Meneja Msaidizi Masoko wa Benki ya Exim Tanzania, Bi Anita
Goshashy (Watatu Kushoto) akikabidhi magodoro kwa Mganga Mkuu wa Hospitali
ya Rufaa ya Mwananyamala, Dkt. Sophinias Ngonyani (Kushoto). Wakishuhudia ni
Wafanyakazi wa Benki ya Exim. Benki ya Exim imetoa magodoro 60
katika Wadi ya Wazazi katika Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala jijini Dar es
Salaam mwishoni mwa wiki katika kuadhimisha Siku ya Mama Duniani. Wa kwanza kushoto
ni Muuguzi Kiongozi Sr. Tuswege Mwamwaja na Kulia ni Muuguzi Mkunga Bi.
Marietha Mwageni. (Picha na Mpiga Picha Wetu)
Na Mwandishi Wetu
BENKI ya Exim ya Tanzania imeadhimisha Sikukuu ya Mama
Duniani kwa kuchangia magodoro 60 katika wodi ya wazazi ya Hospitali ya
Mwananyamala iliyopo jijini Dar es Salaam katika kutoa heshima kwa kinamama
wote na kuunga mkono jitihada za kuboresha afya ya uzazi nchini.
Kwa sasa, Hospitali ya Mwananyamala ambayo ni hospitali
kubwa ya rufaa jijini Dar es Salaam inatoa huduma kwa wakinamama wanaotarajia
kujifungua zaidi ya 3100 kwa mwezi, ikiwa na vitanda 136 tu katika wodi hiyo ya
wazazi.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi magodoro hayo
hospitali hapo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Meneja Msaidizi Masoko
Bi Anita Goshashy alisema mchango huo ni moja kati ya utekelezaji wa shughuli
za benki yake zinazolenga kuisaidia jamii inayoizunguka.
“Mwaka jana, Benki ya Exim imeweza kufikia faida ya
shilingi bilioni 20, na tumekuwa na utamaduni wa kurejesha kile tukipatacho
toka kwa jamii. Sasa, leo hii tuko hapa Mwananyamala kukabidhi vitu hivi, ikiwa
kama njia ya kutambua mchango wa kina mama zetu na kuonyesha jinsi gani
tunaisaidia jamii inayotuzunguka kama benki,” alisema Bi. Goshashy, aliongeza
kuwa benki itaendelea kuipiga jeki jamii hususani katika sekta ya Afya,
Mazingira na Elimu.
Bi. Goshashy alisisitiza kuwa, “Leo hii tunakabidhi magodoro
haya ili kuweza kusaidia kuboresha uzazi uliosalama. Kina mama wengi
wanaotarajia kujigfungua ufariki wakati wakijifungua. Mchango wetu leo
utasaidia katika katika kuboresha hali hiyo hapa Hospitali ya Rufaa ya
Mwananyamala. Jitihada zetu hazitaishia hapa tutaendelea kufanyakazi karibu na
jamii inayotuzunguka.”
Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Dkt.
Sophinias Ngonyani aliipongeza Benki ya Exim kwa msaada huo, na kuongeza kuwa
msaada umewafikia kwa wakati muafaka na kuziasa taasisi nyingine za kifedha na
makampuni mengine nchini kuiga mfano huo.
“Kwa niaba ya Jamii ya Hospitali ya Mwananyamala, Ningependa
kuelezea shukrani zangu za dhati kwa hatua nzuri mliyoichukua kuweza kutusaidia
vitanda hivi ambavyo vitatumika kwa wakinamama ambao tunawathamini kwa kiasi
kikubwa maishani mwetu. Mchango huu utasaidia Jamii ya Mwananyamala kwa kiaasi
kikubwa sana,” alisema Dkt. Ngonyani.
Dkt Ngonyani alisema kuwa kadri ya serikali inapojitahidi
kuzipatia vifaa vituo vya afya, jitihada haziwezi kutoshereza mahitaji yote kwa
ujumla katika hospitali hizi, ndiyo maana kuna haja ya wadau wengine, hususani
makampuni kujitokeza na kuunga mkono jitihada hizo na kuweza kuleta mabadiliko
chanya katika sekta ya afya nchini.
“Nawapongeza kwa utekelezaji wenu mzuri wa sera yenu ya kufanya
shughuli za kijamii. Ombi langu kwa benki ni kwamba bado tunakumbana na
changamoto nyingi kama hospitali ya rufaa, Nawaasa msichoke kutupatia michango
yenu katika sekta hii nyeti iokoayo maisha ya watu wetu,” Dkt. Ngonyani
aliongeza.
No comments:
Post a Comment