali ya michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Julai, Glasgow,
Scotland. Hafla hiyo ilifanyika leo jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Francis
Dande)
Viongozi wa Shirikisho la
Riadhaa Tanzania (RT), wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe (wa nne kushoto),
viongozi wa Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo pamoja na wachezaji
wa Riadha watakaoshiriki michezo ya Jumuiya ya Madola, mara baada ya kukabidhi
bendera ya taifa kwa timu za Tanzania zitakazokwenda kuweka kambi nje ya nchi
kwa ajili ya michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Julai Glasgow,
Scotland.
Na Mika Ndaba
WAZIRI
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amewataka wachezaji
wanaokwenda katika kambi za kujinoa na Mashindano ya Jumuiya ya Madola
‘Commonwealth Games’ itakayofanyika jijini Glasgow , Scotland ,
Julai mwaka huu kuitumia vizuri ili waweze kurejea nchini na medali.
Membe,
aliyasema hayo jana katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere
jijini Dar es Salaam ,
wakati akiwaaga wachezaji 45 wanaokwenda nchi mbalimbali kushiriki mafunzo kwa
ajili ya kuboresha viwango vyao kabla ya mashindano hayo ya Madola.
Alisema
kitendo cha wao kufanya vizuri kitakuwa ni faraja kwa Rais Jakaya Kikwete, ambaye
amekuwa mdau mkubwa wa maendeleo ya michezo, amekuwa na kiu ya kuondoka
madarakani akiona medali zikitua nchini, hivyo waende wakitambua kuwa wamebeba
dhamana kubwa ya Watanzania ambao wamechoka kuona wakirejea mikono mitupu.
“Rais
alinipa ushauri kwamba vijana wetu wanakaribia kuingia kwenye michuano, hawa
ndio wamebeba dhima ya taifa, hivyo wanatakiwa kuandaliwa vizuri ili waweze
kuiletea nchi heshima mbele ya Wazungu,” alisema Membe huku akiwasihi
kujiepusha na vitendo vya kuzamia ‘kujilipua’, kubeba dawa za kulevya na
vitendo ambavyo vitaichafua fursa hii adhimu.
Alisema
endapo watafanya vema katika michuano hiyo, wanaweza kujikuta wako katika
maisha mengine, maana watageuka mashujaa wa Tanzania .
Kwa
upande wake, Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Anthony Mtaka, alisema
wachezaji hao wanatakiwa kufanya jitihada katika mafunzo yao, ili
watakaposhiriki Jumuiya ya Madola warejee na ushindi ili kuwavutia wadhamini
kuwekeza katika michezo mingine nje ya soka kama ilivyo sasa.
Alibainisha
kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuboresha mchezo huo na kuweza kuleta ushindi
nchini badala ya kubakia kuwa kama washiriki au watalii kama
ilivyokuwa hapo awali.
“Hakuna
mdhamini atakayejitokeza endapo tukishindwa, asilimia kubwa wamewekeza katika
mpira wa miguu. Licha ya kusambaza barua katika wizara nne, lakini tumejibiwa
moja tu na Mheshimiwa Membe, kwa hiyo inatakiwa kufanya vizuri kulipa fadhila
na kujiwekea hazina ya baadaye,” alisema Mtaka huku akitoa changamoto kwa wizara
yenye dhamana na michezo, kufanyia kazi hotuba ya Rais Kikwete siku ya Kifimbo
cha Malkia, Ikulu, badala ya kuigeuza wizara ya kulipana mishahara tu, bila
kuwajibika.
Katibu
Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi, alisisitiza kuwa wachezaji
wanaokwenda mafunzoni katika nchi walizopangiwa, wanatakiwa kushiriki vilivyo
katika mazoezi, kwani hakuna mchezaji atakayekwenda Glasgow bila ya kuwa na kiwango stahiki.
“Tutaondoka
na idadi ya wachezaji 50, lakini sisi tulipanga tuchukue watu 36, hivyo
kutokana na Waziri Membe kutaka washiriki wote waende, basi inatakiwa kufanya
juhudi za ushindi. Kwenda wote haimaanishi wengine wakatalii isipokuwa
kushiriki katika mazoezi, ili waweze kuwa fiti kwa mashindano na kubeba
medali,” alisema Bayi.
Timu
za riadha, ngumi, judo, kuogelea, mpira wa meza na kunyanyua vitu vizito,
ziliagwa jana, ambapo zitakwenza kujinoa China ,
Newzealand, Uturuki na Ethiopia .
Zitaanza kuondoka kuanzia kesho na kundi la mwisho litaondoka Mei 4.
No comments:
Post a Comment