Na Mwandishi Wetu, TANGA
TIMU ya Coastal Union ya Tanga “Wagosi wa Kaya” kesho Jumapili itacheza mechi ya kirafiki na Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani ikiwa ni maandalizi ya msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania Bara ambao unatarajiwa kuanza Septemba 20 hapa nchini.
Akizungumza leo, Ofisa Habari wa Coastal Union,Oscar Assenga amesema maandalizi ya kuelekea mchezo huo yanaendelea vizuri na tayariwalishafanya mazungumzo na uongozi wa wakata miwa hao hivyo watawasili mkoani hapa siku moja kabla ya mchezo huo.
Assenga amesema kuwa mchezo huo utakuwa ni wa pili kwa timu ya Coastal Union kucheza ikiwa mkoani hapa baada ya kurejea kutoka Visiwani Pemba ilipokuwa imeweka kambi ya mwezi mmoja kwa ajili ya matayarisho ya ligi kuu soka Tanzania bara.
Amesema baada ya mchezo wa kwanza timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Polisi Morogoro hivyo waliona umuhimu wa mechi hiyo lengo likiwa kukipa makali kikosi hicho kabla ya kuwavaa wekundu wa msimbazi Simba siku ya ufunguzi wa Ligi kuu.
Ameongeza kuwa wanategemea mechi hiyo itakuwa na upinzani mkubwa sana hivyo wakazi wa Tanga na vitongoji vyake watumia fursa hii kuja kuiona timu yao ya Coastal Union ikipambana kwenye mchezo huo kabla haijaanza msimu mpya wa ligi kuu Tanzania bara
Hata hivyo amesema kuwa msimu huu timu hiyo imepania kuhakikisha inafanya vizuri katika mechi zake za nyumbani na ugenini ili kuweza kuchukua ubingwa wa Ligi kuu Tanzania bara.
No comments:
Post a Comment