Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij
amesema moja ya sababu za kikosi chake kupoteza mechi dhidi ya Msumbiji
(Mambas) ni wachezaji wake kucheza kwa wasiwasi katika kipindi cha kwanza.
Taifa Stars iliruhusu bao la kwanza
sekunde chache kabla ya kumalizika kipindi cha kwanza katika mechi ya marudiano
ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika kutafuta tiketi ya kucheza hatua ya
makundi iliyochezwa leo (Agosti 3 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa wa Zimpeto
hapa Maputo.
Bao hilo katika mechi hiyo iliyomalizika
kwa wenyeji kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, hivyo kusonga mbele kwa jumla ya
mabao 4-3 lilifungwa kwa kichwa na mshambuliaji Josemar Machaisse.
Nooij alisema wasiwasi katika
kipindi cha kwanza ndio ulioipa Msumbiji fursa ya kutawala mechi hiyo katika
kipindi hicho na kukimalizia ikiwa mbele kwa bao hilo la mshambuliaji huyo wa
klabu ya Bravos de Maquis ya Angola.
Alisema timu yake ilitulia kipindi
cha pili baada ya kumuingiza Amri Kiemba badala ya Khamis Mcha. Pia alilalamikia
bao ambalo Taifa Stars ilifunga dakika ya 16 kupitia kwa John Bocco lakini
likakataliwa na mwamuzi Dennis Bate kutoka Uganda.
Aliongeza kuwa mchezaji Elias
Pelembe aliyeifungia Msumbiji bao la pili dakika ya 83 kwa mpira wa adhabu nje
ya eneo la hatari ndiye aliyemaliza mchezo huo. Pia ni mchezaji huyo
aliyebadili matokeo ya mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam ambapo Msumbiji
ilisawazisha dakika tatu kabla ya filimbi ya mwisho.
Taifa Stars inayodhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager, na ambayo ilicheza vizuri kipindi cha pili ilipata
bao lake dakika ya 78 na Mbwana Samata kwa shuti la pembeni akiwa nje ya eneo
la hatari na kumshinda kipa Ricardo Campos.
Matokeo hayo yameipeleka Msumbiji
katika kundi C lenye timu za Cape Verde, Niger na Zambia. Mechi za hatua ya
makundi kutafuta tiketi ya kucheza fainali za Afrika zitakazofanyika mwakani
nchini Morocco zitaanza kuchezwa mwezi ujao.
Mechi hiyo ndiyo itakayoamua ni
timu ipi kati ya Tanzania na Msumbiji itakayoingia hatua ya makundi ya michuano
ya Afrika kwa ajili ya kutafuta tiketi za Fainali itakayofanyika mwakani nchini
Morocco.
Katika mechi ya kwanza iliyochezwa
jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita timu hizo zilitoka sare ya mabao
2-2. Timu itakayosonga mbele itaingia kwenye kundi lenye timu za Cape Verde,
Niger na Zambia.
Taifa Stars inarejea Dar es Salaam
kesho (Agosti 4 mwaka huu) saa 8 mchana kwa ndege ya Air Tanzania.
Kikosi cha Stars kilipangwa hivi;
Deogratias Munishi, Said Moradi, Shomari Kapombe, Kelvin Yondani, Nadir Haroub,
Erasto Nyoni, Mwinyi Kazimoto, Mcha Khamis/Amri Kiemba, John Bocco/Simon Msuva,
Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu/Mrisho Ngasa.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
MAPUTO
No comments:
Post a Comment