HABARI MSETO (HEADER)


August 11, 2014

Kinondoni kutoa Redd’s Miss Tanzania

Na Mwandishi Wetu

KUMEKUCHA! Miss Kinondoni anayemaliza muda wake, Lucy Tomeka, ametamba ni lazima mrembo wa Redd’s Miss Tanzania mwaka huu atoke Kinondoni.


Lucy alisema ana uhakika huo mkubwa kutokana na kuwaona washiriki wa Redd’s Miss Kinondoni na kuona wana vigezo vyote vya kulitwaa taji hilo.


Mrembo huyo ambaye atakabidhi taji la Redd’s Miss Kinondoni mwishoni mwa wiki alisema, ana uhakika huo kutokana na uzoefu alioupata wakati akishiriki Redd’s Miss Kinondoni.


“Taji lazima lirudi nyumbani, warembo wa Kinondoni kusema kweli wana sifa zote, wana kila aina ya sifa. Tena mwaka huu naona upinzani ni mkali zaidi kuliko miaka yote, kutokana na sifa ya warembo hao,” alisema Lucy.


Naye Mratibu wa Redd’s Miss Kinondoni, Husna Maulid, alisema warembo 20 wanatarajiwa kuchuana Ijumaa wiki hii ili kumpata mshindi kati yao.


“Ijumaa fitina yote inaisha, kinachosubiriwa ni siku tu na warembo 20 wapo katika mazoezi makali kwa ajili ya shindano hilo.”

Shindano la Redd’s Miss Kinondoni linatarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa Escape 1 uliopo Mikocheni, Dar es Salaam huku kukiwa na burudani kali toka Malaika Band inayoongozwa na Christian Bella.


Taji la Redd’s Miss Kinondoni kwa sasa linashikiliwa na Lucy Tomeka, ambaye naye alivikwa na aliyekuwa Redd’s Miss Tanzania, Brigitte Alfred.


Warembo wanaoshiriki shindano hilo wanatoka vitongoji vya Sinza, Msasani na Dar Indian Ocean, huku kiingilio kikitarajiwa kuwa Sh 10,000 kwa viti vya kawaida na Sh 30,000 viti maalumu.


Wadhamini wa shindano hilo ni Redd’s Original, Kitwe General Traders, CXC Africa, Jambo Leo, Clouds FM, Michuzi Media Group, Father Kidevu, Greaters Salon, EFM na Habari Mseto Blog

No comments:

Post a Comment

Pages